Sambaza....

Afisa Habari wa klabu ya soka ya Yanga Dismas Ten amesema maandalizi kuelekea katika mchezo wao wa Ligi dhidi ya Mbeya City yanaendelea vizuri na kwamba Kati ya wachezaji 20 ambao wamesafiri na timu hakuna ambaye anamajeraha yatakayomuweka nje ya mchezo huo.

Ten amesema kikosi chao kimesafiri salama na kimefika jijini Mbeya wakiwa na ari ya kushinda Ili kuendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara ili kurejesha taji mikononi mwao.

“Asubuhi daktari amefanya vipimo kwa wachezaji wote na amesema kwamba katika wachezaji 20 waliokuja hakuna ambaye anatatizo kwa maana kwamba wote wapo vizuri na wana ari ya mchezo, ni imani yetu kwamba tutapambana ndani ya dakika 90 kutafuta matokeo na kuifanya timu kupata alama tatu na kuzidi kuendelea kukaa kileleni,” amesema.

Amesema wanaendelea kuamini kuwa hakuna timu ambayo inajiandaa kupoteza mchezo na ndio maana wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa wanawaheshimu wapinzani wao ambao ni Mbeya City kama timu nzuri ambayo inaweza kuleta changamoto.

“Kama ambavyo Mwalimu wetu amekuwa akisisitiza, lengo letu ni kushinda katika kila mchezo, tunahitaji kupata alama tatu, tupo kwenye mbio za kutafuta ubingwa, tuliuazimisha msimu uliopita kwa hiyo mara hii tunahitaji kuurejesha Ili kuendelea kuandika rekodi ya kuchukua ubingwa Mara 28,”ameongeza.

Ten ameendelea kuwashukuru mashabiki wa Yanga ambao wameonesha kuichangia timu yao, amesema wao Ndio wamewezesha timu kusafiri kuelekea jijini Mbeya, aidha njia pekee ambayo Wanaweza kuwalipa ni kupata matokeo mazuri kwenye michezo yote iliyopo mbele yao.

Yanga watacheza na Mbeya City Jumamosi hii kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ukiwa ni mchezo mwingine wa Ligi kuu soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2018/2019.

Sambaza....