Ligi Kuu

Macho yangu yanamkubali Djuma, Masikio yangu hayamkubali Julio

Sambaza....

Vipo vingi sana ambavyo hatujavipata na tunahitaji kuvipata ili kufikia sehemu ambayo tunaitaka. Tunataka mafanikio, mafanikio ni vigumu kuyapata kama hakuna mtu wa kuyajenga mafanikio haya.

Kimsingi katika mafanikio ya mpira wajenzi ni wengi sana wanaohitajika ili kukamilisha hekalu letu la mpira wa miguu. Kuna wakati vidole vyetu viliimba sana kuhusu maendeleo ya soka la vijana.

Kila aina mstari tuliuchora ili tu wahusika wakuu waelewe, tuliandika kwa kuwabembembeleza na kuwaonesha namna ambavyo wanaweza kuanza, maneno yetu yalikuwa matamu sana mpaka yakawa burudani masikioni mwao burudani ambayo iliwaletea usingizi mkubwa machoni mwao.

>>Haukuwa muda sahihi kwa Pierre kuja Simba

Tulipoona mboni za macho yao zimefumba, tulipiga kelele ili wafumbue macho, walipofumbua macho tuliongea kwa ukali na kuwakumbusha kuwa jua la jioni halimsubiri mtu.

Mbele yao hawakuona hatari ya giza, usingizi ulikuwa mzito sana kwenye mboni za macho yao. Waliamua kutembea huku wakiwa na usingizi mzito machoni mwao.

Usingizi ambao uliwafanya wasiwaze vizuri namna ya uendeshaji mzuri wa mpira wetu, ndiyo maana ligi yetu mpaka sasa hivi haina ushindani.

Ushindani ambao haupo hata kwenye biashara za nje ya uwanja kwa timu husika na wachezaji wetu. Hakuna timu ambao inafanya biashara kwa ukubwa na kwa umakini kwa kutumia nembo ya timu. Hata majina ambayo wachezaji huyatengeneza uwanjani hayawanufaisha kibiashara nje ya uwanja.

Mshahara na posho za kuunga unga ndiyo tegemeo kubw a kwao, hawafikiri jinsi ya kuongeza njia mbadala ya kuingiza pesa na hili tushaimba sana, tukaandika sana mpaka vidole vidole vyetu vikaumia lakini hatukuwai kuacha kuandika kwa sababu tunatamani kufika pale juu.

Juu penye kila aina raha, raha ambayo inatokana na juhudi za mapigano yetu ya mafanikio yetu, mafanikio hayawezi kuja bila weredi kuwa ndani yake.

Julio

Kwetu sisi weredi tumeufunika kaniki, hauonekani tena, hauna umuhimu tena ndiyo maana tunafanya vitu vingi kwa mazoea yale yale ya jana. Hatujawahi kuwaza leo mpya na mbinu mpya mikononi mwetu.

Ndiyo maana tunaamini watu wanaoongea kwa kufurahisha kuliko wanaotenda kwa kufurahisha. Watu kama Masau Bwire ni muhimu sana katika mpira wetu kuliko mtu anayeongea kwa vitendo.

Na wakati mwingine tunaamini maneno hujenga timu imara kuliko ujuzi bora wa kocha ndiyo maana kuna wakati Mtanzania atasimama kumsifia Julio na kumkataa Masoud Djuma.

Hawa ni watu wawili tofauti, mmoja anatoka sayari ya Mars mwingine anatoka sayari ya Venus na kinachowatofautisha ni mstari wa weredi.

Hata ukiwasikiliza wanavyoongea na vyombo vya habari ni rahisi sana kugundua hawa watu siyo wa baba na mama mmoja , mmoja ni kocha wa kandanda na mwingine ni kocha wa mpira.

Djuma kwenye moja ya mikutano na waandishi wa habari.

Masoud Djuma ataongea kwa ufundi kilichotokea uwanjani, madhaifu ya timu yake wapi ilikwamba wapi ilikuwa bora na mwisho wa siku atamsifia mpinzani wake (huu ndiyo msingi wa weredi wa kazi yake ) lakini Julio ataongea siasa zilizotokea uwanjani hutomsikia akielezea ubora wa timu yake zaidi ya yeye kujisifia, hutomsikia akiongea ubora wa mpinzani wake na kumsifia mpinzani wake zaidi ya yeye kumponda refa.

Hapa ndipo tulipo sisi , hata uchaguzi wa maneno anapozungumza na waandishi wa habari hatilii maanani haoni chochote kile huzungumza.

Ndiyo utofauti wetu na wao, unaanzia kwenye akili ndiyo maana wao hujifunza kila siku sisi hukaaa na kulalamika kila siku ndiyo maana hatuendelei katika sekta yetu ya makocha.

Hakuna anayeona haja ya kujifunza kila siku mbinu mpya za kisasa za mpira, hakuna mwenye taarifa ya mabadiliko ya kimbinu katika mpira kwetu sisi kila kitu ni sawa na tunaonekana kupata kila kitu kwa bahati mbaya ndiyo maana Masoud Djuma anakuja hapa na sisi tunabakia hapa hapa.

Wengi wetu hatufikirii kubadilishana nao, wakati wao wakija kwetu sisi tuwe tunaenda kwao.

Tumekuwa na makocha ambao wengi ambao hawana udhubutu wa kwenda nje kufundisha au wakijifunza vitu vipya kila siku badala yake vyeti vyetu vya ukocha vinaozea makabatini.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x