Blog

Manara mchezaji wa 13, mchezaji muhimu Simba

Sambaza....

Hajawahi kuvaa jezi au njumu na kuingia kwenye uwanja kwa ajili ya miguu yake kuipigania Simba kwenye mechi ya aina ya yoyote.

Hajawahi kufanya hivo hata siku moja kwa sababu tu hana uwezo wa kufanya hivo. Baba yake alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kucheza mpira wa miguu.

Na ni moja ya wachezaji bora kuwahi kutokea katika historia yetu ya mpira wa miguu hapa Tanzania. Historia ya mpira wetu inamkumbuka kwa hilo.

Huyu ndiye alikuwa anauwezo wa kuitumia miguu yake vizuri ili tu aiwakilishe au kuitetea timu yoyote ambayo alikuwa anaitumikia.

Huyu ndiye alikuwa na uwezo wa kuunda idadi ya wachezaji 11 muhimu ndani ya uwanja na kuifanya timu ipate matokeo ambayo ni chanya.

Kumekuwa na daraja kubwa sana ambalo linawatenganisha Haji Manara na Sunday Manara!. Daraja la kimajukumu.

Wote wanautumikia mpira lakini tofauti yao ni moja tu, baba aliwahi kuutumikia mpira kwa kutumia miguu yake ya adhabu, miguu ambayo iliitwa Computer.

Wakati mwanae Haji Manara anautumikia mpira wa miguu kwa kutumia mdomo wake. Yani mdomo wake kaufanya kama kiungo muhimu katika upatikanaji wa matokeo chanya ya klabu ya Simba.

Unaona utofauti uliopo hapo?, safi !, sasa huwezi kubeza hata siku moja uwezo wa Haji Manara kwenye hili hata kama hatumii miguu yake kuipa matokeo chanya timu yake.

Mdomo wake umekuwa silaha nzito sana katika upatikanaji wa matokeo ya klabu ya Simba. Kwa kifupi huyu ndiye mchezaji wa kumi na tatu wa Simba!.

Kuna ule msemo kuwa timu huwa na wachezaji kumi na mbili. Kumi na moja ambao huwa wanakaa uwanjani na kuucheza mpira .

Na mchezaji wa kumi na mbili ni yule ambaye huwa anakaa jukwaani kwa ajili ya kumshangilia, kumpa nguvu yule ambaye yuko uwanjani kwa ajili ya kucheza.

Lakini kwa Simba na kuna mtu muhimu anaongezeka, mchezaji wa kumi na tatu ambaye ni Haji Manara.

Huyu anauwezo mkubwa wa kumuunganisha mchezaji wa kumi na mbili ni wale wachezaji kumi na moja waliopo uwanjani na kuwa kitu kimoja.

Kwanini nasema hivo ?, Haji Manara amekuwa mtu ambaye ni kiungo kikubwa cha kuwashawishi mashabiki wa Simba waje uwanjani bila uoga.

Haji Manara haogopi kuwaaminisha mashabiki wa Simba kuwa timu yao ni bora na wanatakiwa waje uwanjani kwa ajili ya kuiunga mkono.

Haji Manara amewaaminisha mashabiki wa Simba kuwa klabu ya Simba ni kubwa na yenye thamani kubwa kuzidi klabu yoyote Afrika Mashariki na wanatakiwa kujivunia kwenye hilo.

Na hiki ndicho huwa wanakifanya. Watajivunia sana. Watatembea kifua mbele kwa kuamini wao ni bora na wenye thamani kubwa kuzidi yoyote yule.

Na huwezi kuwabadilisha kwenye hilo. Na ndiyo maana mechi zao za kimataifa hujaza mashabiki wengi sana.

Mashabiki ambao huwa wanahamasika sana kuipa nguvu timu yao. Nilikuwa natazama mechi dhidi ya As Vita.

Dakika za mwishoni mashabiki wa Simba walisimama kwa pamoja na kuanza kumshangilia Simba kuwa nguvu kwa kuimba SIMBA, SIMBA, SIMBA.

Ni muda ambao ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 1-1. Mashabiki wa Simba waliwakumbusha wachezaji wao kuwa wako kwenye klabu ya thamani.

Wanatakiwa kuzidi kuionesha thamani yao kama ambavyo msemaji wao husema. Wanatakiwa kuibuka mashujaa.

Waliwakumbusha kuwa wanauwezo wa kuibuka mashujaa kwenye hiyo mechi. Mwisho wa siku wachezaji wa Simba walipigana sana dakika za mwisho bila kukata tamaa na wakafanikiwa kuibuka na ushindi.

Hapa nilikuwa na mawasiliano makubwa sana kati ya mashabiki wa Simba na wachezaji wa Simba. Mawasiliano ambayo yalisababisha wao kukumbushana umuhimu wa thamani ya klabu ya Simba.

Mawasiliano haya yameunganishwa vizuri na Haji Manara. Huyu ambaye alitumia kinywa chake kuwapa nguvu wachezaji wa Simba kuwa watachukua alama zote Tisa kwenye uwanja wa nyumbani.

Huyu ambaye kila uchwao alikuwa anawasisitiza mashabiki wa Simba waje kwa kujiamini kuwa watabeba hizo alama zote tisa.

Huyu ambaye alikuwa anawaambia watu kuwa Simba ni klabu yenye thamani kubwa sana hivo kila mtu apiganie thamani ya klabu (mashabiki na wachezaji ).

Umegundua kitu hapo ?, huyu ndiye mchezaji wa kumi na tatu wa Simba na ndiye mchezaji muhimu ndani ya Simba kwa sasa!.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.