Sambaza....

Kocha wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya Umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) Oscar Mirambo ameushukuru Uongozi wa vyama vya soka ukanda wa Kusini kwa Afrika (COSAFA) kwa kuwaalika kushiriki mashindano ya Vijana ambayo Leo yanaingia hatua ya nusu fainali.

Mirambo amesema lengo lao ilikuwa kucheza mechi nyingi za kirafiki ili kujiweka tayari kwa ajili ya mashindano ya Afrika ambayo yatafanyika mwakani na Tanzania watakuwa wenyeji, hivyo kualikwa katika mashindano hayo imekuwa ni sehemu nzuri kwa wao kupata uzoefu wa mechi za kimataifa.

“Tunashukuru kwa kupata nafasi ya kushiriki kwenye haya mashindano, tunawashukuru watu wa COSAFA kwa kutualika imekuwa ni “platform” nzuri kwetu sisi kupata uzoefu katika michezo ya kimataifa,” amesema.

Akizungumzia mashindano hayo Mirambo anasema yamekuwa mazuri na ya ushindani pia wanafurahi kuona wamefika hatua ya nusu fainali Licha ya kuanza vibaya, kwani kwa kufika hatua hiyo wametimiza lengo lao la kucheza mechi nyingi za Kimataifa.

“Mashindano yamekuwa mazuri sana, japo hatukuanza vizuri tunashukuru Mungu tumeweza kurekebisha kile ambacho kilitukwamisha kupata matokeo kwenye mchezo wetu wa kwanza, leo tunaenda kucheza nusu fainali dhidi ya Zambia,”

“Tunafurahi kuona tumefanikisha malengo yetu kwa asilimia 100, lengo letu kuja kwenye haya mashindano lilikuwa kucheza idadi kubwa ya mechi ni faraja kwamba mpaka yatakapokuwa yameisha tutakuwa tumecheza michezo mitano…… Sasa tunaenda kucheza Nusu fainali na Zambia, ni timu kubwa, ni timu ambayo ina uzoefu mkubwa kwenye soka la vijana, tunategemea kupata ushindani mkubwa,ila matamanio yetu ni kufanya vizuri na kuingia fainali,” amesema.

Katika Mashindano hayo ya AUSC Region 5 Tanzania ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Angola, kabla ya kuzinduka na kuichapa Malawi 2-1 na baadae kuichapa Afrika Kusini 2-0 na kukata tiketi ya kucheza na Zambia kwenye nusu fainali mshindi atakutana na eSwatini au Angola katika fainali.

Sambaza....