Zamani

Mkasa wa Luis Figo kurushiwa bichwaa la nguruwe!

Sambaza....

Kati ya vipindi ambavyo huvuta hisia za mashabiki wa soka ni wakati wa usajili wa wachezaji. Katika kipindi hiki lolote linaweza kutokea na ukajikuta unalala na viatu.

Binafsi nililala na viatu kwenye dirisha la usajili la kiangazi la 2012. Sikuwahi kufikiria kwamba Robin Van Persie angeondoka Arsenal ghafla msimu ule, mbaya zaidi akatua kwa mahasimu wetu Manchester Utd. Mashabiki wa Gunners haikutupendeza ile, jamaa tulikuwa bado tunamhitaji sana!

Robin Van Persie akitambulishwa na Sir Alex Furgeson kuwa mchezani mpya wa United.

Narudia! kipindi cha usajili lolote linaweza kutokea ukabaki unaduwaa!

Mashabiki wa Liverpool hawana hamu na usajili wa dirisha dogo la Januari la 2011, walishuhudia mshambuliaji wao hatari Fernando Torres akiwaacha kwenye mataa na kutimkia Chelsea. Iliwauma sana na mabango ya kumuita Yuda walibeba.

Fernando Torres akitambulishwa na Chelsea.

Sasa turudi kwenye topic yetu ‘Mkasa wa Luis Figo kurushiwa bichwa la nguruwe’. Hili halina ubishi kwamba Luis Figo ni kati ya wachezaji bora na staa kuwahi kutokea. Kwa walioanza kufuatilia mpira zamani hasa ile miaka ya 2000 wanamjua vizuri fundi huyu kutoka Ureno ambaye ndiye mchezaji bora wa dunia mwaka 2000.

Dirisha la usajili la kiangazi la 2000 lilishuhudia Figo akihama kutoka Barcelona kwenda kwa mahasimu wao wakubwa Real Madrid, kipindi hicho Figo alikuwa hashikiki! Mashabiki wa Barcelona hawakuridhia kuondoka kwa Figo waliyekuwa wanampenda na kumtegemea, walimuona msaliti.

Luis Figo.

Mziki ulikuja kutokea miaka miwili baadae kwa mara ya kwanza Figo aliporejea Nou Camp tarehe 23 Novemba 2002 katika mechi ya El Clasico iliyomalizika kwa suluhu. Takribani mashabiki 100,000 wa Barca walionyesha chuki ya wazi wazi dhidi yake. Walimzomea kila alipokuwa na mpira. Figo ambaye alikuwa na jukumu la kupiga kona, kila akienda kwenye kibendera mashabiki walimrushia vitu mbalimbali akiwemo chupa.

Luis Figo katika Dimba la Camp Nou.

Vitu vingi vilirushwa lakini ambacho kimebaki kwenye historia ni bichwa la nguruwe alilorushiwa Figo na mashabiki wa Barcelona wakionesha hasira yao kwake kwa kuondoka Barca na kujiunga na mahasimu wao Real Madrid.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.