Sambaza....

Kikosi cha soka cha Mtibwa Sugar kimeondoka Jumapili hii kutoka katika mashamba ya Miwa Turiani mkoani Morogoro na kuelekea mkoani Mbeya ambapo siku ya Januari 8, 2019 watacheza mchezo wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.

Afisa habari wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru Ligalambwike amesema msafara umeondoka ukiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo, ukizingatia mchezo uliopita waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC.

Amesema pia kutokana na matokeo ya hivi karibuni kwa timu zote mbili kunazidi kuwapa morali ya kupambana ili kuibuka na ushindi katika mchezo huo na kujaza kibaba chao cha alama kwenye msimamo wa ligi kuu.

“Kikosi kimeondoka kikiwa na matumaini makubwa, tumetoka kuifunga timu ngumu ya Azam, lakini pia ukiangalia matokeo ya hivi karibuni Tanzania Prisons wamekuwa wakisuasua sana, tunavijana wachanga ambao wanaweza kutupatia alama tatu kwenye mchezo huo, ni hakika toka tumetoka kwenye mashindano ya Kimataifa tumekuwa na nguvu ya kupambana ili kurudisha hadhi yetu,” amesema.

Michezo ya mzunguko wa kwanza kikosi cha wana tam tam kiliibuka na ushindi katika michezo yote miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City, mchezo wa Tanzania Prisons wana tam tam waliibuka na ushindi wa goli 1-0 likifungwa na Stamil Mbonde na mchezo wa Mbeya City wana tam tam waliibuka na ushindi wa goli 2-1 magoli ya wana tam tam yakifungwa na Stamil Mbonde na Ismail Mhesa kwa upande wa wana tam tam na Erick Kyaruzi (Mbeya City).

Aidha alipouliza kama wamekata matumaini ya kutwaa ubingwa kutokana na tofauti ya  alama ambazo wanazo na Yanga SC, Kifaru amesema “Bado tunaweza kutwaa ubingwa, tumecheza mechi chache kuliko Yanga, pia tunakikosi kizuri ambacho kinauwezo wa kushinda kila mchezo, hata Yanga kuna mahala watateleza au Simba au Azam nasisi tutapenyea hapo,” amesema.

Mtibwa Sugar ‘WanaTam Tam’ wana alama 26 wakiwa katika nafasi ya sita baada ya kucheza michezo 15 msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania Bara.

Sambaza....