Blog

Mtoto wa kishua anaefanya Kandanda kuonekana mchezo mwepesi

Sambaza....

Kama upo karibu na mkongwe yeyote hapo jirani muulize kuwa aliitizama fainali ya kombe la dunia mwaka 1994, kati ya Brazil na Italy ambayo Brazil walishinda kwa matuta? Akijibu ndio muulize tena anamkumbuka Iomar do Nascimento ‘Mazinho’? kama anamkumbuka basi soma makala hii kwa heshima yake.

Mwambie yule Mazinho wakati anacheza fainali ile pale Rosa Bowl California alikuwa na mtoto mmoja aitwaye Thiago Alcântara aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu ambaye miaka 26 baadae anakuja kuisimamisha dunia yote na kumtizama.

Ndio ni yule jamaa aliyepigiga pasi nyingi kwa ukamilifu dhidi ya Barcelona wakati Bayern Munich wanaibuka na ushindi wa bao nane kwa mbili na kuiondosha kwa fedheha Barca iliyoongozwa na nahodha Messi.

Thiago Alcantara

Mtoto mmoja wa kishua, kwao maisha si haba kwani Baba yake alitengeneza fedha toka kitambo kupitia soka huku mama yake alivuna matunda kadhaa kwenye mpira wa wavu ‘Volleyball’ ambapo alicheza kwa mafanikio hivyo Thiago haijui njaa.

Wakati vijana wengi wakitafuta ajira na kazi kwa udi na uvumba nchini Brazil na Hispania Thiago yeye alikua hajali na kuamini kwenye soka kuliko kazi nyingine japo uwezo wa kuzipata ulikuepo kulingana na Baba yake kuwa mzee mwenye utajiri wa kutosha.

Flamengo ya Brazil, Galacian na kelme CF za Hispania ni timu alizozichezea akiwa mdogo kabla ya kujiunga na akademi ya La Masia pale Barcelona. Kwaufupi Thiago ni chotara wa Kibrazil na Kihispania aliyeamua kuchagua Utaifa wa Hispania kwani ndiko sehemu aliishi kwa muda mrefu.

La masia pale alicheza kwa mafanikio huku akifananishwa na wakongwe kama Eidur Gudjohnsen na Yaya Toure ambapo mwaka 2019 alianza kuichezea timu kubwa ya Barcelona kwa mafanikio. Mwaka 2013 aliihama Barcelona na kwenda nchini Ujerumani ambapo alijiunga na wababe Bayern Munich anakokiwasha mpaka leo.

Wakikuuliza ana umri wa miaka mingapi wajibu 29, wakiuliza anacheza namba ngapi waambie eneo lolote la kiungo na wakihoji kuhusu kiwango chake wakumbushe mechi ya Bayern Munich dhidi ya Barcelona mwaka huu wakisema hawakuitizama waambie wasiteseke Thiago ni yule jamaa aliyesimama dimba la kati fainali ya UEFA Jumapili iliyoisha na kuwanyima ubingwa PSG yenye Mbappe na Neymar.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.