Ligi Kuu

Mzamiru wa Mtibwa Sugar katika jezi za Simba

Sambaza....

NIMEWAHI kumuona Mzamiru Yassin katika jezi za Mtibwa Sugar. Alikuwa kiungo mahiri. Eneo lake Mtibwa Sugar walikuwa na utitili wa viungo.

Walikuwepo Mohamed Ibrahim ‘MO’, Mussa Nampaka, Shaban Nditti, lakini timu ilicheza kwa kumzunguka Mzamiru. Shiza Kichuya alikuwa staa, lakini hakuwahi kufanya kazi za Mzamiru wakati ule wako pamoja Mtibwa Sugar.

Mzamiru yule wa Mtibwa Sugar siku hizi nimeanza kumuona tena katika jezi za Simba. Siku zake za kwanza na Simba aliifanya kazi hii vyema, lakini katikati kidogo akaja kupotea. Sasa hivi ameibuka upya. Anafanya kazi kweli kweli.

Anafanya kazi kubwa katikati mwa uwanja. Anapora, anatembea sana kiwanjani. Kama tungekuwa na michoro inayoonyesha sehemu za kutembea kiwanjani, Mzamiru ndiyo angekuwa amechora eneo kubwa katika michezo ya Simba.

Changamoto kubwa aliyonayo mashabiki hawajawahi kumuelewa. Awe na jezi za Taifa Stars awe na jezi za Simba hawamuelewi. Sijui kwanini hawamuelewi. Mara nyingi wanamuona kama kiungo wa hovyo anayecheza kwa kupendelewa na makocha. Hawaoni mchango wake.

Ni mara chache kukuta kundi la mashabiki limesimamia sehemu moja kumkubali Mzamiru. Ni mara chache kuliona hili, lakini kuona kundi hilo limegawanyika kuhusu kiwango chake ni kawaida.

Kazi hii anayoifanya Mzamiru, ingesifiwa kama ingekuwa inafanywa na baadhi ya wachezaji wengine. Kila siku tungesikia wakimwagiwa sifa. Lakini kwa Mzamiru ni kama hana anachokifanya. Nasikia mwenyewe hajali sana jinsi anavyochukuliwa na watu. Anajali anachokifanya.

Katika timu yenye utajiri wa viungo mahiri, lakini bado nafasi yake iko kikosini. Kibaya zaidi Mzamiru wa leo anacheza timu moja na kina Meddie Kagere, Ibrahim Ajib, Cletus Chama, Gelson Fraga. Ni ngumu sifa ya moja kwa moja kumfuata aliko.

Kupata nafasi ya kucheza katika eneo la kiungo Simba kwa sasa si kazi ndogo. Ni kazi ngumu inayowashinda watu wengi. Rafiki yangu Said Ndemla ni moja wao. Muda mwingi Ndemla amekuwa mpenzi mtazamaji jukwaani au benchi.

Lakini Mzamiru amekuwa mchezaji anayecheza na kufanya kazi kubwa, lakini hatajwi sana vinywani mwa mashabiki. Ndemla asiyecheza mara nyingi na Mzamiru anayecheza mara nyingi, lakini mashabiki wanampenda Ndemla. Huwaambii kitu juu yake. Muda mwingine wanapenda wamuone akiwa katika timu yao bila kutumika. Inatokea katika maisha.

Mzamiru

Kazi hii anayoifanya Mzamiru leo, haijaja katika njozi. Kuna kitu cha ziada amekifanya katika viwanja vya mazoezi. Kitu hicho marafiki zangu wengi hawana. Kibaya zaidi hawataki hata kujifunza.

Siku ambayo Mzamiru atakosekana katika kikosi cha Simba kwa michezo kadhaa, tunaweza kukaa mbele ya luninga zetu na kuziona Simba mbili tofauti. Tutaiona Simba yenye Mzamiru ndani yake na tutapuuza kama tunavyopuuza sasa, lakini tutaiona Simba iliyomkosa Mzamiru, kisha tutajua Mzamiru ni mwanaume wa kiwango gani.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.