Ligi Kuu

Nagwanda imenifanya nione kesho ya Simba Sc

Sambaza....

Ndiyo mabingwa watetezi, tena ubingwa ambao walichukua kwa ustadi mkubwa kuanzia nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja.

Walihakikisha wanasajili kikosi imara, chenye nyota wengi mpaka kikawa kinaitwa kikosi cha bilioni 1.

Inasemekana lakini kikosi chao cha msimu uliopita kiligharimu bilioni 1!.

Watu wengi walitegemea mpira wa bilioni moja, kuanzia chenga ziwe bilioni moja, pasi, kukaba, magoli na ushindi ulitakiwa uwe wa bilioni 1.

Simba ilijitahidi sana msimu jana kuhakikisha bilioni 1 inaonekana vizuri uwanjani.

Wachezaji walicheza soka la kuvutia, na timu ilihakikisha inafunga magoli mengi, magoli ambayo yalikamilisha maana halisi ya neno “bilioni 1”.

Mashabiki hawakuwa na kelele, hawakuwa na ugomvi wowote na viongozi, wachezaji mpaka benchi la ufundi kwa sababu waliona kile ambacho kilikuwa kinasemwa kuwa Simba ina kikosi cha bilioni 1 tena imara!.

Hapo ndipo furaha yao ilipokamilika, hawakuwa na uwezo wa kujiingiza kwenye dunia ya huzuni wakati timu yao ilikuwa inatoa sababu nyingi kwa mashabiki kutabasamu.

Hii ndiyo furaha ya shabiki , yeye umpe ushindi tu ! , umwambie ukweli tu na atatembea na ukweli wako!, usimdanganye hata kidogo.

Kama kuna mkate mpe mkate na mweleze sababu kwanini umemnunulia mkate yeye atakuelewa na ataridhika.

Kitu kibaya kwao ni pale unapowaletea dagaa kwa kuwadanganyishia kuwa no samaki!, hawatakuelewa hata siku moja.

Hapo ndipo maisha yako ndani ya timu kama kiongozi yanapokuwa magumu kwa sababu shabiki atakuwa na mgandamizo mkubwa kwako akitaka matokeo kulingana na kitu ambacho umekuwa ukimwaminisha.

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakiaminishwa vitu vingi sana hasa hasa kabla ya msimu mpya kuanza.

Uongo mtamu ulianzia kwa viongozi kusajili wachezaji ambao kwa macho ya nyama walionekana ni wachezaji bora.

Wakawakuza, wakawaimba tena kwa mashairi mazuri, matamu na yenye kuvutia kuwa tumesajili kiungo hatari, beki wa miguu saba, na mshambuliaji kutoka sayari ya Mars.

Wataongea vyote hivi ili wawafurahishe mashabiki na washike imani kwa mashabiki , kwa kifupi usajili ambao ulifanyika katika kikosi cha Simba ilifanyika kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki ndiyo maana hata kocha mkuu wa sasa Patrick Assumes hakuhusishwa kwenye suala la usajili.

Aliletewa wachezaji, bila kujua hitaji lake na mashabiki wakazidi kuaminishwa na ziara ya nchini ya Uturuki.

Wengi waliamini kambi ya Uturuki itakuwa na matunda mengi, itaifanya timu ioneshe kiwango kikubwa.

Itaifanya timu iwe katika kiwango kikubwa ambacho kila timu itakuwa inaiogopa Simba.

Hiki ndicho kilichokuwepo katika akili ya wanaSimba wengi, ndiyo maana walikuwa na hamu ya msimu uanze.

Kwao wao waliamini kila mechi itakuwa haina ugumu kwao kwa sababu inakikosi imara na bora, wale wachezaji wa bilioni 1 walikuwepo na wakaongezewa wengine kina Meddie Kagere.

Hapa ndipo imani kubwa juu ya timu ilipokuwa. Kila mtu akawa anasubiri ushindi wa kutisha kutoka kwa Simba.

Hawakutegemea ushindi mwembamba hata kidogo kwa sababu kikosi chao kimegharamikiwa kuzidi timu yoyote ikizingatia ndiyo kikosi ambacho kiliweka kambi ulaya!, hakuna timu iliyofanya hivo zaidi ya Simba pekee.

Kwa kifupi vitu vyote hivi vilijenga imani kubwa sana kwa mashabiki wengi wa Simba kuwa timu hii itakuwa tishio na haitopata alama katika mazingira magumu.

Hakuna kitu kibaya kama kuwa na mategemeo makubwa, hapa ndipo mashabiki wa Simba walipokosea, kuwa na matumaini makubwa!.

Matumaini ambayo mara nyingi huja na maumivu kipindi ambacho matokeo huja tofauti na kile ambacho mtu alikuwa anakitegemea.

Na kitu kibaya zaidi mashabiki wengi wa mpira hawana uvumilivu hata kidogo!, kwao hakuna neno “kesho” kwenye akili yao neno “Leo” limetawala kwa kiasi kikubwa.

Hawataki kuona matokeo mazuri kesho, kesho ni mbali sana kwao , hutaka kuona matokeo leo tu.

Hawana subira hata kidogo!, hawakuambwa hivo, ndiyo maana matokeo yaliyotokea Nangwanda yamenifanya nione kukosa uvumilivu wa mashabiki wa Simba.

Sidhani kama wataendelea kuvumilia kuona timu yao ikipata matokeo katika hali ya kuhangaika wakati wanaamini wana kikosi kikubwa, bora, imara na chenye gharama kubwa kuzidi timu yoyote.

Mikono yangu inatamani sana kuwashauri kuwa kitu bora na imara hakijengwi kwa siku moja lakini kila nikikumbuka kuwa mashabiki wa mpira ni viumbe tofauti na viumbe wengine, ni viumbe ambao hawana uvumilivu hata chembe ndipo hapo mwanga wa Kesho ya Simba unapenyeza katika mboni zangu.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x