Stori

Ni April ya Wacongo Watupu, Wataamua Wenyewe.

Sambaza....

Naam April 16 iliyokua inasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa Kandanda nchini na Afrika kwa ujumla imefika na sasa kinachosubiriwa ni nyasi za Benjamin Mkapa kuamua ni Simba ama Yanga ataibuka kinara au ni sare kama mchezo wa raundi ya kwanza.

Kitu kizuri kuelekea mchezo huo ni kwamba timu zote zinaingia katika mchezo huo zikiwa katika fomu nzuri kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata katika michezo ya mwisho na kizuri zaidi ni jinsi washambuliaji tegemeo wa timu hizo wakiingia katika mchezo huo wakiwa katika kiwango cha juu kabisa.

 

Simba wametoka kumpa bao tano Ihefu katika FA na bao mbili katika Ligi huku Jean Baleke akifunga mabao katika mechi zote mbili wakati Yanga wao wametoka kumfunga Geita Gold bao moja na Kagera Sugar bao tano na michezo yote hiyo Fiston Mayele akiingia kambani.

Kwenye Ligi Kuu ya NBC Fiston Mayele ana mabao 16 na ndie kinara wa ufungaji wakati Jean Baleke ana mabao saba akianza kucheza January baada ya kujiunga na Simba katika dirisha dogo.

Wawili hawa wakiwa Congo Fiston Mayele akitokea AS Vita na Jean Baleke akiwa TP Mazembe ni Jean Baleke ndio aliibuka kinara wa ufungaji mabao akimzidi bao moja Mayele kwenye msimu wa mwisho walipocheza wote. Lakini sasa wawili hao wamehamishia vita yao nchini Tanzania na watakutana katika Dabi ya Simba na Yanga kesho Jumapili huku kila mmoja akiwa yupo moto katika ufungaji mabao.

Jean Balake akifunga mbele ya mlinzi wa Mtibwa Sugar

Ni wazi Wanamsimbazi wataingia kwa matumaini katika mchezo huo wakiwa na imani na kiwango kizuri kinachooneshwa na Jean Baleke katika ufungaji mabao. Baleke ameonyesha uwezo mkubwa sana katika kufumania nyavu za wapinzani akiipatia faidi Simba katika ufungaji baada ya kuumia Moses Phiri aliyekua tegemeo.

Baleke amekua akifunga mabao akiwa anajua jinsi ya kukaa vyema kwenye eneo la hatari akiwakimbia mabeki na kukaa eneo sahihi la kufunga. Zaidi ni jinsi ambavyo anatumia miguu yote katika kufunga na pia ni mzuri katika mipira ya juu, amekua na uwezo mkubwa wa kupiga kichwa na kufunga.

Fiston Kalala Mayeye kwasasa ni kama amewazoea Simba kwani ameshawafunga mabao matatu katika michezo miwili ya Ngao ya Jamii lakini ana deni katika Ligi Kuu kwani hajawahi kuifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu.

Fiston Mayele akipiga mpira na kufunga mbele ya walinzi wa Real Bamako.

Wananchi hawana shaka wala wasiwasi juu ya uwezo wake kwani wanamfahamu vizuri na alichokionyesha katika msimu wa mwaka jana ikiwa ni msimu wake wakwanza nchini licha ya kukosa ufungaji bora. 

Hakika mchezo wa keshi licha ya uwepo wa kina Aziz Ki, Kenedy Musonda na Benard Morrison kwa Yanga na Clatous Chama, Pape Sakho na Moses Phiri lakini bado matumaini na macho ya Wanakandanda yanabaki wa washambuliaji wawili kutoka Congo Jean Baleke na Fiston Mayele. Hakika mchezo wa watani upo mikononi mwao kesho.

Sambaza....