Ligi Kuu

Nyundo za Kamati ya Masaa 72 kwa vilabu hizi hapa

Sambaza....

Mechi namba 171 (Njombe Mji 0 vs Simba 2). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikina katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 3, 2018 kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, ikiwemo pia mshabiki mmoja wa timu hiyo kuingia uwanjani na kuchukua taulo la kipa wa Njombe Mji lililokuwa golini. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 165 (Mtibwa Sugar 0 vs Simba 1). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo iliyofanyika Aprili 9, 2018 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Kitendo hicho cha washabiki wa Simba iliyokuwa ikicheza ugenini ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, wakati adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 177 (Singida United 0 vs Mtibwa Sugar 3). Mchezaji Tafadzwa Kutinyu wa Singida United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kufanya vitendo vyenye kuonyesha imani za ushirikina katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 6, 2018 kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Katika mchezo huo, Kutinyu alichukua taulo la kipa wa Mtibwa Sugar na kulirusha jukwaani kwa washabiki wa Singida United ambao waliondoka nalo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

Mechi namba 184 (Mbao 0 vs Lipuli 0). Klabu ya Mbao imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mshabiki wake kuingia uwanjani na kuchukua glovu za akiba za kipa wa Lipuli zilizowekwa golini na kukimbia nazo, kitendo kinachoonyesha imani za kishirikina.

Adhabu dhidi ya Mbao katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 6, 2018 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 185 (Yanga 1 vs Singida United 1). Klabu ya Singida United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi ya klabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Vilevile Bodi ya Ligi imepeleka malalamiko kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) dhidi ya Meneja wa Singida United, Ibrahim Mohamed kwa kuongoza vurugu za timu yake kulazimisha kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi.

Mechi namba 191 (Simba 3 vs Mbeya City 1). Klabu ya Simba imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika sita katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 12, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kitendo cha Simba ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo wakati adhabu dhidi yao imekijita katika Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 194 (Azam 0 vs Njombe Mji 1). Kocha wa Azam, Aristica Cioba amesimamishwa hadi suala lake la kumtukuna Mwamuzi baada ya mechi kumalizika litakaposikilishwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Uamuzi wa kumsimamisha umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.

Kabla ya kumtukana Mwamuzi, Kocha huyo aliondolewa kwenye benchi (ordered off) kwa kupinga maamuzi kwa maneno na vitendo katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 15, 2018 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mechi namba 200 (Simba 2 vs Tanzania Prisons). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuwakilishwa na maofisa watatu badala ya wane kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kitendo chao ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x