Ibrahim Ajib Migomba.
Ligi Kuu

Rafiki yangu Ajib ananipa unyonge!

Sambaza....

NIMEANDIKA mpaka mwisho nikafuta. Nikaandika tena, nikafuta. Kisha nikaanza kuandika upya. Kiufupi rafiki yangu Ibrahim Ajib ananipa unyonge.

Alianza kunipa unyonge huu alipokuwa Simba na sasa anaendelea kunipa unyonge huu ndani ya Azam fc. Nakwazika sana na kinachomtokea.

Kipaji kikubwa, akili kubwa ya mpira, lakini haonekani kiwanjani. Nini tatizo? Ilitazamiwa ndani ya Azam fc, Ajib aamke tena awe mfalme. Wengi tuliwaza hivi. Kilichotokea sasa Ajib wa Azam fc na Ajib wa Simba hawana tofauti.

Siku zake za mwanzo ndani ya Azam fc alionyesha kitu. Tulikuwa pamoja kule Zanzibar kwenye Mapinduzi. Alipiga mpira mwingi. Nikajisemea moyoni mwangu kuwa sasa huyu ndiyo Ajib.

:: Maisha yamekuwa tofauti siku hizi. Azam fc hivi karibuni imecheza michezo kadhaa ya ligi. Ajib haonekani katika michezo hiyo katika kikosi kilichoanza, hadi wale wachezaji wa akiba benchi. Anakaa zake jukwaani na mashabiki.

Sijui, lakini moyo wangu unaishia kupondeka pondeka kwa kinachomtokea Ajib. Huu ni ukweli mchungu nilioshindwa kuumeza moyoni mwangu.

Nimejikuta kuumia kila ninapoona kikosi cha Azam fc mitandaoni, kisha Ajib yuko jukwaani, huku Azam fc wakiwa kiwanjani wanacheza.

Ajib hajui mpira? Hapana. Kuna timu haitamani kipaji cha Ajib? Hapana. Katika ubora wake kuna timu katika ligi yetu Ajib anaweza kukaa benchi? Bado inakuwa hapana. Shida nini kwa Ajib?

Ni swali gumu. Majibu ya kwanini hachezi liko kwenye Mahakama ya Ajib mwenyewe. Lakini binafsi kila nikimtazama Ajibu ninachokiona A -Push katika kiwanja cha mazoezi.

Ajib anamalizwa na hili. Yuko down sana katika kiwanja cha mazoezi. Unapokuwa down katika mazoezi ni ngumu kupata nafasi ya kucheza mechi. Rafiki yangu Ajib anamalizwa na hili tu.

Siku ambayo Ajib ataacha kila kitu na Ata – push katika kiwanja cha mazoezi na kutega sikio lake kumsikiliza Amorin Abdulhamid, nadhani ndiyo itakuwa njia ya kututoa kifungoni marafikize.

Lakini kama kilichoko leo kitaendelea hivi tutazidi kupondeka pondeka mioyo yetu. Mpira uko kwenye Mahakama ya rafiki yetu. Atupe furaha, atuzidishie machungu.

Sambaza....