BlogMataifa Afrika U17

Serengeti Boys kutumia michuano ya COSAFA kama maandalizi ya mwisho kuelekea AFCON U17.

Sambaza....

Kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ Oscar Mirambo amesema watayatumia mashindano ya Umoja wa Baraza la Michezo Afrika kanda ya tano (African Union Sport Council (AUSC) Region 5 Youth Games) ukanda wa Afrika ya Kusini (COSAFA) kama sehemu pekee ya kujiandaa na michuano ya Mataifa Afrika Mwakani.

Mirambo amesema katika mashindano hayo ambayo yataanza mwezi Disemba mjini Gaborone nchini Botswana Tanzania wakiwa kama waalikwa watapeleka baadhi ya wachezaji ambao wamepanga kuwatumia katika michuano ya Afrika ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

“Mashindano  haya ndio yatakuwa kama kambi ya moja kwa moja, na baada ya mashindano haya ya COSAFA ni wazi kwamba hatutapumzika tutaendelea kuandaa timu na mwisho wa siku tuwe na timu itakayoweza kushindana kwenye michuano ya AFCON mwakani” amesema.

Amesema kwa kuwa michuano hiyo wanaruhusu wachezaji 20 pekee basi itawabidi kuwapunguza wachezaji wao ili waweze kwenda huko wakati wa mashindano hayo ambayo yanatarajia kuanza Disemba 6 hadi 16 mwaka huu.

Katika mashindano hayo Tanzania wapo kundi B Angola, Malawi na Afrika Kusini huku kundi A likiwa na wenyeji Botswana, Zambia, Swaziland na Namibia huku viwanja vitatu vya UB Stadium, Jamal grounds na uwanja wa Taifa vikipangwa kutumika katika mashindano hayo.

Sambaza....