Blog

Shomary Kibwana: Toleo jipya la Kapombe na Juma Abdul!

Sambaza....

Kutoka “Green City” Mbeya kuna jamaa wa Hip hop anajiita Mbeya Boy Chuma anachana saana jamaa, ana mistari yake kadhaa inasema “Njoo muone X, Nyumba inabomolewa” hii ni kwa wapenzi wa Hip Hop ila wale wapenzi wa Soka imbeni hivi “Njoo Umuone Kibwana, Mpira Unachezewa”.

Yes! Ni kijana mdogo zao la Morro Kids aliyekuzwa vyema kwenye misingi ya soka mpaka sasa ni dhahabu wanayojivunia Walugulu na wapenda soka nchi nzima.

Kibwana Shomari

Achana na Juma Abdul wa Yanga, muweke kando Shomary Kapombe wa Simba, kisha tizama hii damu changa ikiwa kiwanjani, ni dhahiri utawapata ladha ya wawili hao.

Beki wa kulia, beki wa kisasa kabisa, anatimiza majukumu ya kukaba kwa ufasaha, anapandisha timu inapobidi, maji anamwaga na ‘Control’ mguu ipo ya kutosha nini kingine mnataka?

Kwenye stori zangu na yeye aliwahi kuniambia kua hakuna timu anaweza kushindwa. Mucheza ikiwa Mwenyezi Mungu atatia baraka zake. Naam ndivyo mchezaji unapaswa kua, kujiamini na kutoogopa changamoto huku malengo na imani yako vikikuongoza.

Umri wa Kibwana ni ushindi tosha kwake, hakuna timu yenye mipango ya muda mrefu itakayomkataa, miaka 20 lakini uwezo na uzoefu alionao ni mkubwa sana. Kumbuka huyu miaka miwili nyuma alikua katika michuano ya vijana ya U-17 pale Gabon na kina Kabwili, Dickson Job na Ally Ng’azi.

Na naamini baada ya miaka kadha Mwenyezi Mungu akitupa uzima, tutaandika, tutaongea na tutajivunia zaidi kipaji hichi kutoka Morogoro.

 

Sambaza....