Sambaza....

Klabu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imethibitisha kushiriki mashindano ya Mapinduzi Cup yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari Mosi mwaka huu kwa kupeleka kikosi kamili.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara amesema watapeleka kikosi kamili na watayatumia mashindano hayo kama sehemuya kujiandaa kwa ajili ya mchezo wao wa kundi D kwenye ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

“Mechi na Waalgeria hao inatarajiwa kupigwa uwanja wa Taifa siku ya Jumamosi ya Tarehe 12 Januari saa kumi alasiri, na iwapo Simba itafuzu kuingia nusu fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi, kikosi cha pili kitabaki Zanzibar na baadhi ya wachezaji huku wengine wakirejea kuwakanili Saoura JS,”

“Na kwa kuwa fainali ya Mapinduzi hufanyika Januari 13, iwapo Simba itafuzu basi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wachezaji kurejea visiwani Zanzibar kucheza fainali hiyo,” amesema.

Manara amesema Simba inathamini sana mashindano hayo ya Mapinduzi kwa kuwa yanadumisha Mapinduzi matakatifu yaliyofanyika mwaka 1964 na ndio maana wameamua kupeleka kikosi kamili kushiriki mashindano hayo.

Katika mashindano hayo Simba wapo kundi A pamoja na timu za KMKM, Mlandege na Chipukizi.

Sambaza....