Ahmed Ally akiongea na Wanasimba
Uhamisho

Simba: Kwa Usajili Huu Tunaungana na Klabu Kubwa Duniani

Sambaza....

Baada ya kumtambulisha skauti wake rasmi wa klabu ya Simba Mels Daadler msemaji wa Simba Ahmed Ally amesema sasa wanaenda kisasa na wanakua miongoni mwa klabu kubwa kutokana na utendaji wao.

Ahmed anakiri utambulisho wa Mels Daalder katika klabu yao utawafanya kuendesha timu kisasa na wanafanya kazi kama ambavyo timu kubwa duniani zinafanya. “Leo tumetambulisha skauti mkuu wa timu yetu. Hili ni jambo kubwa kwa upande wa maendeleo ya kiufundi,” alisema kupitia ukurasa wake wa instagram na kuongeza:

“Kwenye mpira wa kisasa skauti ni mtu muhimu sana, vilabu vikubwa vyote duniani wanamiliki skauti na sisi tumeamua kuungana na wakubwa wenzetu. Skauti ni mtu anaehudhuria mechi mbalimbali kwa niaba ya klabu kwa lengo la kuvumbua vipaji.”

Mels Daadler skauti mkuu wa klabu ya Simba

Kuna aina mbili za skauti ya kwanza ni “Player Scout” kufanya tathmini kuhusu vipaji vya wachezaji kwa lengo la kuwasajili. “Tactical Scouts” kufanya tathimini ya kiufundi kwa wapinzani na kisha kuandaa mpango wa kiufundi kudhibiti mpinzani

Sambamba na kutaja aina za maskauti Ahemd pia alitaja sababu na matumizi ya skauti kwa klabu yake.

Ahmed Ally “Kwa muda mrefu kazi ya kusaka wachezaji imekua ikifanywa na viongozi na wameifanya kazi hii kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu sana. Vipaji vyote vilivyokuja Simba vililetwa na viongozi wetu. Sasa kazi hiyo inaendwa kufanywa kitaalamu zaidi na mtaalamu husika.”

Clatous Chama moja ya sajili zilizofanywa na uongozi wa Simba katika miaka ya hivi karibuni.

“Mfano mwisho wa wiki iliyopita kulikua mashindano ya AFCON U 17, Ni kazi ya Skauti kupiga kambi katika mashindano kama hayo ili kutafuta vipaji. Skauti inasaidia kupunguza usajili wa mihemko mara kadhaaa tumeona tukisajili mchezaji kwa sababu amecheza vizuri kwenye mechi fulani.”

“Skauti atafuatilia hatua kwa hatua za mchezaji kwa kuangalia uwezo wake wa uwanjani, tabia za nje ya uwanja, mahusiano yake na wenzake, hali yake ya kiafya, skauti akijiridhisha ndipo anashauri uongozi uchukue hatua. Skauti akifanya majukumu yake ipasavyo tutapata wachezaji sahihi kwa mahitaji ya timu yetu.”

Ally pia amekiri sio kwamba kukiwa na skauti ndio wachezaji wote watakua sahihi na wataisaidia Simba huku pia akitaka Mells afanye kazi yake kwa usahihi.

Kikosi cha Simba kwa msimu 2022/2023.

“Pamoja na usahihi tuliofanya kuleta Skauti lakini haimaaanishi wachezaji wote tutakaowasajili watafanya vizuri. Kwa sababu mbalimbali usajili unaweza ukabuma na hiyo ndo maana halisi ya mpira.

Tumuombee kwa Mungu skauti wetu Mells aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo kwa maslahi ya Simba,” alimalizia Ahmed.

Sambaza....