Mpira wa miguu kwenye Dunia ya sasa unahitaji mchezaji ambaye atapewa mpango kazi na kocha kisha akaenda kutekeleza majukumu ya msingi ndani ya uwanja kupitia falsafa ya mwalimu halafu kilete matokeo bora.
Nyuma ya Dunia hii ya mpira wa miguu kuna mtu anaitwa Kibu Denis Prosper “Mkandaji” ambaye mitaa ya Msimbazi na Kariakoo ilimpokea, changamoto zote akazipokea na akakubali hizo changamoto zipotee kupitia miguu yake ndani ya uwanja.
Ni kweli kipindi kile cha usajili jina lake halikuwa na matarajio makubwa wala kelele nyingi za ubora wake wakati ule anatoka Mbeya City zaidi ya presha kwake kutoka kwa mashabiki wa Kariakoo wakati Simba SC wanamtangaza kama mchezaji wao mpya.
Sio Msimbazi tu bali hata mashabiki timu nyingine hawakuamini kama anaweza kwenda kucheza mbele ya kivuli cha wachezaji wa nje wakati huo Sakho, Phiri, Banda, Okrah na wengine chini ya kocha Zoran Maki na Roberto Oliveira ” Robertinho” lakini ilikuwa tofauti hasa kwa Robertinho ambaye bado yupo Simba mpaka hivi sasa.
Robertinho amewahi kukiri hadharani kuvutiwa na uwezo wa Kibu Denis ile siku ya kwanza tu mazoezini baada ya kutambulishwa rasmi kama kocha mkuu wa Simba SC! Kocha akakubali uwezo wake hali iliyopelekea kumpa zawadi na baadae dakika za kutosha ndani ya uwanja.
Rahisi sana! Kama ukitaja wachezaji watatu waliopata dakika nyingi za kucheza chini ya Robertinho sidhani kama jina la Kibu Denis litakosekana, lazima litakuwepo sababu ni mchezaji ambaye anatekeleza majukumu yake kwa kiasi kikubwa.
Mwanzoni alikuwa na changamoto kubwa sana ya utulivu kwenye eneo la mwisho lakini chini ya Robertinho ameimarika sana na anafanya vizuri! Nguvu na upambanaji wake ndani ya uwanja ni wa kiwango cha juu sana siku hizi presha kutoka nje imepungua kwake.
Kutoka Kamuyange, Ngara-Kagera mpaka Geita Gold na baadae Mbeye City kwa sasa Nyota imeng’aa Msimbazi na anaisubiri Afcon 2024 akiwa Taifa Stars achilia mbali michuano ya Vilabu ya CAF ambayo ameizoea kwa sasa.
Nyuma ya simulizi hii ya Kibu Denis Prosper kuna mtu mmoja anaitwa Roberto Oliveira “Robertinho”
“Usimkatie mtu tamaa”