Pablo Franco
Tahariri

Tatizo la Simba siyo Pablo wala Mo, tatizo ni Uvumilivu na Uaminifu.

Sambaza....

Wakati nafikiria kuandika makala hii kuna maneno mawili ya kingereza yalikuwa yananisumbua akili yangu, maneno hayo ni PRIME na FORM. Maneno haya mara nyingi hutumika kwenye sayari yetu pendwa ya mpira wa miguu.

Akili yangu ilikuwa inatamani kufahamu tofauti kati ya PRIME na FORM. Katika pita pita zangu nilipata utofauti wa maneno haya, utofauti ambao unaweza ukawa hauna tafasri ya moja kwa moja ya maneno haya.

Kwa mujibu wa vyanzo vyangu neno PRIME kwenye mpira wa miguu unatumika kuainisha timu , kocha au mchezaji ambaye alifikia ubora mkubwa uliodumu kwa muda mrefu. Neno FORM kwenye mpira wa miguu hutumika kuainisha timu, kocha au mchezaji ambaye ana kiwango kizuri kilichodumu kwa muda mfupi bila kumpa mafanikio makubwa.



Wakati naendelea kutafakari tofauti ya maneno haya nikaikumbuka Liverpool, wana fainali wa ligi ya mabingwa barani ulaya msimu wa mwaka 2021/2022 chini ya Jurgen Klopp. Niliikumbuka Liverpool ambayo haikuwa chini ya Jurgen Klopp.

Liverpool ambayo ilikaa miaka miaka 30 bila kuchukua ubingwa wa ligi kuu nchini England, kumbuka mara ya mwisho kwa Liverpool kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya England ilikuwa mwaka 1992, ila mwaka 2020 Jurgen Klopp aliwapa ubingwa Liverpool.

Mwezi October mwaka 2015 wakati Liverpool inamtambulisha Jurgen Klopp aliulizwa kuhusiana na ukame wa makombe uliopo kwenye klabu ya Liverpool. Neno ukame ni neno ambalo Jurgen Klopp alionekana kutolipenda. Alilisisitiza Liverpool hawana ukame ila wana uhaba, uhaba ambao unaweza kutengenezewa mazingira bora na ukaondoka.

Liverpool walikubali kumpa nafasi Jurgen Klopp ili aondoe ukame. Liverpool walikubalina kuwa hawawezi kuondoa ukame huu ndani ya mwaka mmoja au miwili, ila wataondoa ukame huu kwa muda mrefu, walikubaliana na mchakato wa Jurgen Klopp.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa Jurgen Klopp kuingiza falsafa ya gegenpressen counter attacking. Falsafa hii haikuwepo ndani ya Liverpool ila ilikuwepo kwenye kichwa cha Jurgen Kloop.

Kwenye msimu wake wa kwanza, Klopp alitumia mfumo wa 4-2-3-1 mbele akiwa na wachezaji kama  Christian Benteke, Daniel Sturridge, Roberto Firmino, Adam Lallana na  Philippe Coutinho.

Akiwa kwenye mchakato wa kuitengeneza Liverpool bora akaongeza wachezaji wawili, Sadio Mane and Mohamed Salah  2016 na 2017 na akabadilisha mfumo kutoka 4-2-3-1 kwenda kwenye mfumo wa 4-3-3.

Kwenye misimu miwili ya kwanza alifungwa magoli 92, kitu ambacho kilimfanya awaongeze kina Joel Matip, Andrew Robertson, Virgil van Dijk, Fabinho na golikipa Alisson ambao walitatua matatizo ya ya kiulinzi, kipindi hiki Jurgen Klopp alimpandisha Trent Alexander-Arnold kutoka kwenye academy mpaka kikosi cha kwanza.

Taratibu Liverpool ikaanza kutoka kwenye FORM kuelekea kwenye PRIME, wakashinda Ligi kuu ya England kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, Liverpool ikabeba ligi ya mabingwa barani Ulaya, ligi ya mabingwa dunia, kombe la FA, Carabao Cup.

Makombe haya hayakuja kwa haraka, yalikuja kwa timu kutengenezwa kwa muda mrefu. Viongozi na mashabiki wa Liverpool walikubali kukaa muda mrefu bila kuchukua kikombe chochote na kuwekeza imani, uaminifu na uvumilivu kwa Jurgen Klopp ili atengeneze timu anbayo itakuwa bora.

Simba imekuwa kwenye form ndani ya misimu mitano. Imefanikiwa kuingia robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Africa mara mbili na kuingia robo fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika mara moja. Mafanikio haya tunaweza kuyaita ni Form na siyo Prime.

Wachezaji wa Simba wakiingia uwanjani katika moja ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Wangefikia ubora wa kuchukua vikombe hivi au kuingia fainali mbili tungekuwa na nafasi ya kukiri kuwa Simba walifikia kwenye prime ya mafanikio. Kitu ambacho Simba walikosea ni wao kuamini wako kwenye Prime wakati wapo kwenye Form.

Hawachelewa kufika kwenye Prime. Wanatakiwa kuwa na UAMINIFU pamoja na UVUMILIVU ili wafike kwenye matamanio yao. Wanatakiwa wamtafute kocha ambaye watamwamini na kumvumilia.

Wachezaji wa Simba wakishangilia mbele ya mashabiki wao.

Liverpool walimwamini Klopp akaingiza falsafa yake ya “gegenpressen” na akasajili wachezaji ambao wangeweza kuingia kwenye falsafa yake ambayo imewafanya Liverpool kuwa timu ya kutisha.

Bado naamini Simba wanaweza kuwa wakubwa kama wanavyotamani kuwa na bado naamini tatizo la Simba siyo kocha ila tatizo la Simba ni kukosa UAMINIFU na UVUMILIVU kwa makocha wanaowaleta. Misimu mitano iliyopita Simba wamefukuza makocha watano, ni ngumu kuwa na PRIME timu kwenye mazingira kama haya.

Sambaza....