Yanga mazoezini
Ligi Kuu

TFF wazidi kuitafuna akaunti ya Yanga.

Sambaza....

Kamati ya bodi ya ligi kuu ya Uendeshaji na usimamizi wa ligi (Kamati ya saa 72) imeitoza klabu ya Yanga faini ya jumla ya shilingi milioni tatu na laki tano pamoja na kumfungia beki wake kisiki Kelvin Yondani kutokana na makosa mbalimbali.

Katika kikao cha kamati hiyo kilichoketi April 18, pamoja na kupitia matukio mbalimbali na kufanya maamuzi imetoza klabu ya Yanga faini ya shilingi. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Ndanda iliyofanyika Aprili 4, 2019 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Hilo ni kosa la nne msimu huu kwa timu ya Yanga kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi.

Ukiachilia mbali faini hiyo Vilevile Yanga imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani baada ya mechi hiyo kumalizika. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Nayo klabu ya Ndanda SC imetozwa faini ya sh. 1,500,000 (milioni moja na nusu) kwa kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Hilo ni kosa la kwanza msimu huu kwa timu ya Ndanda SC kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Adhabu dhidi ya Ndanda pia ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Naye Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Ukiachilia mbali adhabu hizo pia kamati hiyo imemkuta na hatia mchezaji wa Azam beki Aggrey Morris ambaye amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Mbao FC katika mechi baina ya timu hizo Aprili 7, 2019 iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mbali na Morris pia Mchezaji Paul Peter wa Azam FC amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Mbeya City FC.

Maamuzi ya matukio mengine.

Mechi namba 317- Tanzania Prisons FC 2 vs Mwadui FC 0. Mchezaji Laurian Mpalile wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Mwadui FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 3, 2019 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi namba 326- Singida United 2 vs Kagera Sugar FC 1. Meneja wa Kagera Sugar FC, Mohamed Hussein amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi katika mchezo huo uliofanyika Aprili 6, 2019 kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Ligi Daraja la Kwanza

Mechi namba 110- Mashujaa FC 2 vs Geita Gold FC 1. Kocha wa makipa wa Geita Gold FC, Nassoro Mrisho pamoja na mtunza vifaa (Kit Man) wa timu hiyo Hussein Salehe wamepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kwenda kwenye chumba cha waamuzi na kutoa lugha za matusi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 13, 2019 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Mechi namba 106- Rhino Rangers 0 vs Polisi Tanzania FC 1. Kipa wa Rhino Rangers FC, Mohamed Ally Seif amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF ambapo baada ya mchezo kumalizika aliwafanyia vurugu wachezaji wa Polisi Tanzania FC katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 7, 2019 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Mechi namba 113- Namungo FC vs Friends Rangers. Namungo FC imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Friends Rangers FC kugomea mchezo huo uliofanyika Aprili 13, 2019 kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani Lindi. Hadi mchezo huo unavunjwa na Mwamuzi kutokana na timu ya Friends Rangers kutoka uwanjani, Namungo FC ilikuwa ikiongoza mabao 2-0.

Pia klabu ya Friends Rangers imetozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na kuvuruga mchezo huo wakati Kiongozi wake, Herry Chibakasa amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kusababisha timu yake kugoma. Uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Kuvuruga Mchezo, na Kanuni ya 14(37) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x