Blog

Tshabalala, Gadiel katika vita inayoumiza

Sambaza....

MABEKI bora wa kushoto kwa sasa nchini wako Simba. Ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Gadiel Michael. Mchuano wao ni mkali. Ni mkali kweli kweli. Ni ngumu kumtabiria nafasi ya moja kwa moja mchezaji mmoja. Hii ni vita inayowanufaisha Simba. Nitakuelezea huko chini.

Ugumu wa vita hii unaanzia kwa atakayemuweka mwenzake benchi ndiyo atafanya hadi asiitwe timu ya taifa. Vita inaanzia hapa. Unaitwaje timu ya taifa ikiwa hupati nafasi ya kucheza klabuni kwako? Unaweza kuitwa, lakini kwa kesi maalum.

Wakati Bongo Zozo akijitangaza yeye ni muumin wa vita isiyoumiza, Tshabalala na Gadiel wao wana vita inayoumiza, lakini vita hiyo inawanufaisha Simba. Ni Simba yenye uhakika na ubora wa wachezaji wao wawili kwenye ulinzi wa kushoto kuwa imara muda wote. Ukizubaa umekwisha.

Vita hii haijaachana mbali na vita inayomkabili Aishi Manula. Maisha si mepesi tena kwa Manula kama ilivyokuwa huko nyuma. Simba ana Beno Kakolanya, Taifa Stars ana Juma Kaseja.

Simba imewatengenezea ushindani wachezaji wake. Sijui kama wachezaji wenyewe wanaujua ushindani waliotengenezewa. Hiki ndiyo kipindi ambacho baadhi ya wachezaji wanaishindwa presha ya ushindani, wengine wanaiweza.

Aliwahi kuniambia rafiki yangu mmoja ambaye ni mchezaji kuwa hakuna mchezaji anayependa changamoto kama hizi walizokutana nazo Aishi na Tshabalala. Huwa wanachukia sana. Hawana la kufanya tu.

Sijui Aishi na Tshabalala wamezipokeaje changamoto hizi. Nyuso zao hazionyeshi kuchukia, lakini nani anayejua kilicho ndani ya nafsi zao? Hili ni swali ambalo majibu wanayo wenyewe.

-Mohamed Hussein

Kwao ni ngumu kutokeza hadharani kusema wanaichukia changamoto hii. Kivyovyote vile watasema wameikubali. Rafiki yangu Said Ndemla yeye ni mtu tofauti sana. Hajawahi kuishi katika changamoto za namna hii. Mshindani wake mkuu ni yeye mwenyewe. Akicheza sawa, asipocheza sawa.

Kizuri ni kwamba hawa ni wachezaji ambao hawajapishana sana umri. Kama wamepishana ni miaka miwili au mmoja. Umri ni kitu kingine kinachokoleza ushindani wao wa nafasi kikosini.

Hassan Khatibu aliwahi kuwa mlinzi wa Simba katika Simba B ile ya kina Ajib. Hassan ndiye aliyekuwa nahodha wa timu na staa wa timu. Simba ilimpandisha timu kubwa akaanza kucheza baadhi ya mechi. Baadae Simba ikasajili watu wa shoka. Pole pole mfumo ukaanza kumtenga.

Akaondoka zake Simba kwenda Kagera Sugar. Sasa hivi hana timu. Kila weekend tunakutana katika uwanja wa Makulumra Magomeni katika mechi zetu ambazo nikicheza huwa nang’aa sana.

Nani ajuaye kama Hassan asingeletewa watu wa shoka leo hii ndiyo angekuwa staa wa Simba katika safu ya ulinzi? Hakuna anayejua! Mahitaji ya timu yamemtoa mchezoni Hassan. Siku hizi ni kama vile amekata tamaa na mpira. Haonyeshi kuwa kama ana deni kwa Watanzania.

Natamani kuendelea kuwaona Aishi na Tshabalala wakicheza tena na tena kama ilivyokuwa misimu mingine huko nyuma, lakini kila nikiwazatazama Gadiel na Beno naona maisha si mepesi tena.

-Gadiel Michael

Gadiel na Beno wamekuja ikuleta upinzani wa kweli. Hawakuja na sura za kinyonge kama sura walizokuja nazo kina Kwassi Asante. Hawa wamevuka Mtaa wa Twiga na Jangwani kuhamia Mtaa wa Msimbazi, tena walikotoka walikuwa ni mastaa.

Muda huu tunaoendelea kuitazama vita hizi zinazoumiza, tujue wazi kwa Simba kwao ni vicheko. Wanacheka tu kisha wanaibuka na methali isemayo vita ya panzi furaha kwa kunguru.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x