Blog

Tulimsubiria Neymar, Akaja Salah

Sambaza....

Kivuli cha Lionel Messi ndicho kilichomtoa, hakutaka kusimama kwenye kivuli cha mtu mwingine ilihali kivuli chake kikiwa kimesinyaa.

Mawazo yake na matamanio yake makubwa yalikuwa kujenga Ufalme wake mwenyewe. Ufalme ambao atapokea heshima kubwa kila sehemu ya dunia.

Messi na Neymar wakiwa Barcelona

Aliamini ndani ya Ufalme wake atakuwa huru kufanya maamuzi yoyote aliyokuwa anayatamani kuyafanya pale Barcelona.

Akazidi kuamini ndani ya Ufalme wake kila mtu atamwabudu na kusujudu mbele yake, waimbaji wote alitamani wamtungie nyimbo za kumsifu yeye na kumwabudu yeye kama bwana wa mpira wa miguu.

Mitandao yote ya kijamii alitaka kuiteka ili iwe inamzungumzia yeye juu ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, hata mikataba ya kibiashara na makampuni mbalimbali alitamani aipate yeye.

Aliona ni muda sahihi kwake yeye kumiliki Ufalme, PSG ikampokea na yeye akaipokea kama sehemu ya kwake yeye kujenga Ufalme wake.

Taratibu changamoto za Ujenzi zikawa zinaonekana, Edson Cavan kuwepo pale kama mpigaji rasmi wa penalti ikawa changamoto ya kwanza lakini haikuwa ngumu kwake alifanikiwa kuiruka.

Neymar

Siku zikazidi kukimbia, alionesha uwezo wake ambao ulitufanya tuamini kijana wa kutoka Brazil kaamua kweli kweli kupigania Ufalme wake.

Alionesha njaa ya Ballon D’or, alitumia miguu yake kama silaha kuwaadhibu makipa na mabeki wa timu pinzani. Nyavu za goli zilikuwa zinafurahia uwepo wake uwanjani kwa sababu zilijua wakati wowote zitacheka.

Kuna wakati watu walidhani anaziadhibu timu ambazo zinaonekana dhaifu, macho yetu yakawa yanasubiri mechi za klabu bingwa barani ulaya tuone hasira zake za kujenga Ufalme wake imara.

Shindano hili ndilo shindano lenye mvuto, limebeba hisia halisi za mpira wa miguu na ndilo shindano lenye ushawishi mkubwa kwenye kupata tunzo ya Ballon D’Or.

Hatua ya mtoano ilianza, Real Madrid ndiyo ulikuwa mtihani wa kwanza kwa Neymar, tulitegemea kumuona atakavyoibeba timu yake mbele ya klabu ambayo ni kubwa , klabu ambayo ina wachezaji wenye hadhi ya juu na kizuri zaidi ndiyo klabu ambayo inatetea taji hili.

Hakuna kikubwa alichokifanya kuwashawishi wengi kuwa wakati wake wa kusimama juu ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi umefika.

Nani kukaa kati ya Messi na Ronaldo?

Swali kubwa kwetu lilibaki ni nani atasimama katikati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo?, hatukutaka kuamini kuwa kuna mchezaji ambaye anaweza kusimama juu ya hawa Wafalme.

Tulimtazama Mohammed Salah katika jicho lenye mashaka ndani yake, hatukuweza kumwamini na kumpa nafasi moja kwa moja kuwa anaweza kusimama katikati yao.

Tuliogopa kuingia makubaliano ya kibiashara naye, hii haikumzuia yeye kuinadi bidhaa yake. Aliamini kupitia ubora wa bidhaa yake ndiyo maana hakuchoka kuiboresha kila siku.

Aliibeba Liverpool, hata siku walipokutana na Manchester City wengi walijua ndiyo safari ya mwisho kwa Liverpool.

Lakini Mohammed Salah alisimama na kutuonesha kuwa ni muda sahihi kwetu sisi kumwangalia kama mshindani sahihi wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Mo Salah

Mechi tano mfululizo alizoanza kwenye michuano ya ƙklabu bingwa ulaya msimu huu akifunga goli kwenye kila mechi na kufanikiwa kufikisha idadi ya magoli kumi nyuma ya Cristiano Ronaldo mwenye magoli kumi na tano.

Amevunja rekodi ya Roger Hunt, gwiji wa Liverpool mwenye magoli mengi katika timu ya ƘLiverpool nyuma ya Ian Rush.

Roger Hunt aliwahi kumaliza msimu mmoja akiwa na magoli 42, lakini jana Mohamed Salah kafikisha magoli 43 akibakiza magoli manne kuvunja rekodi ya Ian Rush mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool aliyemaliza msimu akiwa na magoli 47.

Mwanga tayari ushaanza kuonekana mpaka sasa Salah ana magoli 43, Cristiano Ronaldo akiwa na magoli 42 na Lionel Messi akiwa na magoli 40 .

Hapana shaka hawa ndiyo farasi watatu ambao watakuwepo kwenye mbio za kuwania Ballon D’or tofauti na mwanzoni tulivyokuwa tunawaza kuhusu Neymar.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x