Blog

Tumeamua kufanya mabadiliko? Basi Cheo cha Usemaji wa klabu KISIWEPO!

Sambaza....

Hapana shaka unahitaji maamuzi magumu kufikia ndoto yako ambayo unaiota kila siku kuifikia. Unahitaji kujikana kwenye vitu vingi katika maisha yako.

Na kuna wakati mwingine kuna baadhi ya vitu ambavyo huwa tunavipenda sana huwa inatuhitaji kuviacha ili kufikia tu sehemu ambayo tunaiota.

Kwa kifupi mafanikio huja na sadaka kubwa sana. Sadaka yenye mateso makubwa. Sadaka ya jasho na damu!, sadaka inayoumiza sana.

Na hii ndiyo njia sahihi ya kuyafikia mafanikio. Huwezi kupitia njia nyingine zaidi ya hii. Lazima upitie tu tofauti na hapo neno mafanikio utakuwa unalisikia kwa majirani.

Na hiki ndicho Simba ilichokifanya. Ilijikana , ikaamua kuchukua maamuzi magumu. Maamuzi ambayo yalienda sambamba na kutoa sadaka. Sadaka ya kuachana na mfumo wa wanachama.

Wajumbe wa Bodi ya Simba wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao cha kwanza.

Wakaingia kwenye mfumo wa kibiashara. Kampuni yao ya Simba kwa sasa inatazamiwa kuingiza faida na kujiendesha yenyewe kwa faida kuliko kutegemea pesa za wanachama ambao mara nyingi hata kulipia kadi zao huwa hawalipii.

Mfumo ambao Simba wameingia ni mfumo wa kibiashara. Mfumo ambao wanatakiwa kuiendesha klabu kibiashara, mfumo ambao kuna baadhi ya njia wanatakiwa kuziacha.

Wameachana na mambo ya wanachama kuwa na kadi za klabu na kuzilipia, wameingia kwenye mfumo wa hisa mfumo ambao unawawezesha wanachama kununua hisa na kuwa wamiliki wa klabu hiyo kibiashara.

Jambo ambalo ni jema. Lakini kuna kitu ambacho mpaka sasa hivi wanatakiwa kukifiria tena, nacho ni cheo cha AFISA HABARI WA KLABU.

Kilichofanywa na klabu ya Yanga, Dismas Ten akiwa kama Afisa Habari.

Wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuwa na idara ya habari ambayo itakuwa inatoa habari kupitia vyanzo ambacho vitakuwa chini ya kampuni ya Simba.

Kusiwepo na mtu mmoja ambaye atakuwa anahusika na kuisemea klabu. Kuwekwe utaratibu mzuri wa upatikanaji wa habari muhimu kutoka katika ndani ya klabu.

Mfano, kuwepo na idara ya habari kama nilivyosema. Idara ambayo itakuwa na idadi kubwa ya watu ambao watakuwa wameajiriwa na klabu kwa ajili ya kutoa habari mbalimbali ndani ya klabu kupitia tovuti ya klabu, na mitandao ya kijamii ya klabu.

Klabu inatakiwa iwaajiri watu wa Graphics, watu wa kusimamia tovuti ya klabu, wa kusimamia mitandao ya kijamii ya klabu, watu ambao watakuwa ma wapiga picha.

Msemaji wa Simba, Haji Manara, akiwa katika majukumu yake.

Waajiri watu ambao watakuwa wanasimamia TV ya Klabu, waongozaji, waandaaji miswada. Watu wa Sanaa ya make-up.

Watu hawa na wengine wengi watakuwa chini ya idara ya habari. Idara ambayo itakuwa inatoa habari rasmi ndani ya klabu kuanzia kwa viongozi wakuu mpaka kwa makocha.

Mfano kama kutakuwepo na habari muhimu kutoka kwa viongozi wa ndani ya klabu ya Simba, idara hii ya habari kupitia tovuti ya klabu, mitandao ya kijamii ya klabu( Facebook, Instagram, YouTube channel) itaitoa habari hiyo muhimu kwa Umma.

Pia kuhusiana na masuala ya kiufundi kutoka kwenye benchi la ufundi la timu husika, idara hii ya habari inatakiwa kuandaa mazingira mazuri kwa kocha kuzungumza.

Mfano, ikiandaa mkutano na waandishi wa habari kati ya kocha mkuu na wanahabari, siku mbili kabla ya mechi husika, itawapa nafasi nzuri sana watu kupata habari sahihi za kiufundi kutoka kwa kocha mkuu, tofauti na sasa habari za kiufundi zinapatikana kupitia msemaji mkuu.

Tuondoe hii dhana kuwa kabla na baada ya mechi husika, waandishi wa habari kuwapigia wasemaji wa klabu husika na kutaka kujua masuala ya kiufundi kuhusu mechi husika. Hili huwa ni swali sahihi lakini huwa wanauliza sehemu ambayo siyo sahihi.

Tumeamua kujiendesha kibiashara, basi kila kitu ambacho kinahusu klabu kinatakiwa kiendeshwe kibiashara. Na hii itasaidia sana kulinda sura ya klabu kwa sababu, msemaji anaweza kutofautiana na mwandishi wa habari lakini watu wakachukulia kuwa klabu imetofautiana na mwandishi wa habari.

Watu hawatotazama tena kuwa msemaji yeye binafsi katofautiana na huyo mwandishi wa habari. Kwa hiyo itaonekana moja kwa moja kuwa klabu kwa ujumla ina matatizo na mwandishi Fulani.

Kitu hiki kinaweza kuleta picha ambayo siyo nzuri kibiashara kwa klabu husika. Kwa hiyo lazima idara hii iendeshwe kitaalamu na kibiashara ili iwe chachu kubwa ya kujenga picha nzuri kwa watu.

Picha ambayo italeta nvuvu kubwa hata ya kupata wadhamini wengi ndani ya klabu baada ya hao wadhamini kuona kuwa klabu hii inaendeshwa kibiashara zaidi na kila idara ndani ya klabu inaendeshwa kibiashara!

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x