Mashabiki wa Yanga kwenye mechi ya Simba vs JS Saoura
Ligi Kuu

Yanga fanyeni hivi muwe kama Simba

Sambaza....

Inawezekana roho inauma sana kwa shabiki yeyote wa Yanga. Ni wachache sana ambao wanafurahia mafanikio ya Simba kwenye ligi ya mabingwa.

Ni mashabiki wachache mno wa Yanva ambao wanaotazama mafanikio ya Simba kama mafanikio ya nchi kwa ujumla.

Ila wengi wao roho inawauma sana. Kuna wengine wamejificha ndani tangu jumamosi mpaka leo hii jumanne.

Hawataki kabisa kutoka nje, hawatamani kabisa nuru ya nje. Hawana shida kabisa ya kuona hali ya hewa ya nje.

Kwao wao ndani ni eneo sahihi kabisa. Hii ni kawaida sana kwenye mpira wetu. Mpira ambao umegawanywa sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni yenye rangi ya njano/kijani na sehemu ya pili ni yenye rangi nyekundu/nyeupe. Hizi ndizo sehemu kuu mbili za mpira wa Tanzania.

Sehemu zenye upinzani mkubwa sana. Sehemu zenye utani mkubwa sana. Tena ule utani wa kuudhi sana.

Lakini ndizo sehemu ambazo tumeamua kuziishi. Ndiyo maana nikakuambia kuwa kuna mashabiki wa Yanga mpaka muda huu wako ndani tu.

Hawatamani kabisa kutoka nje kwa sababu moja tu KUTANIWA. Hii ndiyo sababu kuu kubwa ambayo inasababisha pia baadhi ya mashabiki wa Yanga kuumia na mafanikio ya Simba.

Wanajua kabisa mafanikio ya Simba ni mkuki unaochoma kwenye mioyo yao. Ndiyo maana ni ngumu sana kukuta shabiki wa hizi timu mbili akifurahia mafanikio ya mwenzake.

Ni kwa nadra sana. Njia ziko mbili tu za kuringishiana. Moja kuombeana mabaya na njia ya pili ni kujibiana kwa mafanikio.Yani mwenzako akinunua Vitz wewe unaenda kununua Starlet.

Na njia ya pili ndiyo njia ambayo Yanga kwa sasa wanaitamani sana. Yanga wanatamani sana kwa sasa kufanya vizuri na wao kwenye michuano ya kimataifa.

Wanatamani sana!, kutamani ni jambo moja na kutimiza matamanio ni jambo la pili. Unatimizaje matamanio yako ?

Umechonga barabara lipi la kutimiza matamanio yako ?. Hiki ndicho kitu ambacho Yanga wanatakiwa kukifikiria.

Naomba tufikirie kwa pamoja na Yanga. Turudishane nyuma kidogo. Hivi karibuni Yanga iliwahi kuingia kwenye hatua ya makundi ya kombe la shirikisho.

Haya yalikuwa mafanikio mazuri kwa miaka ya hivi karibuni ikizingatia timu zetu zilikuwa hazifanyi vizuri sana ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Kwanini Yanga ilifanikiwa kupata haya matokeo mazuri?. Jibu ni moja tu ilikuwa imesajili wachezaji ambao ni wazuri na wakawa wanahudumiwa vizuri.

Kitu hiki hiki Simba wamekifanya msimu huu. Wamesajili wachezaji ambao ni wakomavu, wakawapa huduma nzuri na Leo hii wanafanya vizuri.

Hii ndiyo njia ambayo unaweza ukaifanya na ukapata matokeo mazuri kwa muda mfupi. Huwezi kupata mafanikio kwa sasa kwa kutegemea academy za timu.

Kwa hiyo Yanga ifanyeje ?. Irudi sehemu ambayo iliishia kwanza kwa mipango ya muda mfupi. Waanze kutafuta wachezaji ambao wanaweza kuwafikisha mbali kwenye michuano ya kimataifa.

Wawaweka pamoja, wawape huduma nzuri. Watawapaje huduma nzuri wakati timu yao inakumbwa na tatizo la uchumi ?

Nahisi hili ni swali kubwa ambalo linakusumbua mpaka sasa hivi wakati unaendelea kusoma hii makala yangu.

Kuna kitu kimoja pekee ambacho Yanga wanatakiwa kusimama nacho. Waitishe mkutano mkuu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Uchaguzi mkuu ambao utakuwa na lengo la kuchagua viongozi ambao watasimamia mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu ya Yanga.

Waachane na uendeshwaji huu. Waweke mfumo mzuri wa kibiashara ambao utaifanya klabu iendeshwe kibiashara , baada ya hapo Yanga itakuwa na nafasi kubwa ya kusajili wachezaji na kuwatunza vizuri.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.