Ligi Kuu

Ali Kiba ni ‘hasara’ si faida Coastal Union, wampige chini dirisha dogo!

Sambaza....

Wakati leo Jumamosi wakitaraji kucheza mchezo wa tatu nyumbani Mkwakwani Stadium, Tanga klabu bingwa ya zamani ya Tanzania Bara, Coastal Union itaendelea kumkosa mchezaji wake mpya Ali Saleh Kiba ‘Ali Kiba’.

Kiba ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongo fleva amesajiliwa na Coastal msimu huu na licha ya kwamba hajawahi kucheza soka katika ligi yoyote ya ushindani kwa miaka yake zaidi ya 30 lakini alisajiliwa huku kocha Juma Mgunda akisema mwanamuziki huyo ni mchezaji mwenye  kipaji ambaye ataisaidia mno timu yake.

Huu haukuwa usajili wa kimpira- niliukosoa usajili huu si kwa maana Kiba hawezi kucheza mpira, bali niliamini kwa umri na kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa miaka zaidi ya kumi sasa hawezi kuwa mchezaji.

Tazama, wakati Coastal inalazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Lipuli FC kisha ushindi wao ‘finyu’  1-0 dhidi ya Biashara  siku ya pili ya msimu mwanamuziki huyo alikuwa Canada akifanya shughuli zake nje ya soka  lakini bado kocha Mgunda amenukuliwa akisema atamtumia mchezaji wake huyo katika mchezo wa jioni ya leo dhidi ya KMC FC kama atakuwepo.

Kwa mtu aliyecheza mpira atakuwa anafahamu kuwa ili mchezaji awe fiti kwa misukosuko ya ligi- hasa ligi ya ngazi ya juu kama ligi kuu ni lazima awe na mazoezi ya kutosha walau kwa wiki sita had inane mfululizo. Kitendo cha Mgunda kusema yupo tayari kumtumia Kiba vs KMC endapo atakuwepo hakiwezi kuingia akilini kwa klabu inayosaka matokeo.

Kiba hakuwepo sehemu kubwa ya maandalizi ya ligi, pia tangu ligi ilipoanza Agosti 22 hakuwahi kujumuika na wenzake kwasababu ya kubanwa na majukumu yake ya kimuziki.  Mgunda kama kocha na mchezaji mwenye heshima kubwa nchini wakati wa uchezaji wake huku akiwa sehemu ya timu iliyoshinda kikombe pekee cha ligi kuu mwaka 1988 alifanya makosa kukubali usajili huu wa Kiba katika kikosi chake.

BIASHARA


Usajili wa Kiba ulipigiwa chapuo na ‘wapambe’ wengi wa mwanamuziki huyo huku wakitoa sababu zisizo za kimpira kuwa mwanamuziki huyo ni ‘taasisi’ ambayo inaweza kuisaidia Coastal katika biashara. Kwamba jina lake kimuziki linaweza kuwavutia wafadhili na wadhamini klabuni hapo, huku pia likiongeza ongezeko la watazamaji katika uwanja wa Mkwakwani.

Labda, wanaweza kufanikiwa katika hilo, lakini ni ufinyu na mtazamo mdogo wa klabu na watu wao wa masoko kushindwa kutafuta njia za uhakika za kuimarisha uchumi wa klabu. Kiba ni mwanamuziki nyota nchini- halina ubishi lakini kwa mtazamo wa kimpira hawezi kuisaidia Coastal ndani wala nje ya uwanja kwasababu hana muda wa kutulia klabuni.

NJIA MBADALA NI KUMTEMA DIRISHA DOGO


Kama atashindwa kucheza walau nusu ya michezo 19 ya mzunguko wa kwanza kwa namna yoyote ile – kiuwezo na kimajukumu Coastal itabidi imteme mchezaji huyo na kutafuta mwenye kuweza kutoa mchango kila anapohitajika.

Kama atakosekana katika mchezo wa leo hii inamaanisha Coastal watakuwa nje ya matarajio yao kwani katika michezo yote mitatu ya nyumbani kutokuwepo kwa Kiba kunamaana ile biashara yao waliyotaraji tayari imeanza ‘kudoda’ wakati wangeweza kumpa mchezaji mwingine nafasi ya Kiba ili kuwasaidia ndani ya uwanja.

Naamini bado wataendelea kumkosa Kiba katika michezo mingi zaidi kwasababu katika ‘lugha ya mwili’ tu Kiba anaonekana si yeye aliyehitaji kucheza Coastal bali kuna watu ndio walimng’ang’ania  kwa kuamini ni ‘mtaji mzuri kibiashara’.

Kama ataendelea kuchukua mshahara pasipo kuingia uwanjani wala kuwepo sehemu ya timu kwa muda mwingi – mtu huyo wa nini? Bila shaka watapaswa kumuondoa tu katika kikosi chao na nafasi hiyo kumpa mchezaji mwingine katika dirisha dogo ili awasaidie.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x