Ligi Kuu

Beno nyota, ila Zahera, Jonesia na Kagere wameipendesha zaidi.

Sambaza....

BENO Kakolanya amejiimarisha zaidi kama kipa chaguo bora la kwanza klabuni Yanga SC, na mara baada ya kumalizika kwa dakika 90’ za pambano la mahasimu wa soka nchini Simba SC 0-0 Yanga jana Jumapili kipa huyo aliibuka nyota wa mchezo na kuwa mchezaji aliyezungumzwa mno katika ‘Dar es Salaam-Pacha’ ya kwanza msimu huu.

Dakika ya 10 tu ya mchezo alifuta goli- Kakolanya alitokea kwa kujiamini akitazamana na mshambulizi Mganda, Emmanuel Okwi na kuokoa kwa mguu mpira ambao ungeweza kuwa goli la kwanza katika mchezo huo.

Samba walishambulia kwa dakika zote 30 za kwanza za mchezo na kiki kali ya mbali ya mshambulizi, Mnyarwanda, Meddie Kagere iliokolewa na Beno dakika ya 27 na kufikia hapo kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons ‘akaanza kuoneka kikwazo cha kwanza kwa Simba kushinda mchezo walioupania mno.’

Kwa hakika Beno alistahili kutajwa kama nyota wa mchezo huo lakini kwa jicho la Tatu kocha Mcongo, Zahera Mwinyi, mwamuzi Jonesia Rukyaa na mshambulizi wa Simba, Kagere walichangia mno kuupendezesha mchezo huo ambao haukuwa na magoli.

 

JONESIA RUKYA…..

Alikuwa mtulivu, alitumia busara kuamua maamuzi yake na aliyasimamia vizuri kama mwamuzi wa kimataifa. Alimpa kadi ya njano nahodha wa Yanga, Kelvin Yondan mwishoni mwa robo saa ya kwanza kwa kosa la kumrukia mchezaji wa Simba kwa miguu miwili.

Rukyaa angwezea kumuondoa Kelvin kwa kadi nyekundu lakini alichukulia kosa hilo la kwanza katika mchezo kwa mtazamo wa kawaida wa kimpira na kitendo cha kumuonya kwa kadi ya njano kilimsaidia beki huyo wa kati kuwa kiongozi zaidi kwa wenzanke. Jonesia aliupendezesha mchezo kutokana na maamuzi yake na namna alivyoweza kuwachukulia wachezaji kama binadamu wanaoweza kufanya makosa.

Katika mechi ya mahasimu hao wa soka tatizo kubwa huwa waamuzi lakini jana nilishuhudia mwanamama huyo akifanya kazi yake kwa hekima na busara. Maamuzi yake hayakuegemea upande wowote na hata kama yalionekana makosa kadhaa yanaweza kuewa ya kibinadamu tu lakini kwa hakika mwamuzi huyo mwenye beji ya Fifa ameonyesha wazi yupo tayari kwa kuamua mipambano mikubwa zaidi Afrika.

ZAHERA MWINYI…..

UTULIVU wake ulivutia, ameendelea kumuamini kijana U20, Paul Godfrey katika beki namba mbili na ni yeye aliyeamua kumpanga Abdallah Hajji ‘Ninja’ na si Mrisho Ngassa katika kikosi kilichoanza mchezo. Kumpanga Ngassa kulimaanisha Yanga wangecheza mfumo wa 4-4-2 na kwa aina ya mchezo ulivyokuwa naamini ‘machale’ yalimcheza kocha huyo Mcongo.

Ninja alicheza karibu kabisa na walinzi wake wa kati, Kelvin na Vicent Andrew. Alifuatilia kila njia za Okwi. Katika mfumo wa 4-5-1 ambayo ilikuwa ikibadilika badilika na kuwa 5-4-1, Ninja alikuwa mlinzi wa walinzi wake zaidi na licha ya timu yao kushambuliwa sana hakuchoka. Tackling zake zilikuwa na faida kubwa kwa Yanga na ziliwasumbua sana Simba.

Uamuzi wa kumpanga Mzanzibar huyu na kuwaacha wachezaji wenye uzoefu kama Mzimbabwe, Thaban Kamusoko na Said Juma Makapu wanaoweza kucheza hapo ulikuwa wa ‘kiume’ na Zahera aliweza kufanikiwa kulinda timu yake kutokana na maamuzi aliyoyafanya katika upangaji wa kikosi chake.

Alimtoa mchezaji wake bora katika michezo mitatu iliyopita ( kabla ya Simba v Yanga,) Ibrahim Ajib dakika kumi tu baada ya kuanza kipindi cha pili na alisema alifanya hivyo kwa sababu Ajib alishindwa kucheza vile alivyotakiwa.

Kuisaidia Yanga katika mashambulizi ya kushtukiza. Matheo Anthony ambaye alichukua nafasi ya Ajib alikuwa na kasi zaidi hivyo Zahera alimtoa Ajib kwa sababu hakutaka kuona timu yake ikishambuliwa tu bila kujbu lolote. Ndivyo makocha wazuri walivyo.

Zahera alikuwa bora kama kiongozi wa timu na hata wachezaji wake walivyokuwa hoi kwa mashambulizi ya Simba hakuwasumbua kwa kuwapigia kelele. Huyu alikuwa staa zaidi wa mchezo kwa upande wangu kwasababu aliisoma Simba kabla, akaendelea kuisopma wakati wa mchezo na hakupoteza utulivu wake kama ‘nahodha asiyevaa beji.’

MEDDIE KAGERE…..

Mchezaji huyu wa ukweli alionekana akipiga ngumi chini mara kadhaa, pia alionekana akiomba sana Mungu kila aliposhindwa kufunga na kwa muda wote wa dakika 90’ alikuwa mwenye ‘uchu’. Bonge la straika, aliwahemyesha walinzi watatu wa Yanga na mara kadhaa alikuwa hatari kwa kipa Beno.

Kama Beno alikuwa mchezaji bora wa mchezo huo basi, Kagere ndiye aliyemsaidia kumpa ubora huo kutokana na harakati zake. Kuna wakati alichomoka isivyotarajiwa katikati ya Kelvin na Andrew na kupiga kichwa cha ‘kuruka’ , hakufunga lakini mashambulizi yake yalikuwa mazito mno kwa Beno hata kama alifanikiwa kuyabeba.

Alikuwa mchezaji bora kwa upande wa Simba-kwa mtazamo wangu, alijituma na hakuchoka kutafuta goli kwa muda wote wa mchezo. Amedhihirisha ni kwanini alikuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi katika mchezo wa jana.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x