Sambaza....

KIUNGO wa zamani wa Real Kings ya Afrika Kusini, Coastal Union, Simba SC, Azam FC, Mtibwa Sugar FC, na Ashanti United, Abdulhalim Humud amesema anaamini kikosi chao cha KMC FC kitanyanyuka kuanzia Jumamosi hii na kuachana na matokeo ya sare.

KMC ambayo inacheza ligi kuu kwa mara ya kwanza itaikabili Biashara United FC katika uwanja wa Kumbukumbu wa Karume mjini Musoma katika mchezo wao wa kumi. Kikosi hicho cha kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije kimeshinda mara moja tu katika michezo tisa iliyopita, sare sita na vichapo viwili-matokeo yanayowatupa hadi nafasi ya 12 katika msimamo- wakiwa na alama tisa.

“ Kweli ni matokeo mabaya sana, lakini mwenye jukumu ni mwalimu, kwa sababu yeye ndiye anatakiwa kujiuliza wapi tunakosea na kurekebisha ili tupate matokeo yenye faida kwetu.” Anaanza kusema Humud nilipofanya naye mahojiano Alhamis hii.

Humud

“ Mimi kila siku naitakia mema timu yangu ya KMC. Matarajio yangu ni kuanza kupata ushindi kwa sababu ukiangalia hali halisi ilivyo- mechi tisa, tumepoteza mbili, tumeshinda moja na droo sita, ni matokeo mabaya sana yanayopaswa timu ijiulize kuna nini kinachokwamisha kupata ushindi.”

KMC itakuwa wageni wa Biashara United-timu nyingine inayocheza ligi kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza . timu zote mbili zinakutana zikiwa katika presha kubwa ya kupata ushindi baada ya mwanzo wa kusuasua. Biashara ipo nafasi ya 17, imeshinda mara moja tu katika michezo yao nanesare tatu na kupoteza mara tano hivyo ni mchezo mgumu Jumamosi hii unataraji kuonekana mjini Musoma.

“ Ni lazima tunyanyuke na kushinda. Ligi ndiyo inazidi kusonga hiyo na matarajio ya wengi ni kuona KMC inafanya vizuri, sasa tunashindwa kufanya vizuri inabidi tujiulize. Ingawa katika soka la Bongo ( Tanzania) mtu ukiwa mkweli unaweza kuletewa fitna na longolongo na maneno kibao, pia unaweza kuambiwa huna nidhamu au kuonekana hupendi timu, lakini lazima tujiulize kama timu- kuna tatizo gani mpaka hatupati matokeo?”

Sambaza....