Sambaza....

MAKA Edward, Yusuph Mhilu, Paul Godfrey ni wachezaji vijana ambao waliweza ´kuruka´ kutoka timu ya vijana na moja kwa moja kupata nafasi ya kucheza ligi kuu Tanzania bara.

Vijana hao watatu waliungana na waliokuwa wachezaji wa timu ya Taifa Tanzania U17 April, 2017 katika michuano ya Mataifa ya Afrika, golikipa Ramadhani Kabwili na mshambulizi, Yohana Mkomola na kutengeneza kundi la ´yosso watano´ klabuni Yanga SC msimu uliopita.

Ukiwatoa, Kabwili na Mkomola ´yosso´ watatu- Paul, Mhilu na Maka walifanikiwa kuingia kikosi cha kwanza chini ya walimu, George Lwandamina raia wa Zambia, Shadrack Nsajigwa na baadae Mzambia, Noel Mwandila.

MHILU na MKOMOLA

Mhilu alionyesha yupo tayari kwa majukumu yoyote- na kuna wakati aliongoza mashambulizi kama mshambulizi pekee na kuonyesha ukomavu- rejea dakika 180 za Yanga vs Dicha FC katika play off iliyowapeleka mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania hatua ya makundi ya Caf Confederations Cup April mwaka huu.

Mkomola

Alipocheza kama mshambulizi wa pili sambamba na Mzambia, Obrey Chirwa alionyesha namna anavyokimbia na kutengeneza nafasi. Wakati Yanga iliposhinda michezo saba mfululizo katika ligi kuu kati ya mwezi February- March, 2018, Mhilu alifunga na kutengeneza magoli kadhaa.

Jitihada zake zilivutia- ni mshambulizi mzuri ambaye Yanga hawapaswi kumuacha akapotea. Kama kocha Mcongo, Zahera Mwinyi ataingia sokoni katika usajili unaotarajiwa kufunguliwa November 15 hii na kusaini mshambulizi mpya, Mhilu anapaswa kutafutiwa mahala ambako atatumia miezi sita kucheza tu mpira.

Yanga hata kama watasaini straika mpya kwasababu za kimpira hawapaswi kumuondoa Mrundi, Amis Tambwe katika usajili huu. Wamtafutie, Mhilu timu itakayompa nafasi ili akirejea Juni, 2019 kuchukua nafasi ya Tambwe awe na uzoefu zaidi.

Ni hivyo pia kwa Mkomola. Naamini mshambulizi huyo kinda anaifaa Yanga kuanzia msimu ujao wakati atakapokuja kuchukua nafasi ya Matteo Anthony.

Tambwe amefanya mambo mengi makubwa na ya kuvutia, Matteo kwa misimu minne sasa ameshindwa kufikia matarajio. Washambuliaji hao wawili ( Tambwe na Matteo) wanaweza kuisaidia Yanga misimu huu, lakini watapaswa kuwapisha Mhilu na Mkomola kuanzia Agosti, 2019.

MAKA EDWARD…

Maka akiwa mwenye kujiamini katikati ya uwanja aliendelea kuifanya jezi namba 8 ya Yanga kuendelea kuonekana baada ya Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kuachana na Yanga baada ya misimu sita mfululizo ya kuvutia.

Maka ni namba ambaye atakuja kufikia malengo ya klabu- kimpira na kibiashara. Msimu huu kama ilivyo kwa Mhilu, Maka naye amekosa nafasi.

Maka Edward (kushoto)

Deus Kaseke, Feisal Salum, Jaffar Mohamed na Mrisho Ngassa walioingia kikosini msimu huu wamekificha kipaji hiki. Na wakati, Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, Pius Buswita wakiangaikia nafasi ya kucheza mbele ya machaguo ya Zahera, – Mcongo, Pappy Tshishimbi, Rafael Daud na Feisal njia pekee ya kumsaidia Maka ni kumtafutia timu itakayomuendeleza vizuri kimpira na kumjenga kiushindani.

HITIMISHO

Paul ameweza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza chini ya Zahera, Kabwili bado ni golikipa chaguo la tatu nyuma ya Beno Kakolanya na Mcongo, Kindoki. Vijana hao wawili wanaweza kuendelea kuisaidia Yanga msimu huu hivyo wanapaswa kuendelea kubaki kundini.

Lakini ili kuwaendeleza vizuri chipukizi wao wengi- Yanga wanapaswa kuwaondoa Mhilu, Yohana na Maka katika usajili huu wa dirisha dogo na kuwarejesha Juni mwaka ujao kwasababu yosso hao wote ni vipaji vitakavyowasaidia.

Sambaza....