Sambaza....

MCHEZO wa Yanga SC 4-3 Stand United katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana Jumapili umeweka rekodi kadhaa bora na za kuvutia katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mshambulizi, Alex Kitenge alifunga magoli matatu kwa mpigo na si Hivyo tu, amefunga ‘Hat Trick‘ ya kwanza ya msimu katika uwanja wa ugenini- tena dhidi ya mabingwa mara nyingi zaidi kihistoria wa ligi hiyo, Yanga.

Japokuwa magoli matatu ya Alex hayajawapa ushindi Stand United lakini kimpira yanawaongezea kujiamini kiufungaji kila wanapocheza uwanja wa Taifa. Isisahulike kuwa ni hawa hawa Stand United waliosawazisha magoli ya mabingwa watetezi Simba SC katika sare ya 3-3 katika dimba hilo.

Stand wanakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kufunga magoli matatu-matatu katika michezo miwili mfululizo ndani ya uwanja wa Taifa, tena wamefanya hivyo dhidi ya mabingwa mara 27 kihistoria-Yanga, na mabingwa mara 19 kihistoria-Simba. Nawapa heshima.

Goli lao la kwanza lilikuja kupatikana dakika ya 15 baada ya kutandaza pasi kutokea nyuma kwenda mbele. Lilikuwa goli moja maridadi la kuongoza kabla ya Mrisho Ngassa kuifungia Yanga goli la kusawazisha dakika ya 21.

Kindoki mazoezini

Walijilinda vizuri kama timu kwa dakika 14, lakini Yanga kama timu kubwa walikuwa na malengo ya kufunga ndani ya robo saa ya kwanza. Lakini wakajikuta wakifungwa wao.

Na wakati walipoanza kupumzika katika robo saa ya pili- waliongeza ustahimilivu. Baada ya kukaba kwa nguvu dakika 15 za kwanza, hawakuchoka, wakajituma zaidi lakini robo saa ya tatu na ya mwisho ya kipindi cha kwanza wakaruhusu magoli mawili ya harakaharaka ( dakika 32- Ibrahim Ajib dakika 35- Deus Kaseke )

Hata walipofungwa goli la nne dakika ya 57 na kuwa nyuma 4-1 bado hawakuchoka, hawakutaka kuzuia. Wakashambulia vizuri hadi dakika ya pili ya nyongeza (90+2) Alex alipokamilisha Hat Trick yake.

Ndiyo, golikipa Mcongoman, Klaus Kindoki ameanza vibaya mno kazi yake ndani ya Yanga. Ameonekana kufungwa magoli marahisi mno lakini Isisahulike Aishi Manula alivyopigika dhidi ya ‘Wapiga debe‘ hao kutoka Shinyanga. Je, nani nyanya Klaus 4-3 Stand, au Manula 3-3 Stand.

Nadhani tunapaswa kuipongeza kwanza Stand kisha kuwalaumu Aishi na Kindoki . Hii timu kutoka mkoani Shinyanga imefunga jumla ya magoli sita katika uwanja wa Taifa- si friendly match bali ligi kuu na wamefanya hivyo dhidi ya Yanga na Simba.

Sambaza....