Sambaza....

KLABU ya Simba Simba SC ipo karibu kumtangaza nahodha wao wa zamani, Suleimani Matola kuwa kocha msaidizi wa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara.

Hapana shaka kuhusu uwezo wa Matola kiufundishaji. Matola ni mtu wa Simba hasa, mshindi kiuchezaji na ndiye nahodha aliyefanikiwa kutwaa mataji mengi zaidi katika historia ya klabu.

Matola alishinda mataji yasiyopungua 23 klabuni Simba wakati wa uchezaji wake, alicheza Simba kwa misimu saba (1999-2005) na kwa muda mfupi mwaka 2008 baada ya kuondoka Super Sports United ya Afrika Kusini.

Kiufundishaji, Matola tayari amejidhihirisha ni kocha mshindi vilevile kama nyakati za uchezaji wake. Alianza kazi hiyo mwaka 2011 akiwa kikosi cha pili cha Simba na alifanikiwa kushinda mataji mawili ya ligi kuu ya vijana, kombe la Mapinduzi na michuano Super 8 .

Akiwa katika msimu wake wa kwanza kama kocha mkuu kwa mara ya kwanza katika ligi kuu Tanzania bara, kocha huyo wa Lipuli FC ya Iringa anasakwa na Simba ili kuchukua nafasi iliyoachwa na Mrundi, Masoud Djuma ambaye amefukuzwa wiki hii.

Matola amewahi pia kuifundisha timu ya daraja la kwanza Geita Gold Sports misimu miwili iliyopita anatakiwa kuchukua nafasi ya Djuma ambaye ameondolewa kwa sababu za kimahusiano na kocha mkuu, Mbelgiji, Patrick Aussems.

Djuma inasemekana alikuwa akiigawa timu na kwa vile ni mwenye ushawishi mkubwa kwa wachezaji inadaiwa alikuwa akiwashawishi kucheza chini ya kiwango kwa lengo la kumuhujumu kocha mkuu aonekane hafai ili afukuzwe.

Djuma alikuwa kocha mkuu wa Rayon Sports Club ya Rwanda na ni yeye aliyeipa timu hiyo ubingwa wa ligi kuu Rwanda mwaka 2016. Alifanya Kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog na Mfaransa, Pierre Lechantre klabuni Simba msimu uliopita.

Lechantre alisema wazi baada ya kuondoka Simba kwamba, Djuma alikuwa akimuhujumu kwa kuwashawishi baadhi ya wachezaji kucheza vibaya ili timu ikose matokeo na yeye afukuzwe.

Djuma alihitaji kuwa kocha mkuu na mshaharj wake aliokuwa akilipwa Simba inajionyesha wazi kocha huyo alikuja nchini kumrithi, Omog na si kuwa msaidizi. Siasa za soka la Tanzania zilimnyima nafasi hiyo nda ndani ya miezi isiyozidi 14, Djuma amekuwa msaidizi wa makocha watatu Simba.

MATOLA NI ´FOTOKOPI´ YA DJUMA…

Rejea wakati akiwa msaidizi wa Mcroatia, Z.Logarusin na raia wa Malta, D.Kerr, Matola alikuwa ´mtuhumiwa´ wa kuwagawa wachezaji na kama Simba imemuondoa Djuma kwa sababu za kimahusiano na kocha wake mkuu, basi chaguo la Matola ni baya zaidi.

Kiufundishaji yuko Safi lakini huyu naye ni mtu mbinafsi ambaye anaweza kushindwana haraka na Aussems kama hatokuwa amebadilika.

Sambaza....