Sambaza....

Kocha mkuu wa Tanzania Prisons Mohamed Rishald Adolf amesema amejifunga bomu kuhakikisha anaisaidia timu hiyo yenye maskani yake Jijini Mbeya inapambana na kubaki kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara.

Adolf Rishald ambaye ni Staa wa zamani wa Pan Afrika na timu ya Taifa, ambaye amekuwa nje ya soka kwa muda mrefu amesema anawafahamu wachezaji wa timu hiyo hata kabla ya kujiunga nayo na anajua namna ambayo wanakipaji cha soka, hivyo ameshazungumza nao kujua namna ya kucheza na kupata matokeo.

“Wachezaji wanafahamu nafasi tuliyopo, wananafasi ya wao kuweka heshima yao kwanza, mmoja mmoja halafu timu, kwa hiyo kila mmoja anaonesha hiyo bidii tumezungumza hayo kila mmoja anaelewa na kila mmoja anajua heshima ya kubakisha hii timu, na kila mmoja anajua dharau tutakayopata kama timu hii itashuka, kila mmoja anafahamu uwezo alionao kusaidia hii timu ibaki, mimi kusema naona kama vile itawezekana,” amesema.

Rishald ameongeza kuwa nafasi kubwa ya kuonesha nia ya kutaka kubaki ipo kwenye mchezo wa Jumanne hii dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

“Nafasi kubwa kwetu sisi ni kuanzia mechi ya Jumanne, tunacheza na timu nzuri, yenye uzoefu kwenye ligi, timu yenye wachezaji wazuri kwa hiyo tutashindana, hii ni mechi yangu ya pili ya kwanza ilikuwa dhidi ya Lipuli lakini bahati mbaya tulifungwa, ukichukulia kama mtu aliyejifunga Bomu basi mimi nimejifunga na haina tatizo kwa sababu nafahamu Prisons ni timu nzuri,” amesema.

Tanzania Prisons inashuka dimbani kuumana na Mtibwa Sugar wakiwa kwenye nafasi ya 20 na alama zao 12 katika michezo 19, ambayo wameshinda mchezo mmoja pekee na kufungwa tisa na kutoka sare michezo tisa.

Sambaza....