Kapombe
Blog

Hii ndio Tofauti kuu ya kiufundi kati ya Kapombe na Kessy.

Sambaza....

Nikitaja jina la Shomari Kapombe bila shaka halitokuwa geni kichwani mwako, unamfahamu vizuri kama mchezaji wa zamani wa Azam na timu ya taifa Tanzania yaani Taifa Stras kwa sasa ni beki wa kutumainiwa wa Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club.

Shomari Kapombe katika eneo lake la kimajukumu uwanjani.

Hivi karibuni Kapombe ameamua kutangaza Rasmi kuachana na timu ya taifa ya Tanzania. Kwa lugha nyepesi unaweza sema katundika daruga kuitumikia timu yake ya Taifa,

Achana na sababu za yeye kuchukua maamuzi hayo, acha tuangalie, je Shomari atakuwa na mbadala wake ndani ya kikosi cha Stars? Kwa haraka haraka utabaini kuwa Hassani kessy Ramadhani anayekipiga pale Nkana Red Devils ya Zambia  ndiye anayetarajiwa kuziba pengo lake.

Kiundani acha nikupe  utofauti wa Kapombe na Kessy kiufundi. Hapa tutaangazia ubora wa wachezaji wote uwanjani, pia bila kusahau udhaifu. Tutaangazia aina ya uchezaji wao “playing patterns” na jinsi gani Kessy anaweza kuwa mbadala wa kudumu wa Kapombe ndani ya kikosi cha Ndayiragije Etienne.

SHOMARI KAPOMBE.

Kapombe ni miongoni mwa mabeki visiki wa upande wa kulia kuwahi kutokea. Amejizolea sifa nyingi tangu akichezea Simba, AS Cannes ya Ufaransa kisha Azam na hadi leo yupo Simba tena.

Kapombe ni miongoni mwa mabeki wa pembeni wa kisasa kabisa kutokana na tabia zake kupanda kushambulia na kushuka kulinda na kukaba kama sehemu ya kutimiza jukumu lake mama. Kapombe pia anaweza kucheza vizuri kama kiungo wa kati.

Kama kumbukumbu zako na zangu zitaenda sawa basi utaikumbuka ile mechi dhidi ya Al Masri ya nchini Misri Shirikisho Afrika mwaka 2018, mechi iliyopigwa pale Port Said Stadium na Kapombe alicheza kwa kiwango cha juu katika nafasi ya kiungo.

Katika Mfumo wa 3-5-2 Shomari Kapombe alicheza katika nafasi ya kiungo katika mechi ya marudio dhidi ya Al Masry ya nchini Misri, Shrikisho Africa chini ya Kocha Mfaransa Pierre Lecchantre na Masoud Juma kama kocha Msaidizi.

Uwanjani Kapombe ni miongoni mwa Mabeki Wastaarabu sana kwa maana huepuka faulo zisizo na maana wala tija. Hukaba kwa kutumia akili na kushambulia.

Sifa kubwa ya kapombe ni kujiunganisha na safu yake ya ulinzi na safu ya kiungo. Ukimchunguza vizuri kapombe utabaini kuwa aina ya pasi anazotoa ni za ndani nane kwa maana  kwanza anaweza toa pasi beki wa kati, kutegemea na nafasi iliyopo,

Anaweza kutoa pasi kwa kiungo wa ulinzi au kiungo wa kati kisha yeye hu- overlap ili kuupokea tena mpira.

Kapombe pia anaweza kutoa pasi kwa winga anayecheza upande wake kisha bado akahitaji kuuomba tena mpira ili kupiga krosi.

Sifa nyingine kuu ya Kapombe ni uwezo mkubwa wa kupiga krosi zenye macho yaani zinazoweza kumfikia mlengwa. Tofauti na mabeki wengine, Kapombe ana staili tofauti ya upigaji krosi.

Kwanza anaweza kupiga krosi katikati ya nusu ya mpinzani na kuudondosha mpira katika boksi la mpinzani pia anaweza kupiga krosi akiwa mwisho kabisa karibu na kibendera cha kona na krosi ikawa na macho.

Kapombe pia ni mzuri zaidi katika kupiga V-Pass anapoingia ndani karibu na goli la mpinzani hii ina maanisha kuwa ana uwezo wa kutoka pembeni na kuingia katikati kwenye box la mpinzani.

Kapombe hu-Overlap na kuingia katika Box la timu pinzania na kupiga V-Pass ili kuwafikia wachezaji Wenza na kufunga Goli.

Kubwa zaidi kwa kapombe ni nidhamu ya kimchezo yaani ni adimu sana kumuona kapombe anazawadiwa kadi ya njano au nyekundu kwa kuzozana na mchezaji mwingine au kufanya faulo mbaya.

HASSANI KESSY RAMADHANI.

Kessy hana tofauti kubwa na Shomari lakini kuna baadhi ya vitu wanatofautiana kabisa. Kuna vitu ambavyo Kessy anavyo lakini Shomari hana.

Kwanza kabisa kiufundi Kessy anaweza kucheza kama “Inverted Full back” Kwa maana timu inaposhambulia, Kessy hupanda na kuungana na kiungo wa ulinzi.

Katika mIchezo mingi ya Timu ya Taifa, Kessy hutumia mbinu hii ili kuongeza idadi ya Wachezaji katikati ya kiwanja. Hii huizuia timu pinzani kufanya shambulizi la kushtukiza kwa kupitia katikati pia hutoa wigo mpana kwa timu kuendelea kumiliki mpira kupitia katikati.

Akishaungana naye huwa ni rahisi kwa wao kupiga pasi za one-two kwenda mbele, muda mwingine hutumia mbinu hii kuwahadaa wachezaji wa upinzani na kuwachanganya hasa kwenye mikao ya kimaeneo.

Staili hii ya uchezaji huwa na msaada sana kwa timu ambayo hutumia mashambulizi ya kushtukiza kuanzia nyuma yaani Lower Zone baada ya kuupora mpira katika eneo lao.

Tofauti ya pili, ni uwezo wa Kessy kucheza kama beki wa kati pindi mabeki hao wanapopoteana kimajukumu. Ni mara nyingi kwa Kessy kuonekana akiokoa mpira katikati, eneo ambalo kiufundi kutokana na tukio husika, Beki wa kati angetakiwa kuwa katika eneo muafaka na kufanya uokozi.

Kasi yake humsaidia kufanya yote hayo kwa wakati mfupi na  kwa kiasi kikubwa hufanikiwa.

Tatu, Kessy ni mzuri kwa interception na Tackling. Ni mzuri sana katika kuingilia mchezo na hata kuipora mipira kwa kucheza tackling licha ya kimo chake. Kitu pekee kinachombeba Kessy ni kutokuwa muoga.

Hassani Kessy katika majukumu na timu ya taifa.

Hizo ndizo tofauti kubwa zilizopo. Lakini wachezaji hawa wawili wana sifa zinazofanana ambazo kwa kiasi kikubwa ni sifa za mabeki wa pembeni wa kisasa yaani kulinda kama jukumu Mama lakini kushambulia kupitia pembeni (Overlapping and downlapping).

Lakini udhaifu mkubwa wa Kessy ni kushindwa kudhibiti hisia zake na muda mwingine kukosa nidhamu kabisa ikiwa ni matokeo ya tendo hilo. Ni rahisi sana kwa Kessy kufanya faulo isiyo ya lazima haijalishi ni eneo gani. Hapa mashabiki wa Simba Mtakuwa mmenielewa.

Niambie kwa Staili hizi za Uchezaji unadhani ulikuwa ni muda sahihi kwa Shomari kutundika daruga kuichezea Taifa Stars? Je Unadhani Kessy ndiye Mbadala sahihi wa Kapombe?


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.