Blog

Ibrahim Ajib ndie Anthony Martial wetu?

Sambaza....

Nchini England jijini Manchester kwenye viunga vya uwanja Old Trafford kuna mtaalamu mmoja kutoka nchini Ufaransa anaitwa Anthony Martial, fundi kwelikweli akiwa na mpira mguuni.

Martial alisajiliwa United akitokea Monaco chini ya Muholanzi Luis Van Gal, huenda hii ndio zawadi kubwa ambayo mashabiki wa United wanaikumbuka mpaka leo kutoka kwa Mdachi huyo. Martial ana kila kitu cha  mpira ambacho mshambuliaji wa kisasa anatakiwa kuwa nacho.

Anajua kukokota mpira, ana chenga za maudhi, shabaha ya goli, ana kipaji kwelikweli. Liverpool wana kumbukumbu nae vizuri katika utambulisho wake siku ya kwanza akivaa jezi ya United katika uwanja wa Old Trafford. Alijitambulisha vizuri mbele ya mashabiki ya United tena kwa mahasimu wao wakubwa.

Kijana huyu wa Ufaransa amebarikiwa kipaji kikubwa lakini ni kama anawachanganya mashabiki wake na wa United kutokana na kutokujituma pindi awapo uwanjani. Amekua katika kiwango cha kupanda na kushuka kila siku, hawezi kua na mfululizo wa michezo mitatu mpaka mitano akicheza kwa kiwango cha juu.

Anthony Martial.

Amekua akicheza vizuri na kuwafirahisha katika mchezo mmoja au miwili halafu akaja kuwakera mashabiki katika mchezo unaofuata. Mashabiki wengi wanaamini Martial anauwezo zaidi ya pale alipo huku wakitegemea anaweza kua mchezaji mkubwa na tegemeo kwa United. Hata Ole katika kuijenga United mpya amekua akimuweka kama muhimili katika eneo la ushambuliaji pamoja na Rashford na Daniel James.

Vile ambavyo mashabiki wa United wanamuona  Martial kama mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu na hajafika wanapotaka ndivyo ambavyo Ibrahim Ajib anawachanganya Watanzania wengi waliopo nyuma yake. Wengi wanaamini Ajib bado haja “Offer” kila kitu kilichopo katika ubongo wa mguu wake.

Ibrahim Ajib Migomba

Ibrahim Ajib wa msimu uliopita akiwa na Yanga sio huyu wa leo akiwa Simba, amekua sio tena tegemeo kikosini kama ilivyokua misimu miwili nyuma, huku wengi wakiamini kwa kipaji na uwezo wake hastahili kukalia benchi la Simba.

Ni kama alivyo Martial, Ajib amejaliwa uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuufanya anavyotaka lakini bado hajafikia ile kiu na hamu ya mashabiki wa mpira wanavyotaka. Kipaji pekeakee bila juhudi ni kazi bure na ndicho kinachotokea kwa mafundi hawa wa mpira Anthony Martial na Ibrahim Ajib.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.