Championship League

Ligi Daraja la Kwanza sasa mubashara kwenye TV.

Sambaza....

Hatimae kile kilio cha muda mrefu na matamanio ya Watanzania wengi kimesikika na sasa michezo ya Ligi ya Championship zamani ikijulikana kama Daraja la kwanza sasa itaonyeshwa mubashara kwenye televisheni.

Kampuni ya Startimes kupitia chaneli yake ya TV 3 leo wameingia makubaliano na Bodi ya Ligi ya kuonyesha michezo yote iliyobaki ya Ligi ya Championship ambapo michezo hiyo iliyobaki itaanza kurushwa Machi 25 mwaka huu.

Mkurugenzi muendeshaji wa TV3  Ramadhani Msemo amesema wao wanaona ni fursa muhimu kwao kuonyesha Ligi hiyo lakini pia akawakaribisha wadau wengine wa soka katika kulisogeza mbele soka la nchi.

“Tunawataarifu rasmi sasa TV3 tumeingia makubaliano na Bodi ya Ligi yakuonyesha michezo yote ya Ligi Daraja la kwanza inayojulikana kama Championship League. 

Moja ya mchezo wa Ligi ya Championship uliopigwa katika Dimba la Uhuru uliowakutanisha Transit Camp na Fountaine Gate

Hii kwetu ni nafasi yakipekee na tunawakatibisha wadau wote waje tuungane na Bodi ya Ligi ili kuendelea kuboresha maendeleo ya soka nchini,” alisema Ramadhani Msemo.

Nae msemaji wa Bodi ya Ligi Karim Boimanda amesema Ligi ya Championship ni miongoni mwa Ligi Bora katika ukanda huu kwasababu ina wachezaji wengi bora wanaocheza Ligi hiyo.

Karim Boimanda “Ligi hii ina mvuto sana tena wakipekee katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, kama utachukua Championship Ligi yetu halafu ukaipambanisha na Ligi kuu nyingine za ukanda huu basi utagundua hii Ligi ni bora na inabebwa na ubora wa wachezaj.”

Pia Karim Boimanda aliongezea kwamba kilikua ni kilio cha muda mrefu nasasa wanashukuru maana pia itawavuta wadhamini na kuongeza ubora wa Ligi.

Msemaji wa Bodi ya Ligi Karim Boimanda

“Tunawashukuru wenzetu wa TV3 wameitikia wito wa muda mrefu na hili ni jambo kubwa kwa Taifa letu na kwa ukuaji wa Ligi zetu. Lengo letu kubwa ni kuitangaza Ligi yetu na kuwavutia wadhamini ili tupate Ligi bora yenye ushindani,” alisema Karim Boimanda

Makubaliano hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa Mlimani City ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka pamoja na waandishi wa habari za michezo nchini.

Mpaka sasa Ligi hiyo kinara ni JKT Tanzania wa Ligi hiyo wakiwa kileleni na alama zao 53 wakifwatiwa na Pamba pamoja na Kitayosce zinazoshika nafasi ya pili na yatatu.

 

 


Sambaza....