Stori

Nitakwenda na Saidoo, Inonga na Diarra Chini ya Kocha Nabi

Sambaza....

Tayari TFF kupitia kamati yake ya tuzo tayari imeshafanya uteuzi wa wachezaji mbalimbali watakaowania tuzo katika maeneo mbalimbali msimu katika Ligi zote zilizo chini ya TFF.

Kamati hiyo imetangaza tuzo za Ligi Kuu ya NBC, Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti, Championship Ligi,  First Ligi na kombe la FA !ambapo wachezaji wameshawekwa katika makundi mbalimbali ambayo ni pamoja na kocha bora, kiungo bora, mlinzi bora, kipa bora na baadhi ya tuzo zingine ambazo zitatolewa siku ya tuzo.

Katika Ligi Kuu ya NBC kuna tuzo ya mchezaji bora, kocha bora, kipa bora, beki bora na mchezaji bora wa Ligi hiyo na hapa ndio nitapatazama zaidi katika makala hii ya leo katika mtandao wako pendwa kabisa wa Kandanda.

Nasraddine Nabi.

Katika eneo la kocha bora pasi na shaka kura yangu inaangukia kwa kocha wa Yanga Nasraddine Nabi. Katika kinyang’anyiro hicho kocha Nabi yupo pamoja na Hans Plujim (Singida Big Stars) na Robert Oliveira (Simba sc). Nabi ameiongoza Yanga kutetea taji lao la Ligi Kuu huku akipoteza mchezo mmoja pekee huku pia akiwa katika fainali ya FA.

Nasraddine Nabi ameongeza uwezo wa wachezaji wengi wa Yanga na kupelekea timu yake kucheza kwa ubora mkubwa, ikishinda mechi nyingi tena kwa ubora mkubwa ikiwa pia ni timu yapili nyuma ya Simba kufunga mabao mengi. 

Kwa upande wa mlinzi bora nitakwenda na Henock Bacca wa Simba mbele ya kina Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wa Yanga pamoja na Shomary Kapombe na Mohamed Hussein wote wa Simba. Inonga amekua muhimili katika ulinzi wa Simba na kuifanya ngome ya Simba mpaka sasa iwe imeruhusu magoli 15 pekee mpaka sasa (magoli machache zaidi katika Ligi).

Mlinzi wa Simba Henock Inonga Baka akishangilia bao la kwanza la Simba katika mchezo dhidi ya Yanga.

Henock anastahili kutetea tuzo yake aliyoibeba msimu uliopita kutokana na ubora mkubwa aliouonyesha lakini pia hata takwimu pia zipo upande wake, mpaka sasa ana mabao matatu katika Ligi, lakini pia akiiongoza Simba kutoka uwanjani bila kuruhusu bao katika zaidi ya michezo 15 ya Ligi. Unapaswa ukumbuke goli lake pia dhidi ya Yanga katika mchezo wa debi.

Katika tuzo ya kipa bora hakuna ubishi Djigui Diara wa Yanga anastahili kutwaa tuzo huyo na kuitetea baada ya kuitwaa msimu ulimalizika. Akiwa ndie kipa mwenye “cleansheet” nyingi zaidi ya Aishi Manula wa Simba na Benedict Haule wa Big Stars anaoshindania nao tuzo.

Diara amekua na mchango mkubwa kwenye kuisaidia timu yake kutetea ubingwa akicheza kwa nafasi kubwa kama kipa wa kisasa ambae anaifanya timu yake ianzie kucheza kutokea chini kama kocha Nabi wa Yanga anavyotaka.

Djigui Diarra.

Katika eneo la kiungo wakati huu kumekua na ushindani wa hali ya juu kutokana na majina ya wanaowania tuzo lakini pia kumekuwepo na malalamiko kutokana na baadhi ya nyota kutokuwepo katika eneo hilo. Khalid Aucho na James Akamiko wamezua taharuki kutokana na kukosekana kwao. Si hao tu huenda kama Feisal Salum asingekua na mgogoro na timu yake ya Yanga huenda angekuwepo katika kinyang’anyiro hiki.

Yupo Saidoo Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin na Clatous Chama wa Simba, Aziz Ki wa Yanga pamoja na Bruno Gomes wa Singida Big Stars. Mpambano ni mkali katika eneo hili lakini mchango wa mchezaji kwa timu yake pamoja na takwimu ndio kitu muhimu katika kuamua nani ni bora hapa.

Mingoni mwao wote hao ni Saidi Ntibazinkiza ndio mwenye namba nzuri kuliko wengine wote. Saidoo aliyezitumikia Simba na Geita msimu huu amehusika katika mabao 22 mpaka sasa akiwa na mabao 10 na pasi 12 za mabao. Akikatibiwa na Chama aliyehusika katika mabao 18 (magoli 4 na pasi 14 za mabao). 

Saidoo Ntibazonkiza.

Kwangu binafsi nitakwenda na Said Ntibazonkiza wa Simba katika tuzo ya kiungo bora, licha ya kushindwa kuipatia ubingwa timu yake ya Simba lakini amekua na mchango mkubwa kwa timu zote mbili alizozichezea msimu huu (Geita Gold na Simba sc).

Nani mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu huu!? Swali ambalo ni jepesi lakini pia linaweza kuwa gumu kwa upande mwingine. Yupo Fiston Mayele na Djigui Diarra wa Yanga, Said Ntibazonkiza na Mzamitu Yassin wa Simba halafu yupo Bruno Gomez wa Big Stars.

Ni lazima mchezaji bora awe mchezaji aliyefunga mabao mengi? Au ni lazima awe mchezaji aliyehusika na mabao zaidi? Au mchezaji bora anapatikana vipi, vipi kwa upande wa walinzi ama walinda mlango?  Ama kwa vyovyote vile huwezi kuitenganisha tuzo ya mchezaji bora ya msimu huu na Fiston Kalala Mayele kutoka Yanga.

Fiston Mayele.

Amefunga mabao 16 mpaka sasa akiwa na pasi tatu za mabao maana yake amehusika katika mabao 19 ya Yanga. Si tu amekua na muendelezo mzuri akiwa Yanga lakini pia amechangia kwa kiasi kikubwa na kuipa ubingwa Yanga. 

Pasi na shaka kwangu mimi nitakwenda na Saidoo Ntibazonkiza kama kiungo bora, Henock Bacca beki bora na kipa bora Djigui Diarra wakiwa chini ya kocha bora kabisa Nasraddine Nabi. 

 

Sambaza....