Uhamisho

Pawasa: Niligombaniwa Uwanja wa Ndege na Simba na Yanga

Sambaza....

Wapwa, anasimulia Boniphace Pawasa Mchezaji wa zamani wa Simba na Timu ya Taifa ambaye kwa sasa ni Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa upande wa Beach Soccer.

Mpwa wenu nilipata bahati ya kukutana na Pawasa na kupiga nae stori mbili tatu huku akinikumbushia enzi zao na jinsi ambavyo aliziingiza vitani Simba na Yanga.

“Mashabiki wa Tanzania wameingiwa na ugonjwa mbaya sana. Wao wanaamini mchezaji bora ni yule anayetoka nje ya nchi, akitambulishwa mzawa wanalalamika,” alisema Pawasa na kuongeza

“Nakumbuka mimi nilisajiliwa wakati nipo kidato cha tano  Makongo Sekondary. Tulikuwa tunatoka kwenye mashindano ya shule, msafara wetu ulipofika uwanja wa ndege tuliwakuta maafisa wa Yanga na Simba wakinisubiri.”

Boniface Pawasa akiitumikia Simba mwaka 2003 katika mchezo dhidi ya Asec Mimosa.

Pawasa anaendelea kusimulia na kusema hata hivyo hakuweza kuonana nao wala kukutana nao licha ya kumfuata yeye uwanjani hapo.

“Mkuu wa msafara mwalimu, alipowaona akaniambia ingia kwenye basi la shule kisha tukasondoka. Alijua hao jamaa wana mambo yao hakutaka wanichukue pale.”

“Baadae nikiwa shule watu wa Yanga walikuja tukafanya mazungumzo wakaondoka. Baadae nikaitwa ofisini nikajiuliza nimekosa nini!? Kufika ofisini nikaambiwa Simba wamekuja, wameshakulipia ada ya miaka miwili wanataka ujiunge nao.

“Basi ikabaki kufanya mazungumzo binafsi mimi na Simba. Hiyo ndio sababu iliyofanya niende Simba SC.”

Boniface Pawasa kocha wa Timu ya Taifa ya soka la ufukweni.

Pawasa anasema Yanga wamelamba dume kwani mchezaji waliemsajili Nickson Kibabage ni chaguo sahihi kabisa na ni mchezaji wa kiwango kikubwa, lakini pia ametoa masikitiko yake akisema wazawa hawathaminiwi.

“Zamani wachezaji wazawa tulikuwa tunathaminika sana, sio kama sasa hivi. Yanga kumtangaza Kibabage mashabiki wanalalamika wakati ni usajili mzuri kabisa.”

“Yule bwana mdogo anauzoefu, amecheza Morocco, akarudi Mtibwa kiwango kikapanda Singida wakamchukua. Naamini ni mapendekezo ya benchi la ufundi kwenda Yanga, ataongeza kitu kikubwa.”

“Kwa usajili wa ndani kuna quality gani iliyo nje ya Simba na Yanga kwa fullback inayomzidi Kibabage ?!. Hakuna,” alimalizia kocha huyo wa soka la ufukweni.

Sambaza....