Ligi Kuu

Simba Wanazihitaji Alama Tatu Zaidi Kuliko Yanga.

Sambaza....

Aprili 16 Jumapili hii ndio mwisho wa majigambo, kelele na nyodo kwa Watani wa Jadi kwani ndio mchezo wa mwisho wa Ligi watakaokutana msimu huu baada ya mchezo wa raundi ya awali kumalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.

Imekua tofauti kidogo wakati huu wawili hao wakikutana kwani ni kama mbio za ubingwa zimemalizika hivi baada ya Yanga kukaa kileleni kwa alama nane na Mnyama Simba akionekana amekata tamaa za ubingwa na kuwekeza nguvu zaidi katika michuano ya FA.

 

Dabi hiyo namba tano kwa ubora Afrika inapigwa  katika Dimba la Benjamin Mkapa imeonekana kuwa ni muhimu zaidi kwa Simba kupata alama tatu licha ya kwamba huenda zisiongeze chochote katika kuwania ubingwa lakini zitakua na maana kubwa kwa mashabiki wao.

Kuna sababu tatu ambazo zinafanya ushindi kwa Simba uwe muhimu sana kwao. Sasabu ya kwanza ni kufuta uteja mbele ya Yanga, kutimiza ahadi mbele ya wanachama wao na kumaliza msimu kibabe.

1. Kufuta Uteja Mbele ya Yanga!

Mara ya mwisho Simba kumfunga Yanga ilikua ni mwaka 2019 katika mchezo wa raundi ya pili kwa bao la Meddie Kagere, wakati mara ya mwisho kumfunga Yanga katika michuano yote ni July 2021 katika fainali ya FA mkoani Kigoma kwa goli la Thadeo Lwanga.

Thadeo Lwanga akifunga bao mbele ya walinzi wa Yanga katika fainali ya Kombe la FA Kigoma katika uwanja wa Lake Tanganyika.

Tangu mwaka 2019 Simba hajamfunga Yanga kwenye Ligi amekua akipokea kichapo ama kutoka sare, wakati kwenye Ngao na FA amekua akifungwa kabisa. Na mara ya mwisho Simba alipokea kipigo cha mabao mawili kwa moja katika Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu na msimu uliopita alifungwa bao moja bila katika nusu fainali ya FA.

Ni wazi sasa mchezo wa Jumapili viongozi, wachezaji na mashabiki watataka kumaliza uteja huu na kutaka kumfunga Yanga.

2. Kutimiza Ahadi ya Kumfunga Mtani.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Simba zilizomuweka madarakani Mwenyekiti Mangungu tena kwa mara ya pili aliahidi mbele ya Wanachama wa Simba miongoni mwa vitu vitakavyofanyika ni kwanza kumfunga Mtani ambae hawajamfunga kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu.

Lakini pia hata msemaji wao Ahmed Ally akiongeza na waandishi wa habari hivi karibuni amesema anawataka wachezaji wao waingie katika historia ya kuwafunga Yanga na kuzidi kutengeneza historia katika mioyo ya wapenzi na wanachama wa Simba.

3. Kumaliza Msimu Kibabe.

Ni dhahiri shahiri Simba wana nafasi finyu ya kutwaa  ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani mpaka sasa wapo alama nane nyuma ya Yanga huku michezo mitano pekee ikiwa imebaki kumalizika kwa Ligi. Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa robo fainali watakutana na Wydad Casablanca.

Tumaini pekee la Simba limebaki katika kombe la FA ambapo watakutana na Azam Fc nusu fainali na endapo watashinda watakutana na mtani wao tena Yanga ama Singida Big Stars.

Hivyo ni wazi kumfunga Yanga Jumapili kutawafanya walau kufuta machozi ya kukosa ubingwa lakini pia kumtibulia sherehe za ubingwa mtani wake.

Jesus Moloko wa Yanga akimtoka mlinzi wa Simba Mohamed Hussein “Tshabalala”

Kwa Upande wa Yanga!

Yanga wao ni wazi wataingia katika mchezo huo wakiwa kifua mbele kwani hawana presha yoyote kutokana na historia nzuri mbele ya Mnyama waliyonayo hivi karibuni.

Hata kama Yanga watapoteza katika mchezo huo lakini bado watakua na uongozi wa alama tano mbele ya Mnyama na bado watakua na michezo mitano mbele yakulinda uongozi wao na hatimae kutwaa ubingwa.

 

Sambaza....