Sambaza....

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba Sports Club imepangwa kuanza na mabingwa wa zamani wa nchini Kenya AFC Leopards katika michuano ya SportPesa Super Cup inayotazamiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.

Mnyama Simba watacheza mchezo huo Januari 23 na kama watafanikiwa kuifunga AFC Leopards basi watakutana na mshindi walima alzeti Singida United ama Bandari ya kutoka nchini Kenya ambao wao watacheza Januari 22.

Aidha mabingwa watetezi Gor Mahia ya Kenya wao watakuwa na kibarua kizito watakapoanza kwa kuchuana na kigogo wa vigogo Mbao FC kutoka jijini Mwanza mchezo ambao utapigwa Januari 23.

Mshindi wa mchezo atakutana na ama bingwa wa kihistoria wa Tanzania Bara Dar Young Africans au Kariobangi Sharks ya Kenya ambao wao watacheza Januari 22.

Ikumbukwe kuwa bingwa wa michuano hii atapata nafasi ya kucheza na timu ya Everton kutoka nchini Uingereza katika tarehe ambayo itapangwa hapo baadae.

Sambaza....