Blog

Unayakumbuka matukio haya? Matukio 10 yaliyoitikisa ligi msimu wa 2018/19.

Sambaza....

Wakati tunajiandaa na kipute kipya cha msimu wa ligi kuu Tanzania bara 2019/2020 sio mbaya kama tukakumbushana baadhi matukio, rekodi na vimbwanga vilivyojitokeza msimu uliopita.

Kumbukumbu hizi huenda zikatujenga kwani Waswahili walisema mtu hukosea njia wakwati wa kwenda tu na wala sio wakati wa kurudi. Hata hivyo kufanya kosa sio tatizo, tatizo ni kurudia kosa ulilokwisha wahi fanya.

Mambo haya, mengine yaliongeza ladha ya ligi na mengine yalipunguza ladha kabisa, matukio mengine ni rekodi, na mengine ni aibu. Nimekukusanyia matukio haya na kukuwekea pamoja.

MFUMO WA PLAYOFF

Mapema mwezi July, shirikisho la soka Tanzania TFF, Kupitia kamati yake ya Utendaji, ilibadili mfumo wa kuzipata timu zinazopanda na kushuka daraja.

Mfumo huu uliigawanya ligi daraja la kwanza kuchezwa katika makundi mawili yenye timu 12, huku kila timu itakayoongoza kundi lake ndiyo inayopanda daraja huku timu zilizoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kundi hucheza mechi za Mchujo nyumbani na ugenini ili kupata timu mbili zitakazoungana na timu zitakazoshika nafasi ya 17 na 18 za ligi kuu kucheza Playoff.

Mfumo huu huzishusha daraja jumla jumla timu zilizoishia nafasi ya 19 na 20 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara.

LIGI BILA MDHAMINI MKUU.

Msimu wa mwaka 2017-18, ligi kuu ilikuwa ikidhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Kama Mdhamini Mkuu na ndio maana ilikuwa ikifahamika kama VPL yaani Vodacom Premier League.

Msimu uliopita hakukuwa na mdhamini kuu, Viongozi wa TFF, muda wote waliwahadaa wadau wa soka nchini kwa kudai kuwa, mdhamini mkuu atapatikana muda si mrefu.

Lakini hadi Simba anakabidhiwa ubingwa , ligi imemalizika bila mdhamini mkuu. Athari ya hili ni timu nyingi kukosa japo fedha za kujikimu kwani Mdhamini mkuu alikuwa akizisaidia timu nyingi yakiwemo masuala ya vifaa na usafiri.

Udhamini wa Vodacom ulikuwa ni wa miaka mitatu na wenye thamani ya bilioni 6.6. kujitoa kwa Vodacom kulizifanya klabu kukosa milioni 80 zilizokuwa zinatolewa katika awamu nne yaani kila awamu ni milioni ishirini.

Udhamini huo pia uliambatana na zawadi za washindi wa ligi, ambao walipewa shilingi milioni 80.4, mshindi wa pili ,milioni 40.2, wa tatu 28.7, wan ne 22 na timu yenye nidhamu ilipata milioni 17.

Bila kusahau mchezaji bora na mfungaji bora kila mmoja alipewa shilingi milioni 5.7, kipa bora milioni 5, huku kocha na mwamuzi bora walipewa milioni 8.6 kila mmoja.

Hadi ligi inamalizika bodi ya ligi imeshindwa kabisa kupata mdhamini mkuu.

 KAGERA SUGAR KUSHUKA DARAJA KIMIZENGWE.

Hii ndio timu pekee iliyojikusanyia alama zote sita, yaani nje ndani kwa bingwa wa ligi Simba SC, lakini pia ndio timu iliyoshuka kwa sheria ngumu ya head to head yaani kama ni chuo unaweza iita ni “TECHNICAL SUP”.

Mambo yapo hivi, Mechi za mwisho ndio zikuwa na maana kubwa kwa timu nyingi ikiwemo Kagera Sugar na Stand United.

Kagera Sugar na Stend United zimejikuta zinafanana kwa kila kitu yaani zote zimejikusanyia alama 44, na tofauti ya magoli  hasi 11 na kati ya hizi mbili moja inatakiwa ishuke daraja na nyingine ikacheze Playoff na Pamba FC.

Katika utata kama huu, na kwa mujibu wa sheria za TFF, kinachofuata kuangaliwa baada ya alama kuwa sawa, tofauti ya magoli kuwa sawa ni tofauti ya magoli katika mechi za ligi zilipokutana yaani ‘Head to head’.

Na katika hili, Mchezo wa kwanza uliopigwa pale shinyanga, matokeo yualikuwa ni sare ya 1-1, na mchezo wa raundi ya pili pale Kaitaba, Kagera alilala nyumbani kwa goli 3-1, hivyo kuna tofauti ya mabao mawili,,,, na hatimaye Kagera Sugar inashuka daraja..

Kipindi haya yote yanatokea, kumbe Msimamo wa TFF ulikuwa na kasoro, Kumbe Kagera Sugar ilibidi ndio wakacheze Playoff na Stand United Washuke daraja jumla jumla…Tff bhana we acha tu.

GADIEL MICHAEL KUFANYIWA TUKIO LA KINYAMA..

Beki wa kushoto wa Yanga kipindi hicho, Gadiel Michael,katika Msimu huu wa ligi alifanyiwa mambo mengi lakini kwa bahati nzuri, kijana huyu ni mstaarabu sana na inafika wakati namfananisha na Beki kisiki wa zamani wa Simba na Taifa stars ya Maxio Maximo Juma Jabu JJ.

Miongoni mwa matukio aliyofanyiwa ni zile rafu mbaya dhidi ya James Kotei wa Simba zilizosababisha Kotei kufungiwa baadhi ya michezo lakini Bora hizi rafu, Gadiel dhidi ya Alliance ya Mwanza, alishawahi kufanyiwa tukio lililowahi kumfanya Juma Nyosso afungiwe baada ya kumfanyia tukio kama hilo John Bocco.

Gadiel Michael

Lakini kwa bahati mbaya hakukuwa na aliyelalamika licha ya ushahidi wa video kusambaa mitandaoni na kuonyesha kilichotokea.

ALAMA 93 ZA SIMBA

Klabu ya Simba ndio klabu iliyomaliza ligi ikiwa na alama 93, alama ambazo zina maana kubwa sana kwa soka letu na klabu ya Simba.

Kwa harakaharaka tu, Alama hizo ndizo alama kubwa zaidi ya timu mabingwa katika ligi mbali mbali katika ukanda wa Afrika mashariki. Wote tuanajua kuwa ligi yetu inatimu 20, maana yake Simba amecheza mechi 38, ameshinda mechi 29,sare 6,kupoteza michezo mitatu na tofauti ya magoli 62.

Kenya, bingwa ni Gor Mahia, akicheza mechi 33 akiwa na alama 71, Uganda Bingwa ni KCCA akiwa na alama 66 katika michezo 30, Rwanda bingwa ni Rayon Sports akiwa na alama 69 katika mechi 29 aliyocheza na Burundi ni Algo Noir ikiwa na alama 68 katika mechi 30 iliyocheza.

Ili kujua Simba amekusanya alama nyingi zaidi, chukua mechi zilizozidi kwa Simba zidisha na alama za ushindi yaani 3 kisha jumlisha na alama za timu husika zilizopo, na majibu yatakuwa hivi..

Gormahia ya Kenya itakuwa na alama 86, KCCA ya Uganda alama 90, Na Algo ya Burundi itakuwa na alama 92 .

COASTAL UNION KUWASILI SIKU YA MECHI KUTOKA TANGA.

Ni tukio ambalo lilitikisa sana, Yaani Coastal Union ilitoka jijini Tanga kwa Costa mpaka Dar ndani ya siku moja na kucheza mechi.

Ilisafiri zaidi ya kilometa 196 sawa na mile 122, kisha ilifanikiwa kucheza mechi dhidi ya Bingwa wa sasa, timu ya Simba.

Hatrick Mbili katika mchezo mmoja, Emmmanuel Okwi na Meddie Kagere wakijizolea mipira yao, Coastal walilala kwa goli 8 kwa moja.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu 2018/19

Ushindi huo, ulimfanya Meddie Kagere kuwa mchezaji aliyeifunga Coastal Union Goli nyingi zaidi, ameifunga goli 5 katika msimu mmoja pia kipigo hicho ndicho kipigo kikubwa zaidi katika ligi msimu uliopita.

Madai ya Coastal kuwasili siku ya mechi yalithibitishwa na kocha wa timu hiyo Juma Mgunda na kudai kuwa timu yake ilivuna ilichokipanda.

  KELVIN YONDANI KUPOKWA UNAHODHA.

Yondani amedumu katika kiti cha unahodha kwa miezi 6 pekee kabla ya kitambaa hicho kupewa   Ibrahim Ajib Migomba.

Baada ya aliyekuwa nahodha wa Yanga Nadir Haroub Canavaro kustaafu soka, mwezi July mwaka 2018 na kupewa jukumu la Umeneja, kitambaa chake kilichukuliwa na Kelvin Yondani.

Yondani alipewa wasaidizi wawili ambao ni Juma Abdul Mnyamani na Thaban Sikala Kamusoko ambao wangemsadia katika majukumu yake ya Unahodha.

Lakini matukio ya nidhamu mbovu ya Kelvin Yondani yalimfanya Zahera kumvua kitambaa hicho na kisha kumvisha Mr. Assist, Ibrahim Ajib hii ilikuwa ni mwezi wa kwanza mwaka 2019 kabla ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga.

 BENO KAKOLANYA KUACHWA KATIKATI YA SAFARI.

Hayakuwa maamuzi rahisi kwa kocha Mwinyi Zahera kumuacha mchezaji tegemeo na golikipa namba moja wa Yanga, Beno Kakolanya.

Beno aliachwa kwa sababu kuu mbili, kwanza ni tabia zake za kugomea mazoezi kama sehemu ya shinikizo la kutaka kulipwa malimbikizo ya madeni yake kwa Yanga zikiwemo fedha za usajili.

Beno Kakolanya

Pili ni kutokana na wakala wake. Kocha Zahera alionekana kushangazwa sana na kitendo hicho cha mchezaji kutoka timu hasimu kuwa na wakala mwenye nafasi ya uongozi kutoka timu pinzani kwa maana ya Simba.

Suleimani Haroub ambaye ni mjumbe mpya katika bodi ya wakurugenzi Simba ambaye pia alikuwa katibu mkuu wa chama cha soka mkoa wa mbeya (MREFA) ndiye wakala wa Beno, kitendo ambacho kilimfanya Mwinyi zahera kutomuamini tena Beno na kumuacha kabisa katika kikosi chake.

Baada ya kuachwa na Yanga, Beno alihaha na wengine wakidai huenda angetimkia Zambia na wengine wakidai anawindwa na Mnyama Simba SC, pia Beno aliipoteza nafasi yake ya golikipa namba mbili katika kikosi cha Stars chini ya kocha Emmanuel Amunike.

Kwa kuzingatia sababu hii ya pili toa maoni yako hapo chini, je kuna ubaya wowote kwa mchezaji wa Yanga kuwa chini ya wakala ambaye ni shabiki au kiongozi wa Simba? Na hata kinyume chake?

ZAHERA ALIA KAMA MTOTO, AGEUKA MWOKOZI JANGWANI.

Mwinyi Zahera, Papaaa, kuna wakati aliitwa hadi profesa! Majina yote haya ni kutokana na juhudi zake zisizo na kikomo katika kuhakikisha anaisimamia timu hasa wachezaji na benchi zima la ufundi na kuhakikisha timu inapata matokeo chanya licha ya hali ya uchumi kuwa mbaya klabuni hapo.

Katika kipindi chake cha uongozi kama kocha mkuu msimu uliopita, alianza majukumu yake rasmi kwa kukaa kwenye benchi la Yanga katika mechi dhidi ya Simba, lakini MIsimamo yake na maamuzi yake yaliifanya klabu isiyumbe kiasi cha kuhama katika reli.

Zahera alitumia hadi fedha zake kutoa motisha kwa wachezaji, Zahera alishawahi kutoa machozi hadharani kule mkoani mbeya kwa kuitetea Yanga pekee, ZAHERA alikuwa tayari kuitetea Yanga na kuisemea popote aendapo.

Hakuwahi kuogopa kuisema TFF kwa kulinda maslahi mapana ya Yanga, Zahra aliwaheshimu Mashabiki zaidi kuliko hata viongozi wa klabu yake waliokuwa wanaleta mambo ya ajabu.

Kama ulikuwa hujui, Zahera alishawahi kutishia kuondoka Yanga kama wanachama na wanayanga nchini watashindwa kuichangia klabu hiyo ili kupata fedha za usajili, aliyafanya haya yote ili kuifanya Yanga inakuwa ni klabu yenye ushindani na kutoyumba kwa kiasi kikubwa.

Kiufupi zahera alikuja kuifundisha Yanga akiwa tayari ni shabiki lia lia wa klabu hiyo

BOCCO KUFIKISHA MABAO 114.

Jumapili ya September 23 mwaka 2018 huenda ndio tarehe iliyokuwa ya furaha zaidi kwa Mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Raphael Bocco baada ya Simba ya Simba kuitungua Mwadui fc goli 3-1 ugenini huku Bocco akitupia goli mbili na kumfanya afikishe jumla ya goli 100 katika ligi.

Goli hizo 100 zinamfanya John Bocco kuwa binadamu wa kwanza kuifikia hiyo rekodi tangu kuanzishwa ligi kuu Tanzania bara.

Sherehe ya kufurahia kuifikia rekodi hiyo iliingia doa baada ya dakika ya 81, Bocco kupewa kadi nyekundu, baada ya kufanya tukio lisilo la kiungwana la kumpiga ngumi beki  Revocatus Mgunga na kumpelekea kupewa adhabu ya kuzikosa mechi kadhaa ikiwemo dhidi ya Mtani wao Yanga.

Hadi ligi imemalizika, Bocco alikuwa na jumla ya magoli 114, huku 16 akiyafunga katika msimu uliopita.

Kwa upande wangu naishia hapa,  Niambie wewe unayakumbuka matukio gani mengine?

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x