Blog

Xavi! Kinda wa Kidachi aliekimbizwa Barca na Raiola

Sambaza....

Nikiwa kwenye daladala ninasikiliza stori za konda aliyepiga mvinyo kiasi, ghafla nikaona jumbe inaingia kwenye simu yangu tena Instagram toka kwa mjuzi wa Soka mmoja ikisema “Huyu Xavi dunia inamsubilia kwa hamu. Ipo sku tutakua mashabiki zake.”

Shauku ikaniijia, nikakumbuka huyu dogo nilishawahi kumfuatilia japo sio kwa undani, ila kwakua kwetu nilifunzwa kuwasikiliza wakubwa na kutendea kazi maono yao basi ikabidi nizame chimbo kumtizama zaidi huyu Xavier Quantin Shay Simons ni nani.

Bwana wee! Mkubwa hakosei, huyu dogo ni tajiri saana wa soka hapa tunazungumzia tuzo, makombe, pesa na rekodi kibao.

Mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka saba Barcelona walimsajili kwenye akademi yao kinda huyu akitokea CD Thader ya huko kwao Uholanzi na kuanza kupewa mafunzo na misingi ya La Masia.

Xavi alidumu pale Barcelona kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuchukua tuzo ya Ballon d’Or kwa vijana wadogo mara nne, pia alikua mchezaji bora kwa madogo hao aliyehusudiwa na kutabiriwa makubwa zaidi kwa baadae.

Miaka tisa baadae akiwa na miaka 16 anakuja kuvunja mioyo ya Viongozi, mashabiki na wadau wa Barcelona baada ya wakala wake Mhuni Mino Raiola kumaliza mchezo kimafia na kumuuza Paris Saint-Germain.

Vuta picha dogo kanolewa kwa miaka tisa, mbinu na falsafa za ki’La Masia zote kapewa na akitarajiwa kuwa nembo ya Barcelona lakini wakala Mino anamchukua na kwenda kuvuna pesa PSG, hii iliwauma sana Barcelona.

Nikirejea kwenye stori zangu na mjuzi mmoja aliwahi kuniambia “Raha ya Rasta/Nywele ndefu kwa mchezaji awe anaujua mpira” kisha nikamtizama dogo akiwa dimbani nikasema Naam! huyu mtoto katafsiri semi ya mjuzi huyu.

“Box to box midfielder” Nywele zinaenda kushoto, mpira unapita kulia yeye anuwahi mbele, kiuhalisia anavutia kumtizama sana.

Kwa wanaomjua wakala Mino Raiola lazima wakubali kuwa jamaa ni mhuni, panga pangua mshahara anaolipwa dogo kwa mwaka pale PSG si chini ya billioni mbili za kibongo (£1m.) na hapo ana umri wa miaka 17 tu.

Simon Xavi

Nje ya hayo Xavi tayari anamkataba na kampuni ya Nike, hapa viwalo vyote na njumu wanasimamia wao na bado analipwa, kumbuka pia bado yupo kwenye timu ya vijana pale PSG hajapandishwa kwa wakubwa japo tarehe tano mwezi huu aliweza kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sochaux akiwa na timu ya wakubwa bila kusahau amecheza timu zote za vijana za taifa la Uholanzi.

Hayo ni mafanikio makubwa sana kwa kijana mdogo kama huyo na ni mambo ya kuigwa na wenye ndoto kubwa katika soka.

 

Sambaza....