Tetesi

Yanga yamtaka beki mwenye rekodi ya kipekee

Sambaza....

 

Ligi kuu Tanzania bara mpaka sasa hivi imesimama kutokana na ugonjwa wa Corona. Lakini pamoja na kusimama kwake , mazungumzo ya namna ya kuirudisha ligi hii yanaendelea vizuri.

Watu wengi mpaka sasa hivi wanasubiri ni siku gani ambayo ligi hii itarejea tena ili kumpata bingwa wa ligi kuu Tanzania bara pamoja na timu ambazo zitashuka daraja.

Kikosi cha Kagera Sugar kilichoaanza dhidi ya Yanga.

Msimu huu wa 2019/2020 kuna beki mmoja wa Kagera Sugar , David Luhende ambaye mpaka sasa hivi ndiye mchezaji pekee anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi zote 29 za ligi kuu na mechi tatu za kombe la shirikisho.

Kwa jumla msimu huu David Luhende , beki wa kushoto wa Kagera Sugar amecheza mechi 32 na mechi zote kacheza dakika zote tisini kwenye kila mechi, kwa hiyo kwenye msimu huu kacheza jumla ya dakika 2,880 kwenye mechi 32.

Kutokana na kiwango chake kuimarika kwa kiasi kikubwa , timu ya Yanga imeonesha nia ya kutaka kumsajili David Luhende kutoka kwenye klabu ya Kagera Sugar.

Tetesi ambazo zinazidi kuenea ni kuwa baada ya Gadiel Michael kuondoka na kwenda kwa wapinzani wao wakubwa nchini Simba , Yanga wameshindwa kupata beki mwingine wa kushoto mwenye kiwango kikubwa.

Hivo kutokana na kiwango kikubwa kilichooneshwa na David Luhende , Yanga wameonesha nia ya wao kumtaka tena. David Luhende aliwahi kupita pia kwenye klabu hii.

Alipotafutwa kuulizwa kama atakuwa tayari kurudi kwenye klabu yake ya zamani , David Luhende alisema kuwa yeye kazi yake ni mpira wa miguu kwa hiyo yuko tayari kufanya kazi sehemu yoyote ambayo kuna maslahi.

“Mimi kazi yangu ni mpira wa miguu niko tayari kwenda kucheza klabu yoyote tu ambayo itanitengenezea mazingira mazuri ya mimi kunifaika na kazi yangu”- alimalizia beki huyo kisiki

Sambaza....