Sambaza....

Sijui “wahenga” walikuwa ni watu wa aina gani ! najiuliza walikuwa wakiwaza nini hadi wakasema “hakuna marefu yasiyokuwa na ncha”? maana kila ninachokiona lazima kina mwanzo wake na kitakuwa na mwisho wake pia.

Mwakilishi pekee wa Nchi na kanda ya Mashariki na kati katika  mashindano ya kimataifa, Simba SC tayari imesha safiri kuelekea kule DRC Congo kuwavaa Pomboo Weusi, AS Club Vita katika mchezo wao wa pili katika kundi D klabu bingwa barani Afrika.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa inaongoza kundi kwa kujikusanyia alama 3 na magoli matatu  kibindoni baada ya kuwachalanga Waarabu JS Saoura  katika mechi ya awali iliyochezwa hapa Tanzania.

Kwa upande wao AS Club Vita wao wapo katika nafasi ya tatu, baada ya kuruhusu magoli mawili kutoka kwa Al ahly ugenini katika mchezo wao wa kwanza. Club Vita wataingia na moto katika mchezo wao dhidi ya Simba kwa kuwa wanajua nini wanatakiwa wapate wakiwa pale Stade des Martyrs, Kinshasa.

Klabu kama Simba bila shaka malengo yake makubwa ni kuhakikisha inashiriki katika michuano ya kimataifa yaani Klabu bingwa au shirikisho Afrika. Miongoni mwa mipango ya Simba na Kocha Patrick Aussems ni kuhakikisha Simba inafika hatua ya makundi, ambapo lengo hili tayari limeshafanikiwa, lengo la pili ni kutetea taji la TPL, na hapa ndipo hadithi inapoanzia.

Kimataifa Simba tayari wameshajikusanyia alama 3, huku wakijipanga zaidi kule Congo wapate alama nyingine 3, au 1 ili wajiwekee nafasi kubwa ya kufuzu hatua inayofuata. Na kwa bahati mbaya kama mambo yataenda mrama  maana yake Simba watahitaji kuchukua kombe la TPL ili kupata nafasi ya kushiriki klabu bingwa mwishoni mwa mwaka huu.

“THIS IS SIMBA” ndio kaulimbiu iliyowatoa Simba kutoka hatua ya mtoano hadi kufikia hatua ya makundi. Kaulimbinu hizi huasisiwa na msemaji wa klabu, Haji Manara ambaye anaonekana kutumia nguvu nyingi kubuni jinsi ya kuwakusanya mashabiki wa Msimbazi katika mechi zake za nyumbani na ugenini. “This is Simba” iliasisiwa rasmi Agosti 8, katika tamasha la Simba “Simba Day”.

Kauli hii ilitumika vizuri kuwavuna Mbabane Swallows ya Eswatini, nyumbani na Ugenini, ikaja kumalizwa na kipigo cha ugenini dhidi ya Nkana Red Devils ya Kitwe nchini Zambia cha goli 2-1.

Baada ya matokeo hayo, Simba ilitakiwa kupata goli moja tu, kisha ifuzu hatua ya makundi, hapo ndipo “KUFA   AU KUPONA” ilipoanzia. Kauli hii ilizaa matunda kwani Simba ilipona kwa ushindi wa goli 3-1 katika uwanja wa nyumbani. Kauli hii iliondoka na matumaini makubwa kwa klabu, kwani iliwafanya wapenzi wa Simba na wadau wa soka nchini kuvijaza viti 60,000 vya uwanja wa taifa, yaani hadi lile jukwaa la wa upande wa pili nalo lilijaa wekundu na weupe wote ukiliita jina la Chama na Kagere.

Simba haikuishia hapo, ikafanikiwa kufuzu na kuingia hatua ya makundi na ikajikuta inaangukia kundi D.  Baada ya kuanguakia  huko, Simba ikaja na kaulimbiu nyingine ambayo ndiyo inayotumika hadi sasa ya “YES WE CAN”, ikiwa na maana ya “  Ndio Tunaweza”.

“YES WE CAN” kaulimbiu ya klabu ya Simba katika harakati za kusaka pointi katika michuano ya kimataifa. kauli hii iliasisiwa na msemaji wao Haji Manara.

Hivi unadhani kwa klabu kama Al ahly inaweza kuja na kaulimbiu kama hii? Klabu ambayo ina uzoefu mkubwa katika mashindano haya?. Kauli hii hutumiwa na watu ambao hujihisi wanadharaulika mbele ya washindani wake. Barack Obama aliitumia kaulimbiu hii katika uchaguzi wa Marekani na kisha akawa Rais, hata yeye alikuwa akidharaulika, akionekana hawezi kuwa Rais akiwa na asili ya Aufrika Mashariki.

Unakumbuka zile kauli za Simba ni “Underdog”?  naam! zile zimechangia kwa kiasi kikubwa ujio wa kauli hii. Simba ilijua imeshaanza kudharaulika, ikionekana ndio timu ya kuchukua  pointi nyumbani na ugenini. Lakini huwezi amini, endapo Simba ikishinda mbele ya AS Vita Club basi itakuwa imepiga hatua kubwa sana kuelekea hatua inayofuata.

Mlango wa Simba kupitia klabu bingwa, unafunguka japo si rahisi kwa kuwa timu zote zina nafasi kubwa. Ukitaka kujua hilo angalia matokeo ya mechi za awali, timu zote zilizocheza mechi za awali nyumbani zimepata matokeo, na zile zilizocheza ugenini katika kundi D zimepoteza, hivyo tuwapime AS Vita mbele ya Simba nyumbani kama watapata matokeo, na kama wakipata ugumu wa kufuli la mlango huu linazidi kuwa gumu kuvunjika.

Achana na njia hiyo ya klabu bingwa Afrika, njia ya pili Simba kucheza michuano ya Kimataifa, ni kwa kubeba kombe la ligi kuu. Huku ni kugumu zaidi, kwani kila kukicha Yanga inapata ushindi, ushindi wao unaikosesha Simba afya njema kuelekea kucheza michuano ya kimataifa mwishoni mwa  mwaka huu, matokeo wazuri ya Yanga yanaitesa Simba.

Simba tayari imeshacheza michezo 14, ikijikusanyia alama 33, ikiwa ni tofauti ya alama 20 na Yanga waliopo kileleni na alama zao 53 wakiwa wamecheza michezo 19. Hesabu hapa ni rahisi tu, maana yake Simba wana viporo vya mechi 5, mbele ya Yanga.  Thamani ya mechi hizo ni alama 15 ambapo ukijumlisha na alama za sasa, 33 unapata alama 48, bado kutakuwa na tofauti na alama 5 na anayeongoza ligi.

Andrew Vicent Dante akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Azam. Yanga na Azam zipo kileleni katika msimamo wa TPL, huku Simba ikiwa nyuma kwa tofauti ya alama 20 na anayeongoza ligi.

Kwa Simba, kujumlisha na kutoa sio hesabu ngumu, lakini hesabu ngumu kupata ushindi katika mechi zote 5 za viporo. Kumbuka kuna timu kama Mbao, yenyewe imeshacheza michezo 22, hii ni tofauti na michezo  8 kwa Simba.

Alama 5, mbele ya Yanga kimahesabu ni sawa na kuifunga Yanga yenyewe katika mchezo wa mzunguuko wa pili, kisha Yanga kutoka sare na Azam (najaribu kuwaza), mambo yakiwa hivi basi Yanga na Simba watakuwa sawa. Lakini tujiulize je mambo yatakuwa rahisi hivi?

Simba itaandamwa na presha kubwa wakati wa kuvila viporo vyake, tofauti na Yanga ambayo tayari imeshacheza mechi zake na kupata matokeo. Pia  kuanzia duru la pili timu zote zitahitahi kutoshuka daraja na nyingine kusaka nafasi nne za juu na zingine kubeba ubingwa, kwahiyo usishangae kuona Simba ikisimamishwa na Ruvu Shooting ya Masau Bwire hata kama Ruvu haipigani kushuka daraja au kubeba ubingwa, lakini kuifunga au kupata sare na Simba ni faraja kwao.

Kula viporo ni kazi ngumu, na kama ni kazi ngumu basi kuna watakao sema Simba haiwezi kuvila viporo vyake bila kuchacha, hapo ndipo kaulimbiu ya “YES WE CAN” itakapotawala tena midomoni  mwa Wanasimba.

Kauli hii itasikika tena wakati ambao Simba itaandamwa na presha za mashabiki na mechi za viporo, itasikika wakati ambao wachezaji wataaonyesha uchovu baada ya mechi za klabu bingwa na bado wanahitaji matokeo, itasikika wakati ambao Yanga inazidi kuongeza tofauti ya alama  kwa kushinda mechi zake za nyumbani na ugenini.

“YES THEY CAN” ndio wanaweza, Simba wanaweza kufanya kila kitu hapa duniani ikiwemo kubeba ubingwa wa klabu bingwa Afrika na kisha kubeba kombe la TPL, lakini juhudi kubwa na mikakati vinahitajika kufanya yote hayo. Simba itafanya hivyo ikifanya vitu vinne ambavyo hivi hapa;

Kwanza, kuwa na kikosi kipana chenye ushindani. Najua wachezaji nao ni binadamu kuna wakati wanachoka, wachezaji hutumia nguvu nyingi katika mashindano magumu kama klabu bingwa, hivyo huchoka. Itawawia vigumu kucheza mechi zote za klabu bingwa na ligi kuu katika kiwango sawa.

Dawa yake ni kuwa kikosi chenye watu wenye ushindani, yaani asipocheza Emmanuel Okwi akapewa nafasi  Adam Salamba basi ajitahidi aipe timu matokeo kama ambavyo angefanya Okwi, hiyo ndio dhana kamili ya kikosi kipana na chenye ushindani, sio una wachezaji wengi lakini wana tofauti kubwa kiviwango ujue hapo bado unakikosi kifinyu au chembamba.

Pili, kupunguza presha kwa wachezaji. Umuhimu wa mechi huongeza presha kwa wachezaji, na kama wachezaji hawa hawatoandaliwa kisaikolojia basi watajikuta hawafanyi vizuri kutokana na  presha kubwa. Presha itatengezwa na umuhimu wa viporo vyenyewe, maana itafika wakati Simba inataka matokeo lakini kiporo nacho kinataka matokeo maana  kila timu itakuwa na matumizi na matokeo hayo, hapo ndipo presha inapoongezeka.

Sergie Paschal Wawa ” Baba mwenye nyumba” beki mahiri wa Simba katika majukumu yake uwanjani. Anasifika kwa kuwa kiongozi ndani ya uwanja na kupunguza presha ya mashambulizi kwa washambuliaji wa timu pinzani.

Tatu, kuwa na nidhamu ya mchezo. Bila shaka zile za kupanga kupanga kikosi cha kawaida kwa madai ya kufanya “rotation” zitapungua. Kufanya mzunguuko kwa wachezaji ni jambo jema  baada ya kupata matokeo, lakini kocha atalaumiwa kama atafanya hivyo wakati kuna tofauti kubwa ya viwango vya wachezaji waliopo uwanjani na waliopo benchi. Simba itahitaji kuheshimu kila mechi, yaani kila mechi kwao ni fainali na si vinginevyo.

Nne, ni kutekeleza hayo yote niliyoyataja juu. Huwezi ukapunguza presha kutoka kwa mashabiki  tena kama wa Simba endapo tu utafungwa na timu ndogo kwa kuchezesha wachezaji wa kawaida ukilinganisha na umuhimu wa mechi. Kwa timu za Simba na Yanga presha za mashabiki huwaondoa makocha wengi. Aussems akae na kulitazama hili kwa jicho la tatu, kila mechi kwake iwe fainali.

Lakini mwisho wa siku, hii kaulimbiu ya “YES WE CAN” naamini ipo siku itatumika kusaka alama ndani ya ligi kuu Tanzania bara, tena wakati ambao mwenye njaa ndiye anayeonekana  kunenepa, na tajiri  ndiye anayeonekana kuteseka kwa kiu na njaa.

Sambaza....