Sambaza....

Kama uongozi wa juu unatangaza na kufanya uhamasishaji mkubwa kwa wanachama na wapenzi wa klabu kuichangia timu yao nani mwingine anayejitokeza na kuisemea klabu kwamba ‘neema‘ imerejea?

Boaz Ikupilika- mwenyekiti wa matawi ya klabu ya Yanga SC anapaswa kuelewa ana fanya makosa makubwa- pengine anaihujumu klabu yake kwa taarifa ambazo amekuwa akizitoa kwa waandishi wa habari.

Mtu huyu (Boaz)amekuwa akinukuliwa mara kwa mara akizungumzia kuhusu hali ya kiuchumi klabuni Yanga- tena kana kwamba hakuna shida yoyote tangu mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuph Manji alipojitokeza hadharani kwa mara ya kwanza kuiunga mkono timu yake ilipocheza na USM Alger mwezi uliopita katika Caf Confederation Cup.

Ndiyo, inawezekana Manji ametoa ahadi ya kurejea katika nafasi yake aliyokuwa amejiuzulu na kuahidi mambo mazuri lakini Boaz anapaswa kujua kuwa Yanga wanafahamu hali ya kiuchumi ilivyo klabuni mwao ndiyo maana wanachangisha michango kwa wanachama na wapenzi wa timu yao.

Boaz Mfano, amenukuliwa akisema kuanzia mchezo ujao wa Yanga mwenyekiti- Manji ameahidi kutoa Tsh. 10 million kama bonasi ikiwa watashinda mechi. Sawa inawezekana ni kweli, lakini kama taasisi Yanga ina ofisa wake habari- Dismas Ten- huyu ndiye anapaswa kusema yale muhimu yanayoendelea klabuni.

Na hii haipaswi kuwa kwa Boaz tu, wanachama wengine pia wa klabu wanatakiwa kuachana na tabia ya kuiongelea Yanga hasa katika mambo muhimu. Yanga ina msemaji wake anayetambulika. Kuongea ongea na waandishi kuhusu Yanga kwa nia ya kujikuza hakufai.

Yanga wanapaswa kuangamiza kirusi hiki cha Boaz sasa na si kuwashutumu wanahabari kama walivyofanya wikend iliyopita. Wawadhibiti wanachama waopotosha kama Boaz .

Sambaza....