Sambaza....

WANACHAMA/ mashabiki na wapenzi wa Yanga SC wanaweza kupinga kila kitu- kumkataa mwenyekiti wao wa muda, Thobias Lingalanagala, Shirikisho la soka nchiniTFF na hata Baraza la michezo Tanzania ( BMT), lakini katu hawawezi kumshawishi, Yusuph Manji kurejea kuwa mwenyekiti wa klabu yao kwa mara nyingine.

BARUA YA KUJIUZULU

Nimewahi kuandika miezi kadhaa iliyopita kuwa, Manji kamwe hawezi kurejea kuongoza klabu hiyo kutokana na misukosuko aliyoipata mwanzoni mwaka uliopita. Bado naamini hivyo na uthibitisho kuendelea kwake kuaa kimya huku akiamini barua ya kujiuzulu aliyoandika Mei, 2017 ni uthibitisho sahihi.

Manji kwenye moja ya Mechi za Yanga

Manji alishaandika barua ya kujiuzulu Mei mwaka jana- mwezi mmmoja baada ya kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa kwa miezi karibia mitatu kutokana na tuhuma mbalimbali.

Ndio, alipotoka tu gerezani alikwenda kukutana na wachezaji, benchi la ufundi ambao kwa miezi kati ya February- April, 2017 walikuwa na migomo ya kutocheza mechi na wakati mwingine mazoezi kutokana na kutolipwa mishahara yao.

Licha ya kwamba alifahamu hatoweza kuwalipa wachezaji wake, Manji kama ´mtu hasa wa Yanga´ alitumia mbinu ya kiuongozi ili kurejesha hamasa ndani ya timu, hadi kwa wanachama na mashabiki. Kujitokeza kwake akiwa mwenye afya njema kuliwafanya hata wale wanaoegemea upande mwingine kiushabiki kufarijika.

Namna Yanga walivyotwaa ubingwa wao wa mwisho wa ligi kuu Tanzania bara- ambao ulikuwa ni wa tatu mfululizo, ilikuwa ni dalili mbaya, na kama Manji hasingetoka kizuizini kabla ya April- katu Yanga isingetwaa ubingwa Mei, 2017.

Yanga iliyokuwa ikianza kuyumba kiuchumi February, 2017 mwezi mmoja bila uwepo Manji aliyekuwa mahabusu taratibu ilianza kupoteza ubora na kuangusha pointi katika ligi kuu, Machi, 2017 wakaondolewa na Zanaco FC katika Caf Champions League hatua ya mwisho kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi.

Haitoshi, wakakutana na kipigo bab-kubwa kutoka US Alger mwezi April na kuondolewa katika Caf Confederations Cup walikoangukia baada ya kuondolewa katika ligi ya mabingwa Afrika. Wakatema ubingwa wa FA baada ya kuchapwa na Mbao FC katika nusu fainali, mwisho wakatwaa ligi mwezi Mei kutokana na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa dhidi ya mahasimu wao Simba SC.

CLEMENT SANGA MWANZILISHI WA ´MANJI ATAREJEA YANGA´

Tazama, siku chache tu baada ya kumalizika kwa msimu wa 2016/17, Manji aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti. Nakumbuka wakati ule ( Mei 2017) baada ya kujiuzulu kwake, nilimpongeza mno Manji na upande wangu nilimtazama kama kiongozi wa mfano katika soka letu.

Haraka nilishauri klabu kuingia katika uchaguzi wa kujaza nafasi mwenyekiti. Naamini, Manji alihitaji kuona Yanga ikipata mwenyekiti mpya kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili katikati ya mwaka 2017. Alikuwa la funzo alilolipa wakati akiinusuru klabu na anguko baya Agosti, 2012 kutoka kwa utawala wa wakili Lyod Nchunga.

Clement Sanga aliyekuwa makamu mwenyekiti chini ya Manji ndiye chanzo cha yote haya. Aliwaaminisha watu wa Yanga kuwa Manji atarejea. Akakaimu nafasi ya uenyekiti- mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu. Sanga akasisitiza Manji atarejea baada ya miezi mitatu. Mwisho mwaka, hakuna Manji wala kivuli chake.

Kocha Mzambia, George Lwandamina licha ya kuongoza timu kushinda michezo saba mfululizo katika ligi na kurejea katika mbio za taji akaachana na timu kwasababu za kiuchumi February, 2018, ni kweli timu ilifanikiwa kufuzu makundi katika Caf Confederations mwezi April, lakini kiwango cha timu kilishuka mno uwanjani. Wakapoteza ubingwa Mei, 2018 wakiwa dhaifu sana wakipitwa zaidi ya pointi 15 na mahasimu wao Simba.

 

Manji na wachezaji wa Yanga

Kwa mtu asiyejijali binafsi atamuonea huruma Manji na kumshukuru kwa yote aliyochangia Yanga na mpira wa Tanzania. Hata kabla ya kuwa mwenyekiti Manji alijidhihirisha ´kama mwanamapinduzi wa kweli kwa wachezaji wa Kitanzania´ ndio maana nyota wengi walipenda kuichezea Yanga katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Mchezaji ghali wa kwanza Mtanzania wa kizazi kipya ni Juma Kaseja Juma. Golikipa huyo bora wa muda wote wa karne mpya alihitimisha misimu sita mfululizo ya kupenda klabuni Simba na kukubali kiasi kisichopungua US dollar 30 na mshahara usiopungua Tsh. Milioni moja za Yanga, mwezi Juni 2008.

Manji ni mtu aliyekuwa akitoa kwa hiari yake, siwezi kujua alichohifadhi moyoni mwake kama anaipenda Yanga ama la, lakini kwa alichoifanyia klabu hiyo kati ya mwaka 2006 hadi 2017 ni dhahiri anaipenda mno Yanga. Lakini kwa sasa hana cha kufanya.

Ingawa Sanga na baadhi ya watu wa Yanga wanasahau kuwa Manji alilazwa pia mara kadhaa kutokana na maradhi wakati yupo kizuizini, wanasahau pia akaunti zake zilishikiliwa huku makampuni yake kadhaa pia yakisemekana kufungwa.

Umefika wakati wa Yanga kuamini wataendelea kumkumbuka Manji lakini ni lazima mtu mwingine aendeleze uhai wa klabu yao na si kukubali kuiua mikononi mwa shujaa wao-Manji. Wamuache apumzike kwani ndio njia bora ya kuthibitisha mapenzi yao ya dhati kwake.

Kuendelea kumng´ang´ania wakati mwenyewe anaona hawezi ni usariti mkubwa- kwa maana kutomtii mtu ni usariti mkubwa sana. Kwanini mnamsariti hadharani shujaa wenu?

Sambaza....