Makambo
Ligi Kuu

Ni wakati wa Tambwe kumpa ‘sumu‘ Makambo ‘awaangamize‘

Sambaza....

UKIACHANA na tatizo la timu kuanza kuchoka dakika ya 75, katika mchezo wake wa kwanza katika ligi kuu Tanzania Bara mshambulizi Heritier Makambo ameonyesha anaweza kuibeba timu yake ya Yanga SC msimu huu katika ufungaji.

Alikuwa msumbufu kwa walinzi wa kati wa Mtibwa Sugar FC, na aliweza kufunga goli la kwanza la msimu kwa timu yake akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa juu zaidi na mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael dakika ya 32‘ katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Agosti 23 iliyopita.

MSHAMBULIZI HURU.

Ukiachana na uchezaji wake wa kuhamahama eneo lote la kati katika mashambulizi, Makambo anaweza kumpa mbinu zaidi kocha wake- Mcongoman mwenzake, Zahera Mwinyi endapo wakati mwingine akiamua kuchezesha timu yake katika mfumo wa kujilinda na mashambulizi timilifu ya kushtukiza.

Makambo anaweza kudhibiti mpira kando ya walinzi wa timu pinzani na kuufanyia maamuzi. Anaweza kugeuka haraka na mpira- jambo zuri kwa mshambuliaji. Bado anatakiwa kutafuta kasi na kucheza pasi za ‘Nipe Nikupe- One, Two‘ ili apate pasi nyingi sahihi za mwisho.

Mrundi, Amis Tambwe anaweza kuwa mwalimu mzuri kwa Makambo. Tambwe alitamba Tanzania kwa magoli yake ya kichwa, na umaliziaji wa kiwango cha juu akiwa ndani ya eneo la hatari.

Haroun Chanongo, Ramadhani Singano walimsaidia mno Tambwe kufunga magoli yalitokana na krosi- za juu ama chini. Wakati Betram Mwombeki akimsaidia magoli mengine mengi yalitokana na pasi za one-two katika msimu wake wa kwanza Tanzania Bara akiwa mchezaji wa Simba SC msimu wa 2013/14.

Saimon Msuva, krosi za beki wa kulia, Juma Abdul, Oscar Joshua na Mwinyi Hajji kutoka upande wa kushoto- pasi za kupenyeza za Haruna Niyonzima na zile za Nipe Nikupe kutoka kwa Donald Ngoma zilimpaisha Tambwe na ndani ya msimu yake mitatu katika ligi kuu pekee alifunga jumla ya magoli 55- magoli 34 akiifungia Yanga katika msimu mmoja na nusu.

Amis Tambwe

Nguvu ya Makambo ni sababu nyingine ya kuamini mchezaji huyo atafanya vizuri hata atakapotakiwa kuongoza mashambulizi kama mshambuliaji huru. Naamini Juma akirudisha krosi zake timilifu kutoka upande wa kulia na Gadiel akaendeleza anachofanya katika beki tatu ya kushoto, Makambo atahitaji pia pasi za mwisho za Ibrahim Ajib ili kujaribu kuweka rekodo zake.

Ni wakati wa Tambwe kumpa sumu Makambo awaangamize wapinzani wa Yanga. Juma tukumbushe zile krosi zako bomba, mng‘arishe Makambo awapaishe kama alivyofanya Tambwe.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x