Ligi Kuu

Sababu Tatu kwanini Manji na Kaseke wanaweza kurudisha ligi kuu Yanga

Sambaza....

Jambo muhimu kwa timu inayohitaji ubingwa ni kushinda michezo yake mingi ya nyumbani kadri inavyowezekana, Yanga SC kwa kiasi kikubwa iliangushwa na matokeo yake ‘mabovu’ katika uwanja wa nyumbani msimu uliopita. Waliangusha alama 17 licha ya kwamba walipoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Azam FC Mei 28.

Sare saba ambazo ni dhidi ya Lipuli FC Agosti 28 mwaka uliopita katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi ilikuwa ‘ya kichovu’, baadae Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, Simba SC, Mwadui FC, Singida United, Ruvu Shooting nazo zilifuata nyayo za Lipuli na kufanikiwa kuondoka na pointi moja mbele ya Yanga katika uwanja wake wa nyumbani.

Kushindwa kuifunga Prisons iliyocheza pungufu kwa muda mwingi wa mchezo pale Azam Complex Chamanzi mwezi mwishoni mwa Novemba, 2017 kulionyesha wazi kuwa kikosi kilikuwa na sifa kadhaa za kupoteza ubingwa ambao waliushikilia kwa misimu mitatu mfululizo ( 2014/15, 2015/16 na 2016/17)


-Kuwakosa wachezaji muhimu na mbadala wa Niyonzima na Dida

Naamini kitendo cha kuwakosa kwa muda mrefu washambuliaji Amis Tambwe, Donald Ngoma huku wachezaji waliosajiliwa kuziba mapengo yaliyoachwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Deo Munishi ‘Dida’ wakishindwa kufikia walau nusu ya matarajio, na misukosuko ya adhabu na ‘utoro’ wa Obrey Chirwa kulichangia kuipunguzia timu hiyo makali.

Lakini sasa angalau Yanga wana kikosi kipana na licha ya baadhi ya watu kukibeza kikosi chao msimu huu lakini kimtazamo kimeimarika zaidi ya vile kilivyokuwa msimu uliopita. Urejeo ya Kaseke na winga mshambulizi Mrisho Ngassa ni ongezeko lenye faida kwa timu ambayo ilikosa wachezaji wazoefu katika safu ya mashambulizi msimu uliopita.

Kaseke ataongeza nidhamu ya kawaida na ile ya kimchezo kwa wachezaji vijana kama Yusuph Mhilu na Maka Edward ambao wameonyesha mwanga mzuri tangu walipoanza kupewa nafasi na kocha aliyepita George Lwandamina.

Feisal Salum ‘Fei Toto’ bado hajajidhihirisha kama mchezaji wa kiwango cha juu anayestahili kuanza mbele ya Thaban Kamusoko lakini uwepo wake ni ongezeko linguine lenye faida kwa timu. Mohamed Issa ‘Banka’ naye anaonekana ni usajili wa bei rahisi lakini isisaulike kuwa kati ya Septemba hadi Disemba, 2017 wengi walikuwa wakisema ni kiungo bora anayetawanya vizuri pasi zenye macho.

Kwa ujio huu wa Kaseke, Ngassa, Feisal, Banka bila shaka kikosi kimepata nguvu mpya inayoweza kuwafikisha salama Disemba ijayo ambapo kunatarajiwa kufanyika usajili mwingine wa kiwango cha juu zaidi. Kuna wakati ambao Yanga ilimuhitaji Ibrahim Ajib lakini mchezaji huyo hakuwa tayari, sasa ujio huu wa kina Ngassa unaweza kuisukuma zaidi timu hata mchezaji Fulani anapokosekana.

Naamini Yanga wamejitahidi kadri ya walivyoweza kusaini timu kutokana na mapungufu yaliyoonekana msimu uliopita na safari hiii hawataangaika kuziba mapengo kwani Ngoma, Chirwa na Hassan Kessy walioondoka hawakujidhihirisha kama wachezaji wa kiwango cha juu klabuni hapo katika misimu yao miwili, lakini walikuwa na mchango mkubwa.

Rafael Daud, Pius Buswita walionyesha kiwango cha wastani msimu uliopita na walitoa mchango wa kuridhisha ndani ya uwanja, Thaban na Papy Tshishimbi, na Said Juma Makapu nni kundi linguine ambalo linafanya kiungo cha Yanga kuimarika kuielekea mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mtibwa kesho Jumatano katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


-Usajili wa dirisha dogo

Kama kweli wanahitaji kurudisha ubingwa wao msimu huu, Yanga wanapaswa kuongeza baadhi ya wachezaji katika nafasi za beki wa kulia na ile ya kati, mshambulizi mmoja na kiungo mmoja mchezesha timu.

Mchezaji mpya Heriter Makambo ameonekana anaweza kuwa msaada mkubwa kwa safu ya mashambulizi ya Yanga, na Kaseke katika michezo miwili aliyoichezea katika Caf Confederations Cup ameonyesha atakuwa msaada mkubwa katika ufungaji pia, lakini ukitazama kwa jicho la tatu, Tambwe si yule tena kutokana na majeraha.

Matheo Anthony na Juma Mahadhi si washambuliaji ambao wanaweza kukupa kitu unapowahitaji katika wakati mgumu na huku kukiwa na mashaka mengi kuhusu mwenendo wa Ajib, huku Mhilu akitumia muda mwingi kucheza kama mshambulizi wa kwanza msimu uliopita, hii ndio sababu inayonifanya kuamini mshambulizi mpya wa daraja la juu anahitajika.

Katika ulinzi, Vicent Andrew na Kelvin Yondan wanaweza kuanza kutengeneza historia yao ‘kama beki pacha’ yenye mafanikio klabuni baada ya muunganiko wa aliyekuwa nahodha Nadir Haroub na nahodha wa sasa Kelvin kufikia tamati kufuatia kustaafu kwa Nadir.

Lakini wasiwasi wangu ni kwamba kwa misimu miwili iliyopita Andrew bado hajafanya kile ambacho mashabiki wanakitaraji kutoka kwake, wakati Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akiendelea kujifunza kuhusu kumiliki mpira, kuanzisha mashambulizi na kupiga pasi ni wazi Yanga inapaswa kuongeza beki mmoja wa kati katika usajili wa dirisha dogo.

Kuondoka kwa Kessy kunamaanisha Juma Abdul hana msaidizi katika beki ya kulia na isisahulike ni mara chache sana Juma ameweza kucheza walau michezo 10 mfululizo bila maumivu. Hii ni nafasi nyingine ambayo kama itafanyiwa nyongeza nzuri Yanga itapambana vizuri na inaweza kushinda ubingwa msimu huu.

Kushoto hakuna shida kubwa, lakini ni wazi walinzi wa upande huo Gadiel Michael na Mwinyi Hajji wanapaswa kujiimarisha katika ulinzi kutokana na mara nyingi kushindwa kurejea haraka katika nafasi zao pindi wanapoongeza nguvu ya mashambulizi mbele.


-Kurejea kwa Manji

Baada ya mwaka mmoja na miezi kadhaa bila la uwepo wa mwenyekiti wa klabu Yusuph Manji atimaye ureo wake unaweza kumfanya kocha Mwinyi Zahera kupata nafasi ya kuwekeza mbinu zake kwa utulivu. Zahera asiwe na wasiwasi kwa sababu kikosi hikihiki hata kabla ya maboresho kiliweza kucheza michezo saba mfululizo pasipo kuangusha pointi katika ligi kuu msimu uliopita.

Inamaanisha wanaweza kufanya vizuri ikiwa watatulia zaidi huku wakiwa na uhakika wa kupata mishahara yao kwa wakati na si tarehe 90 kama ilivyokuwa. Bila shaka Manji anarejea na kuamsha morali upya klabuni, na kama alivyoahidi kuwa atafanya usajili bab-kubwa katika dirisha dogo na kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha klabuni kwa msimu mzima Yanga wataonyesha kiwango zaidi ya kile walichokionyesha Jumapili iliyopita walipowachapa USM Alger 2-1 katika Confederations Cup.

Urejeo huu utaondoa zile sare za ‘kichovu’ Dar es Salaam na vipigo vya kufadhaisha ugenini kama vile kutoka kwa Prisons ( Sokoine) Mwadui ( Kambarage) na Mbao FC ( Kirumba)

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x