Sambaza....

Uongozi wa klabu ya Singida United inayoshiriki Ligi kuu ya soka Tanzania bara, umekanusha vikali taarifa kuhusu mshambulaji wao Danny Lyanga, kufungiwa kucheza mpira na Shirikisho la soka Duniani (FIFA)

Taarifa za awali zilisema kuwa, mshambuliaji huyo amefungiwa kwa kipindi cha miezi na Shirikisho la soka Duniani FIFA, baada ya kugundulika kuwa amesaini mkataba na Singida United huku akiwa bado ni mchezaji wa Fanja FC ya Oman

Akiongolea suala hilo Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema ameshangaazwa na taarifa hizo huku akisisitiza kuwa Lyanga ni mchezaji wao halali

“Sisi ndio tuliofanya mawasiliano na Fanja FC pia na FIFA, na sisi ndio wenye taarifa rasmi kuhusu mchezaji huyu ni mali ya nani”

“Unaweza kuona hii sio taarifa ya kweli, hatuwezi kuwa na release ya mchezaji ambaye amesaini mikataba miwili au ana mkataba na klabu nyingine, mchezaji wetu hajafungiwa na FIFA kilichotokea ni kwamba Daniel Lyanga tulichelewa kupata ITC yake na dirisha likawa limefungwa hivyo ITC yake bado ipo kule kule Fanja”

Aidha Sanga, alivitaka vyombo vya habari kuwa makini na wanapopata taarifa kutoka kwa watu ambao sio rasmi, ni vema wakawasiliana na uongozi wa Singida United ili kupata uthibitisho wa taarifa za klabu hiyo

“Na hii naomba uwe ni utaratibu tu, kwa watu ambao wanapenda kuchukuwa taarifa na kupeleka kwenye vyombo vya habari, bila kufanya mawasiliano na uongozi wa klabu, Singida United ni timu ya kampuni ina uongozi wake na watu ambao wanapaswa kuulizwa na wakatoa majibu sahihi” aliongeza kiongozi huyo

Sambaza....