Blog

Yondan si Roy Keane, anapaswa kupevuka sasa.

Sambaza....

INAKERA sana pale unapocheza kwa nguvu na kujitolea kwa ajili ya kuisaidia timu yako ipate ushindi- alafu unaona mchezaji mwenzako anapoteza mpira ´kizembe´ huku pia akipitwa kirahisi.

September 2002 niliwahi kuona moja ya maamuzi ya kushangaza na yaliyonifanya nimfuatilie sana Roy Keane. Katika pambano la ligi kuu England, nahodha huyo wa zamani wa Manchester United, Keane alimchapa mtama beki wake Philip Neville.

Keane (Kushoto) wakati akiwa Man Utd
Keane (Kushoto) wakati akiwa Man Utd

Keane alikuwa akikutana na ´maadui´ zake Micky McCathy na Matt Holland waliokuwa na kikosi cha Sunderland. Awali, miezi mitano nyuma akiwa kocha mkuu wa Jamhuri ya Ireland, Micky alimvua kitambaa cha unahodha Roy wakati wa maandalizi kuelekea fainali za kombe la dunia mwaka 2002- Korea Kusini na Japan.

Uamuzi huo haukumpendeza Keane hivyo aliamua kujiondoa kabisa katika majukumu ya timu ya Taifa. Matt alipewa nafasi hiyo. Siku wanakutana kwa mara ya kwanza na Keane baada ya utata uliotokea Mei 2002 katika kambi ya timu ya Taifa- walipaswa kupeana mikono kabla ya kuanza kwa mchezo.

Keane alikuwa nahodha wa United, Matt captain wa Sunderland, Micky safari hii alikuwa meneja wa ´Paka Weusi´. Katika hali ya kawaida, Keane hatapenda kupoteza kama huu na alipoona Neville amepoteza mpira mara tatu na kucheza faulo karibu na eneo lao la hatari akaamua kumchapa mtama ambao Neville aliustukia na kuruka kwanja la nahodha wake.

833A6437
Yondani (Kulia) akipambana na Kagere (Kushoto)

KELVIN YONDAN

Kila napokuwa namuona nahodha wa Kelvin Yondan akiwafokea wenzake mara baada ya yeye kucheza faulo huwa natamani kujua nini huwa kinapita katika akili yake. Lakini Naweza kufahamu ni kwanini huwa vile kwa sababu ni hali niliyowahi kuipitia, hivyo nina uzoefu nayo.

Kuna siku alimfokea na kumlaumu sana Nadir Haroub mara baada ya Amis Tambwe kuifungia Simba SC goli katika mchezo wa Nani Mtani Jembe mwezi Disemba, 2013. Kwa lugha ya mwili Kelvin alionekana kana kwamba anamlalamikia Nadir huku akisema-si nukuu rasmi, ゛Wewe ni mzembe sana, kwanini umeshindwa kumzuia Tambwe na kutufunga kirahisi hivi…゛

Kama walinzi Pacha wa kati, Kelvin alikuwa mbele akifuatilia shambulizi lililokuwa likija upande wao, kati alikuwepo Tambwe katika ulinzi wa Nadir na nyuma kidogo alikuwepo mlinzi wa kushoto, Oscar Joshua kama sijapoteza kumbukumbu. Kelvin alichukia baada ya Tambwe kumtoroka haraka Nadir na kuwahi krosi ya chini mbele yake ( Kelvin) na kufunga goli kirahisi.

Ilikuwa ni busara, ama pengine uanamichezo wa Nadir maana hakujibu shambulizi lolote na ninaamini tukio lile lilimjenga zaidi Nadir na kuimarisha uhusiano wake mzuri kimpira na Kelvin.

Juzi katika mchezo wa ´Pacha´ ya Dar es Salaam, wakati Kelvin anachomoka kwa kasi kutoka nyuma zaidi kumuwahi mchezaji wa Simba kabla hajafika ndani ya eneo la hatari- nilimwambia kakayangu tuliyekuwa tukitazama wote mchezo huo;

“Yondan lazima, anakwenda kucheza faulo. Ana hasira na namna wanavyoshambuliwa na wenzake wanavyocheza.゛Dakika hiyo hiyo akaruka kwa kasi kwa miguu yote miwili na lengo ilikuwa kumuumiza kabisa Meddie Kagere kama sijakosea.

Busara ya mwamuzi, Jonesia Rukyaa ilimuepusha mlinzi huyo wa kati na kadi nyekundu ya moja kwa moja. Alipoonyeshwa kadi ya manjano akaanza kuwafokea viungo wake- labda Feisal Salum na Papy Tshishimbi. Alifoka kwa sababu aliona wanapitwa kirahisi na kushindwa kudhibiti mpira.

Jambo zuri kwake ni kwamba ana uwezo mkubwa wa kucheza na kadi ya njano lakini umefika wakati wa yeye kupunguza hasira pale wenzake wanapofanya makosa na kutopoteza utulivu wake.

Yondani  (Kushoto) akishuhudia moja ya shambulizi
Yondani (Kushoto) akishuhudia moja ya shambulizi

Nakumbuka sana tukio lile la Keane mwaka 2002- kumkosa mtama Phill kutokana na upotezaji wake wa mpira mara kwa mara kisha kucheza faulo karibu na eneo lao la hatari, lakini ni yeye ( Keane) aliyekuja kucheza faulo iliyozaa goli pekee la Sunderland katika sare ya 1-1, huku akiondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko hasimu wake Matt-mfungaji wa goli la Sunderland.

Keane alifungiwa michezo mitano na FA kutokana na hasira zake. Kelvin ni beki mzuri, ana uzoefu mkubwa, ni kiongozi jasiri lakini anapaswa kupevuka zaidi na kudhibiti hasira zake zinazotokana na makosa ya wachezaji wenzake ili awe mchezaji bora na aliyepevuka kiuongozi.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x