La Liga

Hatma ya kocha Solari bado shakani licha ya ushindi dhidi ya Valladolid.

Sambaza kwa marafiki....

Real Madrid jana wamepata ushindi muhimu na ukifuta majonzi ya karibu majuma mawili baada ya kuwachapa Real Valladolid kwa mabao 4-1, lakini kwa uhalisia ilikuwa ni mechi ya mwisho kwa Santiago Solari kuwepo Santiago Bernabeu kama angepoteza mchezo huo.

Lakini hata hivyo kidonda cha kupoteza mataji matatu mfululizo ndani ya siku saba tena kwenye uwanja wao wa nyumbani kinamuweka katika nafasi mbaya zaidi Solari licha ya ushindi mnono wa hapo jana.

Real Madrid hawapo tena kwenye mbio za ubingwa wa La Liga baada ya kuzidiwa kwa alama 12 na wapinzani wao Barcelona, lakini pia waliondolewa kwenye michuano ya Copa del rey na mahasimu wao Barcelona vilevile wakaondolewa kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Ajax Amsterdam.

Alipoulizwa kama anafahamu kuwa mchezo dhidi ya Real Valladolid ni wa mwisho kwake, kocha Solari mwenye umri wa miaka 42 alisema “Siwezi kujitahimini mwenyewe, mimi nitaendelea kuweka mkazo kwenye kazi…….Tutaendelea kufanya kazi kama kawaida, ni jambo la kawaida sana kusikia kelele hasa kutokana na matokeo mabovu ya wiki iliyopita, lakini bado tuna moyo wa mapambano kama ilivyo jadi yetu, kuendelea kupambana kuelekea katika michezo iliyombele yetu na kujaribu kuchukua alama zote tatu,”.

Mkurugenzi wa klabu Emilio Butragueno alilikwepa swali kama ana uthibitisho kuwa kocha Solari ataendelea kuwepo klabuni hadi mwishoni mwa msimu, “Solari ni kocha mwenye uzoefu na weledi wa kazi, lakini tupo hapa kuzungumzia mchezo ulioisha,” alisema.

Solari alikuwa bila ya wachezaji sita muhimu ambao huwa wanaanza katika mchezo huo wa jana Jumapili na kushuhudia wakipindua matokeo baada ya Valladolid kuanza kupachika bao Anuar Mohamed Tuhami kabla ya Raphael Verane, Luka Modric na Karim Benzema aliyefunga mawili kuipa ushindi Real Madrid.

Kama ilivyoripotiwa awali ushindi huo bado haujamuweka sehemu salama kocha Solari kwani uongozi wa Real Madrid umeendelea kufanya juhudi za kumtafuta kocha mwingine, kwani tayari wameshamfuata Zinedine Zidane lakini amegoma kurejea klabuni huku taarifa zikisema kuwa wapo kwenye mpango pia wa kumrudisha kwenye klabu kocha Jose Mourihno.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.