Singano akishangilia moja ya bao
Ligi Kuu

Natamani kumuona Singano wa Simba chini ya Cheche.

Sambaza....

Ni siku nyingi zimekatika kiasi kwamba nikisikia mtu anasema “muda unaenda kasi” ni rahisi sana kumuamini. Ni kama miaka mitano hadi sita kutoka pale yule Ramadhani Singano, wenyewe walimuita MESSI kuwa mchezaji tegemeo ndani ya wekundu wa msimbazi.

Akiwa kama kijana aliyelelewa na wekundu wa msimbazi toka miaka ya 2009, aliitumikia klabu hiyo mpaka mwaka 2015, pale alipoamua kutimkia Azam Fc, baada ya mkataba wake kukumbwa na utata mwingi.

Miongoni mwa matukio ninanyoyakumbuka ni lile la Mwanachama wa siku nyingi wa Simba, Musley Luwah, kumpa gari kama zawadi kutokana na kiwango safi na nidhamu awapo uwanjani.

Alipewa Gari aina ya Suzuki Carry 4WD, kipindi hicho Singano alikuwa kinda wa miaka 21 tu, aliliotumia gari hilo kubebea mizigo na kumuingizia fedha nyingi.

Nakumbuka ni ndani ya mwezi huo huo Singano alionyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa watani wa jadi (nani mtani jembe), Simba ikiiibuka na ushindi wa goli 3-1, alisababisha penati na hata kadi nyekundu kwa Kelvin Yondani.

Matatizo ya kimkataba yalimfanya Singano kuanza kuytafuta njia mbadala. Utata wa mkataba wake, ulisababisha maamuzi yafanywe na TFF, Messi alidai kuwa Simba wamegushi mkataba, kwani anavyojua yeye mkataba wake umemalizika wakati huo huo Simba kupitia kwa mwenyekiti wa kamati ya usajili kipindi hicho, Zacharia Hans Pop wakidai kuwa mkataba wake bado.

Kesi hiyo ilitatuliwa na TFF na Singano kuonekana ana haki ya kuvunja mkataba kwakuwa Simba walishindwa kutimiza baadhi ya masharti ya kimkataba ikiwemo suala la kupewa nyumba.

Siku mbili baadae Julai 9 mwaka 2015, Singano alitangazwa rasmi kuwa mchezaji wa Azam akisainishwa kandarasi ya miaka miwili.

Baada ya kuhamia Azam, Singano hakuwa na muendelezo mzuri wa kiwango chake kama alivyokuwa amezoeleka kule Msimbazi. Kuna kipindi hadi nilikuwa nawaza huenda ni laana za baba mlezi “Simba” , nakumbuka na hili lilikuwa ni pigo takatifu kwa wekundu wa Msimbazi.

Akiwa Azam Fc, kikosi chenye thamani ya Euro 475,000 sawa na pesa halali za kitanzania shilingi bilioni 12, alipitia vipindi vingi vya misuko suko chini ya makocha Stewart Hall baada ya kumpokea Joseph Omog, Zeben Hernandez, hans Van Pluijm na sasa chini ya Muangalizi Idd Cheche.

Majeruhi yaliyomuandama muda mrefu yamekuwa ni mwiba mchungu kwa Singano, na hata alipokuwa fiti mifumo ya walimu ilimfanya asiwe chaguo la kwanza. Singano amekuwa akipata namba hasa baada ya kuja kwa Mholanzi, Hans Van Pluijm, hapo ndipo alianza kidogo japo kwa kuchechemea ukilinganisha na kiwango chake alichokuwa nacho miaka ya 2013 hadi 15.

Baada ya kumtimua Pluijm, Azam kwa sasa ipo chini ya Muangalizi (care- taker)  Iddi Cheche ambaye naye huwa kama sehemu ya benchi la ufundi kwa muda wote pale Azam. Azam tayari imeshashinda michezo yake yote miwili chini ya Cheche, Dhidi ya Rhino na African Lyon.

Katika mechi hizo mbili, nimeanza kumuona Singano akiwa Nusu ya Singano wa Simba. Kiwango hicho alichokionyesha kilinitia moyo kiasi cha kumkumbuka. Singano ambaye hana mwili mkubwa lakini ana akili za miguu, hasa ule anaotumia Messi wa Barcelona kuwaadabisha mahasimu wake.

Singano kulia, wakati akiwa Simba Sc

Natamani “dribbling skills” zake, huku akiwatambuka mabeki wa pembeni mmoja baada ya mwingine. Natamani kuiona mikimbio yake bila mpira kuelekea eneo la hatari la mpinzani, natamani kuona akifunga magoli ya dhahabu, kuliko anayofunga Ibrahim Ajib wa Yanga.

Azam chini Cheche, timu inaonekana ikifunguka, makosa ya kizembe yamepungua, mfumo umebadilika kidogo hasa katika nafasi ya kiungo, Mudathiru Yahya hachezei chini tena bali anasaidia kupandisha timu.

“wanapokuwa katika mazoezi, huwa nawaangalia kipi wanafanya wanapatia na kipi wanakosea, kwahiyo narekebisha baadhi ya vitu vichache japo muda hauruhusu lakini tutajitahidi kuhakikisha tunarekebisha lengo ni kupata ushindi” Maneno ya Idd Cheche

Nina imani na Cheche,ni kocha mzuri, hutumika kuiokoa Azam katika mazingira magumu, anamjua vizuri Singano, maana ni kama mtoto wake. Naamini kabisa atamrudisha Singano kundini, kumpa umaarufu sawa na kufananishwa na Clatus  Chama,Hassan Dilunga, Tshishimbi, Ajib, Jonas Mkude na Feisal Salum.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.