Ligi Kuu

Wananchi Washusha Dozi Nzito kwa Kagera, Aziz Ki Atuma Salamu Msimbazi

Sambaza....

Wananchi Yanga wameendelea kutakata na kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya alama tatu mbele ya “Wakata miwa” Kagera Sugar kwa kuwaangushia kipigo kizito.

Katika mchezo uliopigwa saa moja usiku katika Dimba la Azam Complex wageni Kagera Sugar wamekubali kipigo cha mabao matano kwa sifuri huku Stephen Aziz Ki akitupia bao tatu “hatrick” na mabao mengine yakifungwa na Fiston Mayele na Benard Morrison.

Aziz Ki akimpiga tobo mlinzi wa Kagera Sugar Abdallah Mfuko

Karamu ya mabao ya Yanga ilifunguliwa na Aziz Ki kwa mkwaju wa penati baada ya Fiston Mayele kuangushwa katika eneo la kumi na nane la Kagera na mlinzi Abdallah Mfuko. Aziz Ki tena alifunga bao la pili kwake na Yanga kwa mkwaju wa mbali kabla ya kipindi cha kwanza hakijamalizika

Fiston Mayele na Benard Morrison walifunga mabao yao katika dakika ya 50 na 85 kabla ya Aziz Ki tena kuhitimisha karamu hiyo ya mabao katika dakika ya 90 kuwapa Wananchi ushindi wa mabao matano kwa bila.

 

Kwa ushindi huo sasa Yanga wanafikisha alama 68 wakiwa kileleni na kuendelea kuwaacha Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 8 katika msimamo wa Ligi.

Baada ya ushindi huo mnono sasa Wananchi wanajiandaa na mchezo dhidi ya Watani ambapo tayari nyota Aziz Ki ameshatuma salamu kwa walinzi wa Simba na kipa Aishi Manula ambae alimtungua katika mchezo wa raundi ya kwanza.

Sambaza....